read

Aya 33 – 41: Mtu Hatapata Ila Aliyoyafanya

Maana

Je, Umemwona yule aliyegeuka? Na akatoa kidogo, kisha akajizuia?

Yaani akazuia kutoa. Maana ni kuwa hebu niambie ewe Muhammad kuhusu mtu ambaye ameupa kisogo utajo wa Mwenyezi Mungu, na akawa ametoa kitu kidogo katika mali yake au nafsi yake katika njia ya Mwenyezi Mungu, kisha akajizuia kutoa!

Hii ndivyo inavyofahamisha dhahiri ya Aya. Kisha linakuja swali, kuwa je, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimkusudia mtu maalum aliyemjua Nabii (s.a.w.), au alikusudia mfano wa jumla kwa kila atakayekuwa na sifa hizi? Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa Aya hii ilimshukia Walid bin Al- Mughira, wengine wakasema ni Uthman Bin Affan. Kauli zote mbili zinahitajia dalili. Kwa hiyo basi Aya inabakia na ujumla wake na kuenea kwa kila mwenye sifa hizo.

Je, anayo ilimu ya ghaibu, basi ndio anaona?

Je, huyu mpingaji anayejizuia kutoa anajua kuwa yeye yuko kwenye amani ya adhabu ya siku ya kiyama mpaka akajasiri kupinga na kujizuia? Na atakuwa ameitoa wapi ilimu hii na hali Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameteremsha katika Kitabu yanayokadhibisha madai yake kama atadai hivyo?

Au hakuambiwa yaliyomo katika Vitabu vya Musa? Na vya Ibrahimu aliyetimiza ahadi?

Hakusikia mpinzani huyu aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu katika Tawrat na maandishi ya Ibrahim ambaye alitimiza ahadi kwa njia ya ukamilifu. Hakusikia kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha katika vitabu viwili hivi, kwamba habebi mbebaji mzigo wa mwingine?

Yaani kila mtu ataadhibiwa kwa dhambi zake na hakuna atakayembebea madhambi yake.

Aya hii imekaririka katika Juz. 8 (6:164), Juz. 15 (17:15), Juz. 22 (35:18) na Juz. 23 (39:7).

Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyoyahangaikia.

Makusudio ya kuhangaika hapa ni kufanya amali na harakati katika maisha haya. Aya hii inafahamisha wazi kuwa dini ya Uislamu ni dini ya maisha, kwa sababu inaelezea waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu anawangalia waja wake kupitia matendo yao katika maisha ya dunia na anaamiliana nao kwa mujibu wake.

Maana yake ni kuwa kila atakavyofanya mtu kwa ajili ya heri yake na akatatua matatizo yake atakuwa amekuwa karibu na Mwenyezi Mungu na dini ya Mwenyezi Mungu na atastahiki rehema na karama.

Na kadiri atavyoyakimbia maisha akajiweka mbali na matatizo yake kwa kutosheka na takbira, tahalili, kufunga na kuswali, basi atakuwa amejiweka mbali na Mwenyezi Mungu na dini yake na rehema yake.

Na kwamba mahangaiko yake yataonekana.

Yaani Mweneyzi Mungu atamuhisabu kwa mujibu wa matendo yake Siku ya Kiyama. Makusudio ya kuonekana hapa ni kuhisabiwa; vinginevyo ni kuwa Mweneyzi Mungu (s.w.t.) anajua kila kitu hata mawazo na wasiwasi.

Kisha ndio atalipwa malipo yake kwa ukamilifu.

Iko wazi haihitaji tafsiri, ni sawa na kauli yake Mweneyzi Mungu Mtukufu:

أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِنْكُمْ مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَىٰ ۖ {195}

“Kwamba mimi sitapoteza amali ya mfanya amali miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke.” Juz. 4 (3:195).

وَأَنَّ إِلَىٰ رَبِّكَ الْمُنْتَهَىٰ {42}

Na kwamba kwa Mola wako ndio mwisho.

وَأَنَّهُ هُوَ أَضْحَكَ وَأَبْكَىٰ {43}

Na kwamba Yeye ndiye anayeleta kicheko na kilio.

وَأَنَّهُ هُوَ أَمَاتَ وَأَحْيَا {44}

Na kwamba Yeye ndiye anayefisha na kuhuisha.

وَأَنَّهُ خَلَقَ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالْأُنْثَىٰ {45}

Na kwamba Yeye ndiye aliyeumba jozi, dume na jike,

مِنْ نُطْفَةٍ إِذَا تُمْنَىٰ {46}

Kutokana tone la manii linapomiminwa.

وَأَنَّ عَلَيْهِ النَّشْأَةَ الْأُخْرَىٰ {47}

Na kwamba ni juu yake ufufuo mwengine.

وَأَنَّهُ هُوَ أَغْنَىٰ وَأَقْنَىٰ {48}

Na kwamba ni Yeye ndiye anayetosheleza na anayetajirisha.

وَأَنَّهُ هُوَ رَبُّ الشِّعْرَىٰ {49}

Na kwamba hakika Yeye ndiye Mola wa Shii’ra.

وَأَنَّهُ أَهْلَكَ عَادًا الْأُولَىٰ {50}

Na kwamba Yeye ndiye aliyewaangamiza A’di wa kwanza.

وَثَمُودَ فَمَا أَبْقَىٰ {51}

Na Thamudi hakuwabakisha.

وَقَوْمَ نُوحٍ مِنْ قَبْلُ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا هُمْ أَظْلَمَ وَأَطْغَىٰ {52}

Na kabla yao kaumu ya Nuh. Na hao hakika walikuwa ni madhalimu zaidi, na waasi zaidi.

وَالْمُؤْتَفِكَةَ أَهْوَىٰ {53}

Na miji iliyopinduliwa, ni Yeye aliyeipindua.

فَغَشَّاهَا مَا غَشَّىٰ {54}

Vikaifunika vilivyofunika.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكَ تَتَمَارَىٰ {55}

Basi neema gani ya Mola wako unayoifanyia shaka?

هَٰذَا نَذِيرٌ مِنَ النُّذُرِ الْأُولَىٰ {56}

Hili ni Onyo katika maonyo yale yale ya zamani.

أَزِفَتِ الْآزِفَةُ {57}

Tukio la karibu limekurubia.

لَيْسَ لَهَا مِنْ دُونِ اللَّهِ كَاشِفَةٌ {58}

Hapana wa kulifichua isipokuwa Mwenyezi Mungu.

أَفَمِنْ هَٰذَا الْحَدِيثِ تَعْجَبُونَ {59}

Je, mnayastaajabia maneno haya?

وَتَضْحَكُونَ وَلَا تَبْكُونَ {60}

Na mnacheka wala hamlii?

وَأَنْتُمْ سَامِدُونَ {61}

Nanyi mmeghafilika?

فَاسْجُدُوا لِلَّهِ وَاعْبُدُوا ۩ {62}

Basi msujudieni Mwenyezi Mungu, na mumwabudu.