read

Aya 7 – 11: Toeni Katika Alivyowafanya Ni Waangalizi

Maana

Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na toeni katika alivyowafanyia nyinyi kuwa ni waangalizi wake. Basi walio amini miongoni mwenu, na wakatoa, wana malipo makubwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehimiza kutoa na akapendekeza kwa mifumo mbali mbali. Akakemea na kumtishia kwa adhabu kali mwenye kufanya ubahili na akazuia. Miongoni mwa mifumo ya kuhimiza kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni Aya hii tuliyo nayo ambayo imeweka sawa imani ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kutoa.

Usawa huu unaashiria kwamba mwenye kufanya ubakhili na akazuia basi amemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake kimatendo; hata kama atawamini kinadharia. Vile vile Aya inaashiria kwamba wanachotoa matajairi sio mali yao; isipokuwa wao ni mawakala tu.

Imepokewa riwaya kutoka kwa sahaba mtukufu Abu dharr, kwamba yeye siku moja alitoka na Mtume kuelekea upande wa Uhud. Mtume (s.a.w.) akamwambia: Unauona mlima huu ewe Abu dharr? Akasema: ndio ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mimi sipendi kuwa na dhahabu mfano wake, kisha nitoe katika njia ya Mwenyezi Mungu na nife nibakishe kareti mbili. Abu dhar akasema: sio mirundo miwili ya dhahabu ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Akasema: Hapana karati mbili.1

Tazama kifungu cha maneno ‘Matajiri ni mawakala sio wenyewe’ katika Juz. 4 (3:180).

Na mna nini hata hamumwamini Mwenyezi Mungu na hali Mtume anawaita mumwamini Mola wenu? Naye amekwishachukua ahadi yenu, ikiwa nyinyi ni Waumini.

Makusudio ya ahadi hapa ni amali kutokana na inavyofahamisha dalili mkataa. Dalili hizo ziko nyingi sana, tumetangulia kuzitaja pale tunapofasiri Aya za kilimwengu; miongoni mwazo ni zile tulizozitaja katika Juz. 15 (17:83) kifungu cha ‘Mwenyezi Mungu na ilimu ya chembe hai;’ kama ambavyo tumetaja dalili za utume wa Muhammad (s.a.w.), katika kufasiri Aya zinazoashiria hivyo; ikiwemo tuliyoyataja punde katika Aya ya 77 ya sura iliyopita kwenye juzuu hii tuliyo nayo, kifungu cha ‘Uislamu na wanafikra wakuu wa Ulaya.’

Maana yanayopatikana ya Aya tuliyo nayo ni: vipi nyinyi mnapinga mwito wa Mtume kwenye imani ya Mwenyezi Mungu au kwenye lile linalowapa maisha na hali zimekuwako dalili za kutosha za kuweko Mwenyezi Mungu na umoja wake na ukweli wa Mtume katika mwito wake na unabii wake?

Razi anasema: kutokana na dalili hizo zilivyohukumia wajibu wa kufanya amali, zimekuwa na msisitizo zaidi ya kiapo, ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akauita ahadi.

Yeye ndiye anayemteremshia mja wake Aya zinazobainisha wazi ili awatoe gizani muingie kwenye nuru.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemtuma Muhammad (s.a.w.) kwa hoja za kutosheleza na mawaidha ili awatoe kwenye utuiifu wa shetani kwenda kumtii Mwingi wa rehema – kutoka kwenye upotevu na ufisadi kwenda kwenye uongofu na utengeneo. Mtume akawahofisha na nguvu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake, kama wakipinga, na akawaahidi wema na thawabu nyingi kama wataitikia mwito na kumtiii; akawaambia:

Na hakika Mwenyezi Mungu kwenu ni Mpole, Mwenye kurehemu.

Mwenyezi Mungu ni mpole kwa waja, mwenye huruma, mwema na mkarimu.
Anawafanyia upole bila ya wao kujua na kuwaandalia njia ya heri bila ya kudhania na anawaneemesha, lakini wao wanafanya jeuri.

Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu?

Mali yote iliyo mikononi mwa mtu ni ya kuazima tu atawaachia wa baada yake. Inaendelea hivi mpaka mtu wa mwisho; akishaondoka atakuwa hana mrithi isipokuwa Mwenyezi Mungu: “Hakika sisi tutairithi ardhi na walio juu yake na kwetu sisi watarejeshwa,” Juz. 16 (19:40).

Ikiwa hali ni hiyo basi ubahili ni wa nini? Kwani kujizuia kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu? Katika Nahjul-balagha anasema: “Namshangaa bahili anayeulilia ufukara alioukimbia na unampita utajiri alioutaka. Duniani anaishi maisha ya kifukara na akhera atahisabiwa hisabu ya matajri.”

Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita.

Mkabala wake ni na waliotoa baada ya ushindi wa Makka.

Ufufanuzi wa maana ni kuwa kitu kinaweza kupimwa kwa vipimo na kwa aina; kama vyakula vinywaji, mavazi na vipambo. Thamani ya vitu hivi na mfano wake hukadiriwa kwa kipimo chake na kwa manufaa yake pamoja. Vingine vinapimwa kwa idadi tu; kama vile upigaji kura. Kura ya mjinga na mtaalamu, ya muovu na mwadilifu zote ni sawa katika kumfikisha mgombea kwenye uongozi au bungeni, au kutomfikisha.

