read

Aya 41 – 56: Na Wa Kushoto

Maana

Na wa kushoto; je, ni yapi ya wa kushoto.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kwanza, ametaja malipo makubwa aliyowandalia waliotangulia, kisha rehema na thawabu alizowaandalia wa kuume. Sasa, katika Aya hizi tulizo nazo anataja aina kwa aina ya adhabu itakayowapata watu wa kushoto; miongoni mwazo ni kuwa wao watakua katika upepo wa moto, na maji yanayochemka. Upepo wa moto utavutwa ndani ya mwili na kuchemsha nyama na damu na watakunywa maji yanayochemka tumboni.

Na kivuli cha moshi mweusi.

Neno moshi mweusi tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu yahmum ambalo pia lina maana ya weusi tititi wa kitu chochote na pia moshi mwingi. Maana yanafaa kwa moja wapo au yote pamoja

Si baridi wala starehe.

Ni kivuli lakini hakileti baridi wala kukinga joto, sawa na anayekimbilia kwenye mchanga wa kuchoma.

Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa.

Walipetuka mipaka wakawafanyia uovu waja wa Mwenyezi Mungu na miji yao; wakapora riziki za viumbe na wakastarehe kadiri walivyotaka, kuanzia mavazi ya gharama, chakula kitamu, kinywaji kinachoshuka hadi makazi ya fahari. Basi malipo mbele ya Mwenyezi Mungu yamekuwa ni adhabu ya kuungua, kinywaji cha moto, chakula cha zaqqum, upepo wa kuunguza na kivuli ni moshi.

Na walikuwa wakishikilia kiapo kikubwa.

Imesemekana kuwa ni madhambi makubwa. Lakini kauli ya kiapo chao cha uongo kuwa hakuna ufufuo wala malipo, ndiyo iliyo karibu; kama alivyowasimulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) pale aliposema: Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vya nguvu (kwamba) Mwenyezi Mungu hatawafufua wafu.” Juz. 14 (16:38).

Kiapo chao hiki ni matokeo ya shirki yao, kwa hiyo basi inafaa kufasiri Aya tuliyo nayo kwa maana ya shirki.

Na walikuwa wakisema: Tutakapokufa na tukawa udongo na mifupa, ati ndio tutafufuliwa? Au baba zetu wa zamani?

Walisema, kwa madharau, kuwa kweli mchanga unaweza kugeuka kuwa mtu? Wamesahau kuwa Mungu aliwaumba kutokana na mchanga kisha tone la manii.

Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho, bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu.

Waambie ewe Muhammad! Ndio, Mwenyezi Mungu atawakusanya kesho viumbe ili kuchambua hisabu na malipo ya matendo. Au kama Mwenyezi Mungu angeliwaacha tu hivi hivi bila ya makemeo wala maswali, angelikuwa ni dhalimu na anayefanya mchezo. Ametukuka sana Mwenyezi Mungu na wanayoyasema madhalimu.

Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; zikiwemo: Juz. 13 (13:5), Juz. 15 (17:49) na Juz. 18 (23:81-83).

Kisha nyinyi, mliopotea, mnaokadhibisha, Mmepotea mkaacha njia ya haki, mkaikanusha haki na mkabishana kijinga, basi malipo yenu kwa yakini mtakula mti wa Zaqqum. Na kwa huo mtajaza matumbo.

Sisi hatujui mti huu na kuna mengi tusiyoyajua, lakini tuna uhakika kuwa unaashiria, adhabu mbaya. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amefananisha mashada yake na vichwa vya shetani. Tazama Juz. 22 (37:62).
Na juu yake mtakunywa maji yanayochemka.

Chakula chao ni kichungu kuliko shubiri, kinanuka kuliko mzoga na kinywaji chao ni chumvi.

Tena mtakunywa kama wanavyokunywa ngamia wenye kiu.

Neno kiu tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu him ambalo lina maana ya ngamia mwenye kiu au ugonjwa wa kiu kisichokwisha.

Hii ndiyo karamu yao Siku ya Malipo.

Hii ni ishara ya hali ya watu wa kushoto. Siku ya malipo ni siku ya kiyama. Karamu ni chakula na kinywaji anachoandaliwa anayekuja. Ni karamu mbaya ya kinywaji, kivazi na hata malazi. Fauka ya hayo mikono itafungwa shingoni na kukutanishwa utosi na nyayo. Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu na mwisho mbaya.

نَحْنُ خَلَقْنَاكُمْ فَلَوْلَا تُصَدِّقُونَ {57}

Sisi tumewaumba; basi mbona hamsadiki?

أَفَرَأَيْتُمْ مَا تُمْنُونَ {58}

Je, mnaiona mnayoitoneza?

أَأَنْتُمْ تَخْلُقُونَهُ أَمْ نَحْنُ الْخَالِقُونَ {59}

Je, mnaiumba nyinyi, au tunaiumba Sisi?

نَحْنُ قَدَّرْنَا بَيْنَكُمُ الْمَوْتَ وَمَا نَحْنُ بِمَسْبُوقِينَ {60}

Sisi tumewawekea mauti. Na Sisi hatushindwi,

عَلَىٰ أَنْ نُبَدِّلَ أَمْثَالَكُمْ وَنُنْشِئَكُمْ فِي مَا لَا تَعْلَمُونَ {61}

Kuwaleta wengine badala yenu na kuwaumba nyinyi kwa umbo msilolijua.

وَلَقَدْ عَلِمْتُمُ النَّشْأَةَ الْأُولَىٰ فَلَوْلَا تَذَكَّرُونَ {62}

Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, tena mbona hamkumbuki?

أَفَرَأَيْتُمْ مَا تَحْرُثُونَ {63}

Je, Mnaona mnayolima?

أَأَنْتُمْ تَزْرَعُونَهُ أَمْ نَحْنُ الزَّارِعُونَ {64}

Je, ni nyinyi mnayoyaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha?

لَوْ نَشَاءُ لَجَعَلْنَاهُ حُطَامًا فَظَلْتُمْ تَفَكَّهُونَ {65}

Tungelitaka tungeliyafanya mapepe, mkabaki mnastaajabu,

إِنَّا لَمُغْرَمُونَ {66}

Hakika sisi tumegharamika.

بَلْ نَحْنُ مَحْرُومُونَ {67}

Bali sisi tumenyimwa.

أَفَرَأَيْتُمُ الْمَاءَ الَّذِي تَشْرَبُونَ {68}

Je, mnayaona maji mnayoyanywa?

أَأَنْتُمْ أَنْزَلْتُمُوهُ مِنَ الْمُزْنِ أَمْ نَحْنُ الْمُنْزِلُونَ {69}

Je, ni nyinyi mnayoyateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha?

لَوْ نَشَاءُ جَعَلْنَاهُ أُجَاجًا فَلَوْلَا تَشْكُرُونَ {70}

Tungelipenda tungeliyafanya ya chumvi kali. Basi mbona hamshukuru?

أَفَرَأَيْتُمُ النَّارَ الَّتِي تُورُونَ {71}

Je, mnauona moto mnaouwasha?

أَأَنْتُمْ أَنْشَأْتُمْ شَجَرَتَهَا أَمْ نَحْنُ الْمُنْشِئُونَ {72}

Ni nyinyi mliouumba mti wake au Sisi ndio Wenye kuuumba?

نَحْنُ جَعَلْنَاهَا تَذْكِرَةً وَمَتَاعًا لِلْمُقْوِينَ {73}

Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa wenye kusikiliza.

فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ {74}

Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.