read

Aya 46 – 78: Hakuna Malipo Ya Hisani Ila Hisani

Maana

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuhofisha na kumpa kiaga yule mwenye kupetuka mipaka na akafanya uovu, sasa anamtuliza yule mwenye takua na akalisadikisha tamko jema, na kumwahidi Pepo iliyo na sifa kubwa kwa chakula chake, kinywaji chake, huri laini wake, miti yake, mito yake, samani zake na vipambo vyake kwa namna ambayo haina mfano wala hatuijui.

Nyingi katika Aya hizi ziko wazi hazihitajii tafsiri; mbali ya kuwa ni kukariri yaliyotangulia. Kwa hiyo tutafupiliza tafsiri ila kukiwa na haja ya kurefusha.

Na mwenye kuogopa kusimama mbele ya Mola wake atapata Bustani mbili.

Makusudio ya kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu ni kuwa yeye ni msimamizi wa kila nafsi akijua siri yake na dhahiri yake. Imepokewa kutoka kwa Imam Ja’far Assadiq (a.s.) amesema: “Mwenye kujua kuwa Mwenyezi Mungu anamuona na kusikia anayoyasema, na likamzuia hilo kufanya maovu, atakuwa ameogopa kusimama mbele ya Mola wake.”

Wafasiri wana kauli kadhaa kuhusu maana ya Bustani mbili. Iliyo karibu zaidi na ufahamu ni bustani katika Pepo, kwa sababu neno Pepo limefasiriwa kutoka neno la kiarabu janna lenye maana ya bustani. Hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu katika wasifu wake zenye matawi yaliyotanda; yaani matawi yenye majani na matunda.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Je, nyinyi majini na watu mnakanusha neema hizi tulizozitaja. Kila swali linalokuja kwa tamko hili, basi inayoulizwa ni neema aliyoitaja Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kabla ya swali; kwa hiyo hakuna haja ya kutaja na kubainisha kinachouliziwa.

Ndani yake zimo chemchem mbili zinazopita.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Maana yako wazi, lakini pamoja na hayo mfasiri mmoja amesema: kupita maana yake ni kutawanyika. Mwingine akasema: yaani zinapita baina ya miti. Wa tatu akasema chemchem moja inaitwa tasnim na nyingine inaitwa salsabil.

Wanne naye akasema: zinapita ni kwa ambaye macho yake yanatiririka machozi kwa kumhofia Mwenyezi Mungu.

Hakuna chimbuko la tafsiri hizi isipokuwa hamu ya kusema tu. Kwa nini wana hamu ya kusema? Ni kwa vile tu wao ni wafasiri.

Humo katika kila matunda zimo namna mbili.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Tunda moja linaweza kuwa na aina mbili; kama zabibu kavu na mbichi, tende mbichi na za kuiva1 na matofaha ya tamu na yasiyokuwa tamu.
Wakiegemea matandiko yenye vitambaa vya hariri nzito; na matunda ya Bustani hizo yapo karibu.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili? Mfano wake ni Aya isemayo: “Vishada vyake viko karibu.” (69:23).

Humo watakuwamo wanawake watulizao macho; hajawagusa mtu kabla yao wala jini.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Humo, ni humo Peponi; na kabla yao, ni kabla ya hao waume wa Hurilaini. Maana ni kuwa Hurilaini hawataangalia isipokuwa waume zao, pia watakuwa ni bikra kama walivyumbwa.

Kama kwamba wao ni yakuti na marijani kwa urembo na uzuri.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Ujira Ni Haki Na Ziada Ni Fadhila

Hakuna malipo ya ihsani ila ihsani?

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Kila wanaloliona watu kuwa ni hisani au wema basi kwa Mwenyezi ni hivyo hivyo, kwa Sharti yakuwa lisikataliwe na akili iliyo salama wala kukatazwa na sharia; kama ilivyokuwa wakati wa jahilia, walikuwa wakiona ni wema na jambo zuri kuabudu masanamu na kuwadhulumu wanyonge, hasa wanawake.

Mpaka leo hii bado kuna mamilioni ya watu wanaoona ni hisani kuabudu masanamu na watu wakimfanya Mwenyezi Mungu ana watoto na washirika. Hakuna mwenye shaka kuwa hii ni desturi mbaya sana.

Ikiwa mtu atafanya jambo na watu wakaliona ni zuri na lisikataliwe na akili na sharia, basi mwenye kuilifanya anastahiki ujira na karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu na atamzidisha ziada ya anayostahiki:

لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ {26}

“Kwa wafanyao wema ni wema na ziyada.” Juz. 11(10:26).