Vingine vinapimwa kwa aina tu; kama vile dawa inayopimwa kwa athari ya kuponesha kwake au kinga yake.

Kutoa nako kuko namna kama hii. Mtu anaweza kutoa maelfu kwa ajili ya sehemu ya kuabudu, lakini asiwe na malipo ya yule aliyetoa mkate kumpa mwenye njaa.

Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akakana usawa wa aliyetoa na akapigana kabla ya ushindi wa Makka na aliyetoa baada ya ushindi wa Makka. Waislamu kabla ya ushindi wa Makka walikuwa na dhiki na haja sana na huku makafiri wakiwa kwenye utajiri na nguvu, lakini baada ya ushindi ilikuwa kinyume – ukafiri ulidhoofika na Uislamu ukawa na nguvu.

Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale waliotoa baadae na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi Mungu amewaahidi wema. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.

Hao ni ishara ya wale waliotangulia. Maana ni kuwa kila mmoja kati ya waliotangulia na waliofuatia ana ujira na thaawabu lakini kwa kutofautiana:

وَلِكُلٍّ دَرَجَاتٌ مِمَّا عَمِلُوا ۖ وَلِيُوَفِّيَهُمْ أَعْمَالَهُمْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {19}

“Na wote watakuwa na daraja zao mbalimbali kwa waliyoyatenda na ili awalipe kwa vitendo vyao.” Juz. 26 (46:19).

Kwa maneno mengine ni kuwa waliotangulia wenye kukaribishwa ndio aina hii ya kwanza ambao Mwenyezi Mungu amewataja katika Aya ya 10 ya sura iliyotangulia. Na watu wa kuume ni katika aina hii ya pili. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewataja katika Aya ya 67 ya sura hiyo.

Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amrudishie maradufu, na apate ujira mzuri.

Makusudio ya kukopesha hapa ni kutoa, kwa sababu Mwenyezi Mungu haihitajii mkopo anajitosheleza. Katika Nahjul-balagha kuna maelezo haya: “Mwenyezi Mungu hakuwataka msaada kwa sababu ya unyonge wala hawataki mkopo kwa sababu ya kuishiwa.
Anawataka msaada na hali ana majeshi ya mbingu na ardhi na Yeye ni Mwenye nguvu Mwenye hikima. na anawataka mkopo na hali ana hazina za mbingu na ardhi na Yeye ni mwenye kujitosha msifiwa. Ametaka kuwajaribu ni nani mwenye matendo mazuri zaidi kwenu.”

Umetangulia mfano wake na tafsiri yake kwa ufafanuzi katika Juz. 2 (2:245).

يَوْمَ تَرَى الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ يَسْعَىٰ نُورُهُمْ بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِمْ بُشْرَاكُمُ الْيَوْمَ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ {12}

Siku utakapowaona waumini wanaume na waumini wanawake, nuru yao inakwenda mbele yao, na kuume kwao: Furaha yenu leo ni Bustani zipitiwazo na mito chini yake kukaa humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

يَوْمَ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ لِلَّذِينَ آمَنُوا انْظُرُونَا نَقْتَبِسْ مِنْ نُورِكُمْ قِيلَ ارْجِعُوا وَرَاءَكُمْ فَالْتَمِسُوا نُورًا فَضُرِبَ بَيْنَهُمْ بِسُورٍ لَهُ بَابٌ بَاطِنُهُ فِيهِ الرَّحْمَةُ وَظَاهِرُهُ مِنْ قِبَلِهِ الْعَذَابُ {13}

Siku wanafiki wanaume na wanafiki wanawake watapowaambia walioamini: Tuangalieni ili tupate mwangaza katika nuru yenu. waambiwe: Rejeeni nyuma yenu mkaitafute nuru! Utiwe baina yao ukuta wenye mlango - ndani yake mna rehema, na upande wake wa nje kuna adhabu.

يُنَادُونَهُمْ أَلَمْ نَكُنْ مَعَكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ وَلَٰكِنَّكُمْ فَتَنْتُمْ أَنْفُسَكُمْ وَتَرَبَّصْتُمْ وَارْتَبْتُمْ وَغَرَّتْكُمُ الْأَمَانِيُّ حَتَّىٰ جَاءَ أَمْرُ اللَّهِ وَغَرَّكُمْ بِاللَّهِ الْغَرُورُ {14}

Watawaita wawaambie: Kwani hatukuwa pamoja nanyi? Watawaambia: Ndiyo, lakini mlijifitini wenyewe, na mkangojea, na mkatia shaka na matamanio yakawadanganya, Mpaka ilipokuja amri ya Mwenyezi Mungu ya na mdanganyifu akawadanganya katika Mwenyezi Mungu.

فَالْيَوْمَ لَا يُؤْخَذُ مِنْكُمْ فِدْيَةٌ وَلَا مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ مَأْوَاكُمُ النَّارُ ۖ هِيَ مَوْلَاكُمْ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ {15}

Basi leo haitapokelewa kwenu fidia, Wala kwa wale walio kufuru. Makaazi yenu ni Motoni; na ni marejeo maovu yalioje!
  • 1. Karati moja ni sawa na 0.2gm