read

Aya 18 – 32: Hud Na Swaleh

Maana

A’di walikadhibisha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo?

A’di ni kaumu ya Hud. Walimkadhibisha Nabii wao, Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa adhabu chungu. Akabainisha aina hii ya adhabu kwa kusema:

Hakika tuliwapelekea upepo mkali katika siku ya Nuhsi iendeleayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku ngumu na hatari. Uliendelea upepo wa adhabu siku hiyo mpaka ukawamaliza wote.

Ukiwaangusha watu kama vigogo vya mitende vilivyong’olewa.

Kimbunga kiliwang’oa kutoka sehemu zao na kuwatupa chini kama vigogo vya mtende vilivyong’olewa ardhini.

Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo?

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amelikariri hilo ili kusisitiza kutoa hadhari na maonyo.

Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?

Tazama Aya 17 ya sura hii tuliyo nayo, nuku yake na tafsiri yake ni moja tu.

Thamudi waliwakadhibisha waonyaji.

Thamud ni kaumu ya Swaleh. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameleta tamko la wengi pamoja na kuwa aliyekadhibishwa ni mmoja tu, Swaleh, kwa sababu kumkadhibisha Nabii mmoja ni sawa na kuwakadhibisha manabii wote, kutokana na kuwa risala ni moja na anayewatuma ni mmoja.

Wakasema: Je tumfuate mtu mmoja miongoni mwetu? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa!

Swaleh ni katika sisi na miongoni mwetu, tumemjua tangu utotoni na ukubwani, vipi tumfuate; wala hakuna anayemfuata na kumsadiki isipokuwa mpotevu. Ndio lau angelikuwa na mali, watumishi na wajakazi, ingelifaa kumfuata.

Ni yeye tu aliyeteremshiwa huo ukumbusho kati yetu?

Haiwezekani kabisa! Itakuwaje na yeye ni mmoja wetu:

وَلَئِنْ أَطَعْتُمْ بَشَرًا مِثْلَكُمْ إِنَّكُمْ إِذًا لَخَاسِرُونَ {34}

“Na nyinyi mkimtii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa hasarani.” Juz. 18 (23:34).

Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi!

Kwa mantiki yao ni kuwa inatosha kuwa ni mwongo kwa vile anatokana nao na ni miongoni mwao. Kwa hiyo suala ni aina ya mtu na wala sio haki na msingi.

Hili si geni! Ndio mantiki ya watu wa chumo na vyeo, kila mahali na kila wakati na vile vile mantiki ya wajinga na waigaji.

Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi, kuwa je, ni Swaleh au wale ambao wamemkadhibisha.

Ndio! Watajua karibu kwamba wao ndio wazushi pale Mwenyezi Mungu atakapowapa mtihani wa ngamia, kisha wamchinje na wapate ghadhabu na adhabu ifedheheshayo.

Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu.

Ni mtihani wa kuwapambanua muovu na mwema.

Basi watazame tu na usubiri.

Ngoja kidogo ewe Swaleh na uvumilie maudhi yao, utaona vile watakavyopatwa na adhabu.

Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu itahudhuriwa na atakayehusika.

Wape habari kuwa maji yatagawanywa baina yao na ngamia. Siku moja itakuwa yao na na nyingine ya ngamia.

Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja.

Hawakuwa radhi kugawana maji, ndio wakamwita yule muovu wao zaidi ili amchinje ngamia. Akaitikia yule muovu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Thamud walikadhibisha kwa sababu ya uovu wao. Alipofanya haraka muovu wao zaidi” (91:11-12). Basi walimchinja ngamia na adhabu ikawashukia.

Wametofautiana katika Makusudio ya neno ‘taatwa,’ tulilolifasiri kwa maana ya ‘akaja.’ Kuna waliosema kuwa Makusudio yake ni kuwa yule muovu alikunywa pombe kabla ya kuchinja. Wengine wakasema ni kuchukua ala ya kuchinjia. Sio mbali kuwa Makusudio yake hapa ni kuja bila ya kujali.

Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo?

Yalikuwa ni ya kubomoa. Kukaririka ni msisitizo wa kuhadharisha na kuonya

Hakika tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama majani makavu yaliyosagika yaliyo zizini.

Walipigwa na ukelele mmoja tu, wakawa kama majani makavu yaliyovunjikavunjika yanayopeperushwa na upepo. Mwenye Al-Manar anasema: “Mara nyingi neno Hashim hutumiwa kwa majani yaliyovunjika vunjika.”

Majani haya anayakusanya mwenye zizi kwa ajili ya wanyama wake. Kwa hiyo basi wasifa huu umekuja kwa njia ya majazi, (kufananisha). sio uhakika

Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?

Huenda akanufaika na kukaririka huku mwenye kupotea njia. Kimetangulia kisa cha Hud na Swaleh katika Sura ya Hud.

كَذَّبَتْ قَوْمُ لُوطٍ بِالنُّذُرِ {33}

Watu wa Lut waliwakadhibisha waonyaji.

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ حَاصِبًا إِلَّا آلَ لُوطٍ ۖ نَجَّيْنَاهُمْ بِسَحَرٍ {34}

Hakika tuliwapelekea kimbunga cha vijiwe. Isipokuwa wafuasi wa Lut. Tuliwaokoa karibu na alfajiri.

نِعْمَةً مِنْ عِنْدِنَا ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي مَنْ شَكَرَ {35}

Kwa neema inayotoka kwetu. Hivyo ndivyo tunavyomlipa anayeshukuru.

وَلَقَدْ أَنْذَرَهُمْ بَطْشَتَنَا فَتَمَارَوْا بِالنُّذُرِ {36}

Na hakika yeye aliwaonya mkamato wetu; lakini waliyatilia shaka hayo maonyo.

وَلَقَدْ رَاوَدُوهُ عَنْ ضَيْفِهِ فَطَمَسْنَا أَعْيُنَهُمْ فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ {37}

Na walimtaka awape wageni wake, tukayapofua macho yao. Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!

وَلَقَدْ صَبَّحَهُمْ بُكْرَةً عَذَابٌ مُسْتَقِرٌّ {38}

Na iliwafikia asubuhi adhabu ya kuendelea.

فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ {39}

Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِنْ مُدَّكِرٍ {40}

Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?

وَلَقَدْ جَاءَ آلَ فِرْعَوْنَ النُّذُرُ {41}

Na waonyaji waliwafikia watu wa Firauni.

كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كُلِّهَا فَأَخَذْنَاهُمْ أَخْذَ عَزِيزٍ مُقْتَدِرٍ {42}

Walizikadhibisha Ishara zetu zote, tukawashika mshiko wa Mwenye nguvu, Mwenye uweza.