read

Aya 47 – 60: Kila Kitu Tumeumba Dume Na Jike

Maana

Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio wenye kutanua.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa Makusudio ya kutanua hapa ni kuwa Mwenyezi Mungu anaipanua riziki kwa viumbe wake kwa mvua.

Lakini maana yanayoafikiana na hali halisi na ufahamisho wa Aya, ni kuwa Makusudio ya ya mbingu ni kwa maana yake yaliyo dhahiri; kuwa ni anga pana iliyo na nyota n.k.

Na Makusudio ya kutanua ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaizidisha anga upana kila siku zinavyoendelea kupita.

Wataalamau wanasema kuwa anga inaendela kujivuta kadiri siku zinavyopita, na kwamba ukubwa wa anga ya ulimwengu hivi sasa ni mara kumi zaidi tangu ilipoanza kujivuta. Anasema Sir James Jeans:

“Umbali baina ya makundi ya nyota unafikia miaka milioni moja na nusu ya mwendo wa mwanga. Mwanga unakata masafa ya maili milioni 6 katika mwaka mmoja.”
Anasema Camus kuwa imegundulika kutokana na vipimo vikubwa kwamba baina ya nyota kuna masafa ya uwazi yanayokadiriwa kufikia miaka milioni 5 ya mwaka, na kwamba kumehisabiwa makao ya nyota yanayofikia milioni moja, na kuna uwezekano kuwa kuna mkusanyiko mwingine wa makao ya nyota katika masafa yaliyo mbali zaidi. Hayo yanapatikana katika kitabu Attakamul fil Islam, (ukamilifu katika Uislamu) cha Ahmad Amin Al-iraqi Juz. 2 Uk. 67 chapa ya kwanza.

Sisi hatuna hamasa ya Qur’an kuafikiana na sayansi kutokana na hadhari tulizozieleza katika Juz. 1 (2: 2). Lakini hata hivyo hatuwezi kuepuka kusema kuwa Aya hii tukufu ni usadikisho wa ushahidi kuwa muujiza wa Muhammad bin Abdillah (s.a.w.) ni wa pekee na wa milele kati ya miujiza ya manabii wote na kwamba unazidi kuwa wazi zaidi kadiri sayansi inavyopiga hatua.

Na ardhi tumeitandaza; basi bora ya watandazaji ni sisi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemwandalia mtu ardhi na akamkunjulia mkono wake humo ili ajenge na afanye mambo ya heri, sio shari na kubomoa. Amemwachia huru mkono wake ili afanye kazi na akampa masharti ya kuuzuia mkono huo dhidi ya ndugu yake binadamu, sio amrushie makombora na mabomu ya sumu kwenye shule za watoto, mahospitalini, na viwandani na kwa kila mwenye kuimba nyimbo ya uhuru na kukataa utumwa isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu tu peke yake.

Na katika kila kitu tumeumba dume na jike ili mzingatie.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameumba kila jinsi ya kitu katika viumbe vyote mke na mume; iwe ni binadamu, mnyama, mmea au vitu vigumu, kama mawe n.k. Kwa sababu neno ‘kila kitu’ linaenea kwa vyote.

Hatujui kama wataalamu wameigundua hakika hii au bado wako njiani? Tuliyoyasoma kutoka kwa wataalamu kuhusiana na maudhui haya ni kuwa hakuna chembe yoyote ulimwenguni ila inakuwa imefaungana na kani mbili: chanya na hasi (positive na negative). Yaani nguvu mbili za mvutano. Sijui kama Aya inaafikiana na hali hiyo?

Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.

Kila mwenye kuuzuia mkono wake na kuwaudhi wengine, akasadikisha kauli yake, akaifanyia ikhlasi haki na uadilifu katika vitendo vyake, atakuwa amaeikimbia batili kuiendea haki, atake asitake, lakini muongo mwenye hiyana, huyo ni katika maadui wakubwa wa Mwenyezi Mungu; ajaposoma tahalili na takbiri, akaabudu na kutoa sadaka.

Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokaye kwake.

Kuna aina nyingi za shirki; miongini mwazo: ni kuabudu masanamu, kumnasibishia Mungu mtoto, kuwa kigeugeu katika dini na kuwatumikia maadui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu kwa kutumia jina la uislamu na kuleta masilahi ya waislamu.

Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.

Wakadhibishaji walikwambia wewe, kama vile wa mwanzo walivyoaambia mitume wao.