Kundi katika wanatiolojia wamesema kuwa thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa tendo la wajibu ni fadhila sio malipo wala haki. Wengine wakasema, bali ni malipo na haki.

Imam Ali (a.s.) anasema: “Ingelikuwa kuna yeyote mwenye haki lakini wengine hawana haki juu yake, ingelikuwa hivyo kwa Mwenyezi Mungu tu peke yake, sio kwa viumbe wake, kutokana na uwezo wake kwa waja wake na kwa uadilifu kwa kila linalopita katika hukumu yake.

Lakini amejaalia haki yake kwa waja wake ni kumtii na akajalia malipo yao yawe juu yake, kwa kuwaongezea malipo kwa fadhila na kupanua ile ziyada kwa wanaostahiki.”

Maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu ana haki yake naye anayo haki ya wengine. Hakuna linalofahamisha hivyo kuliko kauli hiyo ya Imama Ali (a.s.).

Kwa hiyo haki ya Mwenyezi Mungu ni kutiiwa na waja wake na haki ya watiifu kwake, Yeye ambaye imetukuka hikima yake, ni malipo kulingana na matendo. Zaidi ya hayo ni fadhila kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hii inaafikiana na hukumu ya kiakili na maumbile, kwani watu wote wanaona ni fadhila na hisani ukimlipa aliyekufanyia kazi zaidi ya malipo yake na stahiki yake. Lakini ukimlipa bila ya ziada wala upungufu basi wewe ni mtekelezaji, lakini sio mhisani wala makarimu.

Zaidi ya hayo Uislamu, kwa misingi yake na matawi yake, unajengeka kwenye fikra ya uadilifu. Na ujira wa kazi ni haki ya wajibu kuitekeleza katika mantiki ya uadilifu na hukumu yake.

Zaidi ya hizo mbili ziko Bustani mbili nyingine.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Yaani katika Pepo kuna kuzidiana kulingana na imani za waumini na kutofautiana na matendo yao. Haya ndiyo yanayopelekea mantiki ya haki na misingi ya uadilifu. Kwa hiyo inatubainikia kuwa Bustani mbili zilizotajwa mwanzo ni za wale wenye imani ya nguvu, wenye kazi iliyo na manufaa zaidi na wenye juhudi zaidi ya wengine, na hizi mbili zilizotajwa sasa ni za walio chini ya hapo.

Za kijani kibivu.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Yaani rangi yake inaeleka weusi kutokana na kuiva sana.

Mna chemchem mbili zinazofurika.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Yaani zinachimbuka maji. Ama zile zilizotajwa mwanzo maji yake yanapita. Kama ambavyo bustani mbili zilozitajwa mwanzo ni tofauti na zilizotajwa baadae vile vile chemchem.

Mna humo matunda, na mitende na komamanga.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa tende na komamanga sio matunda ndio maana kukawa na maunganisho. Razi anasema kuwa katika matunda kuna ya Ardhini, kama vile matango n.k. na kuna yaliyo kwenye miti, kama vile tende n.k. Kwa hiyo kuunganisha kunakuwa kwa mahususi kwenye jumla.

Wamo wanawake wema wazuri.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Yaani wazuri wa umbo na tabia.

Wanawake wazuri wanaotawishwa katika mahema.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Mwenye Majmaul’bayan anasema maana yake ni kutwawishwa kwenye makuba wanayojengewa wanawake wanaotawa nyumbani. Wengine wakasema kuwa makusudio ni mahema hasa; kwani yako mengine yanashinda majumba kwa uzuri. Kauli hii ndio iliyo karibu na dhahiri ya Aya.

Hajawagusa mtu kabla yao wala jini.

Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili? Yaani bado ni bikra. Imetangulia kwa herufi zake katika Aya 56 ya Sura hii. Wameegemea juu ya matakia ya kijani na mazulia mazuri.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?

Yaani kwenye mito ya kuegemea.

limekuwa na baraka jina la Mola wako, Mwenye utukufu na ukarimu.

Mwenyezi Mungu ana utukufu na ukubwa, ikiwa ni pamoja na ukarimu na fadhila kwa viumbe wake. Tazama kifungu cha ‘Mwenyezi Mungu na mtu na Ibn A-arabi’.

Katika Aya 27 ya sura hii tuliyo nayo.

  • 1. Katika lugha ya kiarabu hizi zina majina yake maalumu; kama inab na zabib, na tamri na rutab -Mtarjumu.