read

Aya 17 – 28: Watu Wa Peponi

Maana

Hakika wenye takua watakua katika Mabustani na neema, Wakifurahi kwa yale aliyowapa Mola wao. Na Mola wao atawalinda na adhabu ya Motoni.

Neno ‘wakifurahia’ tumelifasiri kutokana na neno fakihina ambalo pia lina maana ya kuwa njema nafsi. Maana zote mbili zinaendana na Pepo na neema. Lakini maana ya kufurahia inaafikiana zaidi na kauli yake Mwenyezi Mungu inayofuatia: Kuleni na kunyweni kwa raha.

Maana ni kuwa walimcha Mwenyezi Mungu duniani, naye amewakinga na adhabu ya Moto na amewafanyia Pepo kuwa ndio malipo yao.

Kuleni na kunyweni kwa raha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyatenda.

Nyinyi wacha Mungu, mna haki zaidi ya neema hii, kwa sababu mlifanya kwa ikhlasi. Aya inafahamisha kuwa hakuna heshima yoyote mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kiumbe isipokuwa kwa kufanya amali. Ama vyeo nasaba na mali si chochote, ila zikiwa ni nyenzo za heri na masilahi ya umma.

Wakiegema viti vya fahari vilivyopangwa safu.

Kuegema viti pamoja na kuwa faragha, kunafahamisha kutokuwa na matatizo ya maisha na tabu zake.

Na tutawaoza mahurulaini, wanovutia akili na macho kwa uzuri wao na ukamilifu wao. Neema iliyoje!

Na walioamini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao.

Hakuna mwenye shaka kwamba watoto wadogo hawataadhibiwa kwa hali yoyote ile; ni sawa wazazi wao wawe wema au waovu, kwa sababu hakuna adhabu bila ya uasi, wala hakuna uasi bila taklifa. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemwondolea kalamu mtoto mdogo mpaka abaleghe.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekariri katika Aya kadhaa kauli yake: “Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine.” Juz. 8 (6:164).

Ama kauli ya anayesema kuwa mtoto wa kafiri ataingia motoni, kwa vile kama angeliishi basi angelifuata dini ya baba, kuali hii imeachwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu humuhisabu mtu kwa aliyoyatenda, wala hamuhisabu kwa ambayo angeliyatenda.

Unaweza kuuliza: Je, watoto wadogo watafufuliwa na kuingia Peponi?

Jibu: Hakuna njia ya kujua hilo isipokuwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Nabii wake. Akili hapa haina nafasi ya kuhukumu; wala hakuna katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu au Hadith mutawatir kwamba watoto wa makafiri watafufuliwa.

Kuna Hadith isemayo: “Hakika waumini wataongozwa kwa baba zao wenye takua siku ya kiyama.” Wafasiri wengi wamesema kuwa watoto wakubwa wa waumini katika kizazi cha wanaomcha Mwenyezi Mungu watakutanishwa na daraja za juu za mababa zao Peponi, hata kama amali zao njema ziko chini, ili wazazi waburudike nao. Wameitolea dalili kauli yao hiyo kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na wala hatutawapunja kitu katika vitendo vyao; yaani tutawazidisha karama mababa wala hatutawapunguzia mababa kitu chochote katika thawabu zao na daraja zao.

Shia Imamia, Hanafi, Shafii na Hambali wamesema kuwa mtoto atahukumiwa kuwa ni Mwislamu kutokana na mmoja wa wazazi wake. Akiwa mmoja ni mwislamu na mwingine ni kafiri, basi mtoto atahukumiwa kuwa ni Mwislamu, bila ya kuangalia aliye kafiri ni baba au mama. Lakini Malik wamesema unaozingatiwa ni Uislamu wa baba tu, lakini mama hana athari yoyote ya Uislamu kwa mtoto wake.

Kila mtu ni rehani wa alichokichuma. Yeye peke yake atafuatwa na matendo yake na kwayo ndio atakubaliwa nayo kesho kwa Mungu wala hataulizwa aliyotenda mwingine.

Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyopenda.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehusisha kutaja matunda na nyama, kwa sababu ndio vyakula vikuu.

Watapeana humo bilauri zisio na (vinywaji) vya upuuzi wala dhambi.

