read

Aya 57 – 74: Je, Mnaona Makulima Mnayoyapanda

Maana

Sisi tumewaumba; basi mbona hamsadiki?

Waliamini na wakakubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba, lakini wakakana na kukadhibisha kwamba wao baada ya mauti watarudishwa kwa ajili ya hisabu na malipo. La kwanza kwa itikadi, linawezekana ama la pili kwao ni muhali.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawarudi kuwa kuanza kuumba na kurudisha baada ya mauti ni hali moja tu, kulingana na uweza wa Mwenyezi Mungu; bali kurudisha ni rahisi zaidi. Kwani kuumba ni kuleta kitu kisichokuwepo kabisa, na kurudisha ni kukusanya viungo vilivyotawanyika.

Kwa hiyo basi inawalazimu moja ya mambo mawili: Ama muamini yote mawili au muyakate yote. Mwenye kuamini moja na akaacha jingine atakuwa amejipinga yeye mwenyewe. Hii inaitwa dalili ya kulazimiana baina ya vitu viwili, haiepukani na nyingine. Kwa hiyo moja inaitolea dalili nyingine kichanya na kihasi.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akapiga mifano ya kuumba kwake inayofahamisha uwezekano wa kuweko ufufuo; kama ifutavyo:-

1. Je, mnaiona mbegu ya uzazi mnayoitoneza? Je, mnaiumba nyinyi, au tunaimba Sisi?

Ni nani aliyewaumba kutokana na manii yenu kuwa mtu aliyekamilika viungo vyake na silika yake. Ni nyinyi au Mwenyezi Mungu? Mmeshusha manii katika mfuko wa uzazi wa mwanamke tu na kazi yenu ikaisha. Ni nani aliyeyageuza manii kuwa pande la damu nalo kuwa pande la nyama kisha kuwa mifupa na mifupa kuvikwa nyama n.k.? Ikiwa mtasema yote hiyo ni kazi ya asili ya maumbile peke yake, tutawauliza:

Ni nani aliyeyaleta hayo maumbile? Mkijubu kuwa yamejileta yenyewe, tutawauliza: Ni nani aliyempa mtu uhai, hisia na utambuzi? Mkisema ni hayo maumbile, tutawauliza: Hayo yana uziwi na upofu, na asiyekuwa nacho hawezi kutoa.

Mkiendelea kusema kuwa uhai umetokea kwenye maada bila ya makusudio, nasi tutawaambia kuwa maneno haya nayo yametokea bila ya makusudio. Na akili haikubali tafsiri yoyote ya maisha na nidhamu ya ulimwengu isipokuwa kwa sababu ya kiakili iliyofanya. Na haiwezekani kuweko sababu zizizokuwa na ukomo; vinginevyo kupatikana kusingekuwa na athari.

Sisi tumewawekea mauti.

Mwenye kumiliki mauti ndio huyo huyo anayemiliki uhai.

Na Sisi hatushindwi kuwaleta wengine badala yenu na kuwaumba nyinyi kwa umbo msilolijua.

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hashindwi, wala hapitwi na lolote; na yeye ni muweza wa kila jambo. Na kwa uweza wake amehamisha kukosekana kwenye kupatikana. Lau Mwenyezi Mungu angelitaka kuwabadilisha waasi kuwa watu wengine wanaomtii, angelifanya hilo wala hakuna wa kulizuia analolitaka.

Hapa kuna makemeo na kiaga kwa yule anayepinga mwito wa haki:

 وَإِنْ تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُمْ {38}

“Na mkigeuka atawaleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa kama nyinyi.”
Juz. 26 (47:38).

Na bila ya shaka mlikwishajua umbo la kwanza, tena mbona hamkumbuki?

Mmejua kuumbwa kwenu kusikotokana na kitu chochote; sasa je tutashindwa kuvikusanya viungo vyenu na kuvirudisha kama vilivyokuwa baada ya baada ya kutawanyika?

Tafsiri fasaha zaidi ya Aya hii ni kauli ya Imam Ali (a.s.): “Nashangazwa na yule anayepinga ufufuo wa mwisho na hali anaona ufufuo wa kwanza!”

2. Je, Mnaona mnayolima? Je, ni nyinyi mnayoyaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha?

Mtu anatafuta mbegu, analima anapanda na kumwagilia maji, hilo halina shaka. Lakini hiyo mbegu, miche, maji, ardhi na mengineyo, kama jua na hewa yametoka wapi? Wakisema; yametokana na kitendo cha maada isiyokuwa na akili, nasi tutawajibu: Kauli yenu hiyo inatokana na asiyekuwa na akili.
Tungelitaka tungeliyafanya mapepe, mkabaki mnastaajabu, Mkisema: Hakika sisi tumegharimika.

Yaani tumetaabika sana na kugharimika kutayarisha mashamba na wala hatukunufaika na chochote. Na mtaendelea kusema: Bali sisi tumenyimwa riziki. Hakuna kitu kinachotia uchungu kwenye nafsi kuliko kuhisi kunyimwa.

3. Je, mnayaona maji mnayoyanywa? Je, ni nyinyi mnayoyateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha?

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaashiria kuwa Yeye ndiye aliyeleta maumbile yanayosababisha mvua. Maana ni kuwa maji haya, ambayo ni asili ya uhai, na ambayo mtu hana budi nayo kwa hali yoyote, ni nani aliyesababisha kupatikana kwake na kuyapangilia? Ni nyinyi au ni yule ambaye ameumba kila kitu na akakipangilia?

