read

Aya 45 – 49: Basi Waache Mpaka Wakutane Na Siku Yao

Maana

Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakaangamizwa.

Bado maneno yanendelea kuhusiana na waliomkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Maana ni kuwa usijali ewe Muhammad na ukadhibishaji wao na inadi yao, kwani watafikiwa na siku isiyokuwa na kimbilio la kuepuka maangamizi na adhabu chungu.

Siku ambayo hila zao hazitawafaa kitu, wala wao hawatanusuriwa.

Yaani hakutakuwa na hila ya kujikinga siku hiyo wala hakutakuwa na usaidizi.

Na hakika waliodhulumu watapata adhabu nyengine isiyokuwa hiyo.

Yaani wataadhibiwa adhabu nyingine kabla ya siku ya kiyama. Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa hiyo ni adhabu ya kaburi. Wengine wakasema ni yaliyowapata siku ya vita vya Badr. Ama sisi tunayanyamazia aliyoyanya- mazia Mwenyezi Mungu.

Lakini wengi wao hawajui kuwa madhalimu wataadhibiwa kabla ya siku ya Kiyama na ndani ya Siku ya Kiyama.

Na ingojee hukumu ya Mola wako. Kwani wewe hakika uko machoni mwetu.

Makusudio ya hukumu ya Mwenyezi Mungu hapa ni kuwapa muda madhalimu mpaka siku yao waliyoagwa. Machoni mwetu ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), yuko katika hifadhi ya adha ya maadui na vitimbi vyao.

Na msabihi kwa kumsifu Mola wako unaposimama na usiku pia msabihi, na zinapokuchwa nyota.

Mdhukuru Mwenyezi Mungu katika hali zote kwani kumdhukuru yeye ndio dhikri nzuri. Na amewahidi wenye kumdhukuru ahadi ya ukweli.