read

Aya 42 – 62: Kwa Mola Wako Ndio Mwisho

Maana

Na kwamba kwa Mola wako ndio mwisho.

Aya hii na zinazofuatia bado zinaungana na zile alizosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwa ziko katika vitabu vya Musa na Ibrahim. Makusudio ya mwisho ni kusimama mtu mbele ya Mola wake kwa ajili ya hisabu ambayo hataepukana nayo.

Na kwamba Yeye ndiye anayeleta kicheko na kilio.

Kicheko ni ishara ya furaha ya watu wa Peponi na kilio ni huzuni ya watu wa motoni. Inawezekana kuwa ni ishara ya silika ya ladha, uchungu, huzuni na furaha aliyompa Mwenyezi Mungu mtu.

Watu wa falsafa wanasema kuwa mtu hawezi kutaharaki isipokuwa kwa mvuto wa ladha; kama vile tendo la ndoa au kwa kuhofia maumivu; kama vile njaa.

Maada Na Maisha

Na kwamba Yeye ndiye anayefisha na kuhuisha.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye anayetoa uhai na kuuchukua. Ama kauli ya mwenye kusema maada ndio asili ya uhai na ndiyo iliyousababisha, hayo ni madai tu yanayokataliwa na msingi wa akili. Kwa sababu maada haina harakati kwa maumbile yake mpaka ipate sababu ya kuibadilisha.

Ni nani mwenye akili anayeweza kukubali kuwa maada pofu imejitengenezea yenyewe macho, masikio na moyo? Ikiwa uhai ni sifa ya maada kwanini kukatokea kukua, harakati, hisia na kufikiri katika baadhi tu, na kwingine kusitokee?

Ikiwa mtu atajibu kuwa baadhi ya maada zina maandalizi ya uhai na nyingine hazina, tutamuuliza: Je, tofauti hii imetoka wapi? Kutoka ndani ya maada yenyewe au kutoka nje? Ikiwa imetoka ndani basi ni lazima kila maada iwe na uhai; vinginevyo itakuwa kitu kimoja kimesababisha kupatikana na kukosekana kwa wakati mmoja. Na ikiwa imesabishwa na sababu ya nje, basi hivyo ndivyo tusemavyo.

Na kwamba Yeye ndiye aliyeumba jozi, dume na jike kutokana tone la manii linapomiminwa.

Mwanamume anashusha manii yake katika mfuko wa uzazi, mimba inatungwa na anapatikana mtoto wa kike au wa kiume. Ni nani basi aliyeleta maandalizi ya mbegu hii mwilini? Ni nani aliyeleta mamilioni ya chembe hai? Je, wataalamu wanaweza kutengeneza chembe moja itakayotoa mtoto wa kike au wa kiume? Bali je, wanaweza kutofautisha chembe itakayotengeneza mtoto wa kiume au wa kike? Ikiwa mbegu za uzazi zinategemea sababu za maumbile, basi sababu hizi zinaishia kwa yule aliyetengeneza maumbile.

Na kwamba ni juu yake ufufuo mwengine.

Juu yake ni juu ya Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa ufufuo hauna budi kuweko.

Na kwamba ni Yeye ndiye anayetosheleza na anayetajirisha.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewapa waja wake na akawafanya wajitosheleze bila ya kuwa na haja ya kuomba wengine na wengine akawapa ya kuwatosheleza na ziada ya kuweka akiba. Mmoja wa wataalamu anasema: “Mwenye kuonja ladha ya kujitosheleza atakuwa amepata fungu la kujitosheleza na kwamba hilo lina utukufu.’’

Na kwamba hakika Yeye ndiye Mola wa Shii’ra.

Shiira (Sirius) ni nyota inayoangaza. Mwenyezi Mungu amehusisha kuitaja hapa kwa sababu watu wa wakati wa jahilia walikuwa wakiiabudu. Imesemekana kuwa ni kubwa kuliko Jua kwa mara ishirini na kwamba iko mbali na jua kwa mara milioni zaidi ya sisi tulivyo mbali na Jua.

Na kwamba Yeye ndiye aliyewaangamiza A’di wa kwanza.
Hao ni watu wa Hud. Mazungumzo kuwahusu yamekwishapita huko nyuma mara kadhaa. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewasifu kuwa wa kwanza kutokana na wale waliokuja baada yao katika umma. Mwenye Majmaulbayan anasema ni kwa sababu walikuja A’di wengine.

Na Thamudi hakuwabakisha, yeyote katika wao.

Hao ni watu wa Swaleh. Vile vile yametangulia maelezo yao na ya watu wa Nuh ambao amewaashiri Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kusema: Na kabla yao kaumu ya Nuh. Na hao hakika walikuwa ni madhaalimu zaidi, na waasi zaidi kuliko A’di na Thamud.