Watakunywa vinywaji vya kuchangamsha, lakini visivyokuwa na ulevi au vurugu wala kusababisha dhambi na kuchukuliana maneno.

Na watawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizofichwa.

Kusema kwake Mwenyezi Mungu ‘watumishi wao’ ni ishara yakuwa wao watafuata amri zao na makatazo yao.

Wataelekeana wakiulizana.

Wataulizana ilivyokuwa duniani, Vipi wamestahiki heshima hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu?

Umetangulia mfano wake katika Juz. 23 (37:50).

Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa.

Tulimwogopa Mwenyezi Mungu duniani kwa kuhofia ghadhabu yake na kutumai thawabu zake, Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani kwa rehema yake, akatuhusisha na neema yake na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto unaoambua ngozi na kuunguza nyuso.

Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu.

Duniani tulikuwa wema wenye huruma, na Mwenyezi Mungu huku Akhera amekuwa mwema kwetu na Mwenye huruma.

فَذَكِّرْ فَمَا أَنْتَ بِنِعْمَتِ رَبِّكَ بِكَاهِنٍ وَلَا مَجْنُونٍ {29}

Basi kumbusha! na wewe, kwa neema ya Mola wako, si kuhani wala mwendawazimu.

أَمْ يَقُولُونَ شَاعِرٌ نَتَرَبَّصُ بِهِ رَيْبَ الْمَنُونِ {30}

Au wanasema: mshairi, tunamtazamia kupatilizwa na dahari.

قُلْ تَرَبَّصُوا فَإِنِّي مَعَكُمْ مِنَ الْمُتَرَبِّصِينَ {31}

Sema: tazamieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika wanaotazamia.

أَمْ تَأْمُرُهُمْ أَحْلَامُهُمْ بِهَٰذَا ۚ أَمْ هُمْ قَوْمٌ طَاغُونَ {32}

Au akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao ni watu waasi?

أَمْ يَقُولُونَ تَقَوَّلَهُ ۚ بَلْ لَا يُؤْمِنُونَ {33}

Au wanasema: Ameitunga? Bali hawaamini tu.

فَلْيَأْتُوا بِحَدِيثٍ مِثْلِهِ إِنْ كَانُوا صَادِقِينَ {34}

Basi na walete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli.

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ {35}

Au wao wameumbwa pasipo kutokana na chochote Au wao ndio waumbaji?

أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَلْ لَا يُوقِنُونَ {36}

Au wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.

أَمْ عِنْدَهُمْ خَزَائِنُ رَبِّكَ أَمْ هُمُ الْمُصَيْطِرُونَ {37}

Au wanazo hazina za Mola wako, au wao ndio wenye madaraka?

أَمْ لَهُمْ سُلَّمٌ يَسْتَمِعُونَ فِيهِ ۖ فَلْيَأْتِ مُسْتَمِعُهُمْ بِسُلْطَانٍ مُبِينٍ {38}

Au wanayo ngazi ya kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja iliyo wazi!

أَمْ لَهُ الْبَنَاتُ وَلَكُمُ الْبَنُونَ {39}

Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi mna wavulana?

أَمْ تَسْأَلُهُمْ أَجْرًا فَهُمْ مِنْ مَغْرَمٍ مُثْقَلُونَ {40}

Au wewe unawaomba ujira, kwa hiyo wanaelemewa na gharama?

أَمْ عِنْدَهُمُ الْغَيْبُ فَهُمْ يَكْتُبُونَ {41}

Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wanaandika?

أَمْ يُرِيدُونَ كَيْدًا ۖ فَالَّذِينَ كَفَرُوا هُمُ الْمَكِيدُونَ {42}

Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini waliokufuru ndio watakaotegeka.

أَمْ لَهُمْ إِلَٰهٌ غَيْرُ اللَّهِ ۚ سُبْحَانَ اللَّهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ {43}

Au wanaye mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Ametakasika Mwenyezi Mungu na hao wanaowashirikisha naye.

وَإِنْ يَرَوْا كِسْفًا مِنَ السَّمَاءِ سَاقِطًا يَقُولُوا سَحَابٌ مَرْكُومٌ {44}

Na hata wangeona pande linatoka mbinguni linaanguka wangesema: Ni mawingu yaliyobebana.