Je, wameusiana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi.

Ni ajabu kufanana wa mwanzo na wa mwisho katika kuwakadhibisha wenye haki na viongozi wema. Je, walikongamana na kuusiana hilo? Hapana hawakukongamana wala hawakuonana au kuungana. Lililowakusanya ni uadui wa batili dhidi ya haki na ujinga dhidi ya ilimu.

Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi.
Usujitoe roho na kufuru yao na uasi wao ewe Muhammad! Wewe hutaulizwa kuhusu dini yao wala kauli zao na vitendo vyao.

Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini.

Umuhimu wako ewe Muhammad! Ni kufikisha Qur’an na kuwatolea mawaidha kwayo watu wote. Ikiwa hatanufaika na mawaidha mwenye kung’ang’ania ukafiri na ufisadi, basi atanufaika nayo mwenye kuitafuta haki ili aiamani na kuitumia kwa mujibu wake.

Na sikuwaumba majini na watu ila waniabudu.

Maana ya kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake ni kuwa huru kwa kutomwabudu mtu, mali, cheo na matamanio yote, na kutonyenyekea isipokuwa kwa haki tu na uadlifu.

Vile vile, kumwabudu Mungu, kunamaanisha kufanya juhudi ya kuinusuru haki na watu wake na kufanya mambo kwa ajili ya dunia na Akhera. Hakuna anayetia shaka kwamba mwenye kufuata njia hii itampeleka kwenye nyumba ya amani.

Kwa hiyo basi lengo la kuumbwa majini na watu ni kuishi maisha mema ya milele katika nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa sharti ya kujikomboa na aina zote za utumwa na kufanya mambo mema. Mwenye kupuuza na akazembea, asilaumu ila nafsi yake. Na Mola wako si mwenye kudhulumu waja.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 21(31:33-34), kifungu cha: ‘Kwa nini Mungu akamuumba mtu?’

Unaweza kuuliza: Utafanya nini na Hadith Qudsi inayosema: “Nilikuwa hazina iliyojificha nikataka nijulikane, basi nikaumba viumbe wakanijua,” si inafahamisha wazi kuwa lengo la kuumbwa ni kumjua Mungu?

Jibu: Hadith hii inaafikiana kwa ukamilifu na tafsiri tuliyoitaja. Kwa sababu mwenye kumjua Mwenyezi Mungu kisawasawa, hatahitajia kuwaabudu watu, cheo au mali na atafanya kulinga na radhi ya Mwenyezi Mungu na Pepo yake.

Sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe.

Ni kama Mwenyezi Mungu, aliyetukuka kabisa, anasema: Sikuwaumba viumbe ili niwatumie kwenye viwanda vyangu na mashamba yangu.

Wala si kwa kuwatuma sokoni kwenda kuniuzia bidhaa zangu; wala pia sikuwaumba kwa ajili ya kuwapiga vita wanaoshindana na mimi katika uporaji na ulanguzi.

Hapana! Mwenyezi Mungu ni mwenye kujitosha na walimwengu wote. Amewaumba ili tu wafanye amali kwa pamoja kwa ajili ya heri yao wote na wapigane jihadi na yule atayejaribu kuingilia uhuru wao, heshima yao na kupora mali zao, ardhi zao na majumba yao.

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti.

Maana ya kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuruzuku ni kuwa yeye aliye Mtukufu, amemuumbia mtu maisha na akampa nyenzo zitakazomwezesha kuvuna matunda kwa ajili ya maisha yake; kama vile akili, nguvu, usikizi na uoni, na akamwambia: shughulika kwa ajili ya dunia yako na Akhera yako, wala usifanye uchokozi, kwani Mwenyezi Mungu hapendi wachokozi.

Ni sawa na mtoto wako kama utampa mali na kumwambia: fanya biashara kwa ajili ya maisha yako na uwe mwaminifu katika muamala wako.

Hakika waliodhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao.

Makusudio ya waliodhulumu hapa ni mataghuti ambao walimkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Maana ni kuwa fungu la adhabu ya hawa ni sawa na la uma zilizotangulia, walipowakadhibisha mitume wao

Basi wasiniharakishe adhabu ambayo itawshukia tu. Na leo iko karibu sana na kesho.

Ole wao walioikanusha siku yao waliyoahidiwa wanayoiharakisha. Mara ngapi mwenye kuliharakisha jambo, likija anapendelea lisingekuwa!