Na miji ya kaumu ya Lut iliyopinduliwa, ni Yeye aliyeipindua akaiza- misha ndani ya ardhi.

Vikaifunika vilivyofunika kwa adhabu.

Basi neema gani ya Mola wako unayoifanyia shaka?

Maneno yanaelekzwa kwa kila mtu.

Hili ni onyo katika maonyo yale yale ya zamani.

Wafasiri wengi wamesema kuwa ‘Ishara’ hapa ni ya Qur’an au Muhammad (s.a.w.), kwa hiyo isemwe Hii au Huyu.

Hakuna mwenye shaka kuwa Qur’an na Muhammad (s.a.w.) ni katika maonyo ya mwanzo, lakini pamoja na hayo, tunavyofahamu ni kuwa Mwenyezi Mungu ameashiria yale aliyoyataja miongoni mwa dalili na mawaidha yaliyokusanya mambo muhimu yanayotakikana kuchunguzwa na kuwa ni mafunzo; kama maswala ya kuwa kila mtu peke yake ndiye mwenye majukumu ya makosa yake, kwamba Mwenyezi Mungu anamwangalia kupitia matendo yake, kuwa hakuna chimbuko la uhai isipokuwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu tu peke yake na mwisho wa waasi ni maangamizi.

Haya na mengineyo mfano wake ni miongoni mwa maudhui muhimu ya ulimwengu na binadamu. Anapoyataja Mwenyezi Mungu (s.w.t.), ili kumfahamisha mtu kuwa Mwenyezi Mungu yuko na ni mkuu, itakuwa kutajwa kwake hasa kunaashiria kuwa maana yake na malengo yake yanajitokeza kwa wataalamu na kwamba wao ndio wana haki zaidi ya kumjua Mwenyezi Mungu, kumwamini na kumcha:

إِنَّمَا يَخْشَى اللَّهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ  {28}

“Hakika si mengineyo, wanaomcha Mwenyezi Mungu katika waja wake ni wale wajuzi.”
Juz. 22 (35:28).

Tukio la karibu limekurubia.

Makusudio ya tukio hapa ni Kiyama. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameliisifu kuwa linasogea, kwa vile linakuja na kila linalokuja liko karibu na kila lililopita ni kama halikuwako.

Hapana wa kulifichua isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Kulifichua ni hilo tukio la karibu; yaani Kiyama. Unaweza kufasiri kufichua kwa maana ya ilimu; kama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِنْدَ رَبِّي ۖ لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ۚ {187}

Wanauliza hiyo Saa (Kiyama) kutokea kwake kutakuwa lini? Sema: Ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha kwa wakati wake ila yeye tu.” Juz. 9 (7:187).

Pia unaweza kufasiri kwa kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

مِنْ قَبْلِ أَنْ يَأْتِيَ يَوْمٌ لَا مَرَدَّ لَهُ مِنَ اللَّهِ ۖ {43}

“Kabla ya kufika siku isiyozuilika inayotoka kwa Mwenyezi Mungu.” Juz.21 (30:43).

Je, mnayastaajabia maneno haya na mnacheka?

Mananeno haya ni haya mazungumzo ya Kiyama. Imesemkana ni Qur’an. Tafsri zote mbili ni sawa, kwa sabau makafiri walistahajabu ufufuo:

 فَقَالَ الْكَافِرُونَ هَٰذَا شَيْءٌ عَجِيبٌ {2}

أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا ۖ ذَٰلِكَ رَجْعٌ بَعِيدٌ {3}

“Na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu! Je, tukifa na tukawa udongo? Marejeo hayo ni ya mbali!” Juz. 26 (50:2-3).

Pia waliistaajabu Qur’an:

أَوَعَجِبْتُمْ أَنْ جَاءَكُمْ ذِكْرٌ مِنْ رَبِّكُمْ {63}

Je, mnastaajabu kuwafikia mawaidha kutoka kwa Mola? Juz. 8 (7:63).

Wala hamlii? Nanyi mmeghafilika?

Ilikuwa bora mzililie nafsi zenu ambazo mmezidhulumu kwa ukafiri na dhulma:

فَلْيَضْحَكُوا قَلِيلًا وَلْيَبْكُوا كَثِيرًا جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ {82}

“Basi nawacheke kidogo na walie sana, ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.”
Juz. 10 (9:82)

Basi msujudieni Mwenyezi Mungu, na mumuabudu.

Hanafi, Shafi, Shia Imamia na Hambali wamesema ni wajibu kusujudi wakati wa kusomwa Aya hii, kwa sababu Mtume (s.a.w.) alisujudi wakati wa kusomwa kwake na walisujudi waliokuwa pamoja naye, lakini Maliki wakasema kuwa siwajibu.