Mwenyezi Mungu amezindua, kwenye Aya nyingi. kwamba Yeye atafufua wafu; kama anavyoifufua ardhi kwa mvua:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنْزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ ۚ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۚ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {39}

“Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi imetulia, lakini tunapoiteremshia maji mara unaiona inashtuka na kututumka. Bila ya shaka aliyeihuisha ardhi ndiye atakayehuisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza juu ya kila kitu.” Juz. 24 (41:39).

Tungelipenda tungeliyafanya ya chumvi kali. Basi mbona hamshukuru?

Neno chumvi kali tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu ujaj lenya maana ya chumvi kali iliyofikia kufanya kitu kiwe kichungu.

Maana ni kuwa lau Mwenyezi Mungu angelitaka angeliyafanya maji kuwa na chumvi sana yasiyoweza kuwa na manufaa ya kunywewa wala kulimi- wa, lakini ameyafanya tamu baridi, kwa ajili ya kuwahurumia. Pamoja na kuwa neema hii inataka kushukuriwa, lakini bado Mwenyezi Mungu anamlipa mwenye kushukuru.

4. Je, mnauona moto mnaouwasha?

Moto ni neema sawa na maji. Lau si huo mtu asingeliweza kupiga hata hatua moja katika maisha yake; mpaka siku yake ya mwisho angelibakia akiishi na wanyama mwituni.

Ni nyinyi mliouumba mti wake au Sisi ndio Wenye kuuumba?

Moto unasabishwa na vitu mbali mabali; miongoni mwavyo ni kuni, makaa ya mawe, mafuta umeme na mengineyo watakayoyagundua wataalamu baadae au wasiyagundue, Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi.

Umetajwa mti katika Aya kwa njia ya kufananisha tu. Wafasiri wamesema kuwa waarabu walikuwa wakipekecha vijiti kutoa moto, ndio maana Mwenyezi Mungu akaleta mfano unaoendana na maisha ya wakati huo.

Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa wenye kusikiliza.

Neno kusikiliza tumelifasiri kutokana na neno muqwin ambalo wafasiri wametofatiana katika tafsiri yake. Tabari anasema: “Wametofautiana wafasiri katika maana ya neno muqwin. Kuna waliosema ni wasafiri na waliosema ni wasikilizaji.”

Sisi tumchagua wenye kusikiliza kwa vile moto unawanufaisha wasafiri na wasiokuwa wasafiri.
Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wakikusudiwa watu wote. Maana ni mtukuze na umtakase Muumba Mkuu na kila yasiyofanana na ukuu wake. Waislamu wanaisoma tasbihi katika rukui zao. Ama kwenye sujudi zao wanasoma tasbihi iliyoko (87:1).

فَلَا أُقْسِمُ بِمَوَاقِعِ النُّجُومِ {75}

Basi naapa kwa maanguko ya nyota.

وَإِنَّهُ لَقَسَمٌ لَوْ تَعْلَمُونَ عَظِيمٌ {76}

Na hakika bila ya shaka hiki ni kiapo kikubwa, lau mngelijua!

إِنَّهُ لَقُرْآنٌ كَرِيمٌ {77}

Hakika hii bila ya shaka ni Qur’an Tukufu,

فِي كِتَابٍ مَكْنُونٍ {78}

Katika Kitabu kilichohifadhiwa.

لَا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ {79}

Hapana akigusaye ila waliotakaswa.

تَنْزِيلٌ مِنْ رَبِّ الْعَالَمِينَ {80}

Ni uteremsho unaotoka kwa Mola wa walimwengu wote.

أَفَبِهَٰذَا الْحَدِيثِ أَنْتُمْ مُدْهِنُونَ {81}

Je, ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayafanyia udanganyifu?

وَتَجْعَلُونَ رِزْقَكُمْ أَنَّكُمْ تُكَذِّبُونَ {82}

Na mnafanya riziki yenu kuwa mnakadhibisha?

فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ {83}

Basi mbona itakapofika kwenye koo.

وَأَنْتُمْ حِينَئِذٍ تَنْظُرُونَ {84}

Na nyinyi wakati huo mnatazama,

وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْكُمْ وَلَٰكِنْ لَا تُبْصِرُونَ {85}

Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi, lakini hamuoni,

فَلَوْلَا إِنْ كُنْتُمْ غَيْرَ مَدِينِينَ {86}

Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka,

تَرْجِعُونَهَا إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {87}

Kwa nini hamuirudishi, ikiwa nyinyi mnasema kweli?

فَأَمَّا إِنْ كَانَ مِنَ الْمُقَرَّبِينَ {88}

Basi akiwa miongoni mwa waliokaribishwa.

فَرَوْحٌ وَرَيْحَانٌ وَجَنَّتُ نَعِيمٍ {89}

Itakuwa ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema.

وَأَمَّا إِنْ كَانَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ {90}

Na akiwa katika watu wa kuume.

فَسَلَامٌ لَكَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ {91}

Basi ni Salama kwako uliye miongoni mwa watu wa kuume.

وَأَمَّا إِنْ كَانَ مِنَ الْمُكَذِّبِينَ الضَّالِّينَ {92}

Na ama akiwa katika waliokadhibisha wapotovu,

فَنُزُلٌ مِنْ حَمِيمٍ {93}

Basi karamu yake ni maji yanayochemka,

وَتَصْلِيَةُ جَحِيمٍ {94}

Na kutiwa Motoni.

إِنَّ هَٰذَا لَهُوَ حَقُّ الْيَقِينِ {95}

Hakika hii ndiyo haki yenye yakini.

فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ {96}

Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.