read

Aya 75 – 96: Hapana Aigusaye Ila Waliotakaswa

Basi naapa kwa maanguko ya nyota, na hakika bila ya shaka hiki ni kiapo kikubwa, lau mngelijua!

Lugha

Wafasiri wengi wamesema kuwa herufi la hapa ni ziyada kiirabu ya nahau; kama ilivyo katika katika Aya ya mwisho ya Juzuu hii tuliyo nayo (57:29) na “Nini kilichokuzuia kumsujudia.” Juz. 8 (8:12). Wengine wamesema kuwa herufi La hapa ni ya asili, na kwamba maana yake ni ‘Siapi,’ kwa vile jambo liko wazi nilislohotajia kiapo.

Kauli sahii ni ya mwanzo, kwa dalili ya kuli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na hakika bila ya shaka hiki ni kiapo kikubwa, lau mngelijua!” inayofahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ameapa hasa.

Katika Juz. 23 (37:1), tumesema kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kuapia chochote katika viumbe wake, kwa sababu kila kiumbe kinafahamisha kuweko muumba, ujuzi wake na hikima yake; sikwambii tena ikiwa kinachoapiwa athari yake inaonyesha zaidi mpangilio wa ulimwengu na nidhamu yake na kuhifadhika kwake na kubakia; kama vile kuwekwa nyota sehemu zake na mpangilio wake; kiasi ambacho lau itasogea moja tu kutoka sehemu yake kwa nafasi ya unywele mmoja tu, basi kila kitu kitaharabika. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘lau mngelijua!,’ inaashiria kuwa watu wengi hawajui hakika hii; hasa wale wa zama za mwanzomwanzo.

Uislamu Na Wanafikra Wakuu Wa Ulaya

Hakika hii bila ya shaka ni Qur’an Tukufu.

Ndio! Hii ni Qur’an tukufu inayotosheleza miongozo na dalili zote, ni ponyo la ugonjwa wa ujinga na upotevu, inaongoza kwenye vituo vya heshima na salama na ni mkombozi wa vifungo vya dhulma na utumwa.

Siri ya sifa zote hizi na nyinginezo ni kuwa Qur’an inatekeleza mahitajio yote ya maisha, na inafungamanisha dini na matendo, katika maisha ya dunia, kwa ajili ya maisha mazuri ya usawa yasiyokuwa na matatizo wala uadui. Hata wema wa Akhera pia hawezi kuupata ila mwenye ikhlasi na akafanya matendo mema. Kabisa! Hakuna njia ya kwenda kwa Mwenyezi Mungu wala kuokoka isipokuwa kwa matendo yenye kunufaisha:

 فَأَمَّا الزَّبَدُ فَيَذْهَبُ جُفَاءً ۖ وَأَمَّا مَا يَنْفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ۚ  {17}

“Ama povu linakwenda bure; ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi.” Juz. 13 (13:17).

Ndio maana Waislamu wamekongamana kwa kauli moja kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuweka sharia wala hataweka sharia ila kwa heri ya mtu na masilahi yake, na kwamba haiwezekani kabisa kuweka sharia itakayokuwa na madhara kwa mtu yoyote vyovyote awavyo.

Ikiwa itadaiwa kuwa ni sharia ya Qur’an na haiendani na misingi hii, basi hiyo itakuwa imetokana na ujinga wa wajinga au wasingiziaji wanaobandika mambo. Aya zinazofahamisha hivyo zinahisabika kwa makumi; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:

Kauli yake Mwenyezi Mungu kupitia Nabii wake Shua’yb:

 إِنْ أُرِيدُ إِلَّا الْإِصْلَاحَ {88}

“Sitaki ila kutengeneza.” Juz. 12 (11:88).

 مَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُمْ مِنْ حَرَجٍ وَلَٰكِنْ يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ {6}

“Mwenyezi Mungu hapendi kuwatia katika taabu lakini anataka kuwatakasa na kutimiza neema yake juu. Juz.6 (5:6).

 إِنَّ اللَّهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَحِيمٌ {143}

“Hakika Mwenyezi Mungu, kwa watu, ni Mpole, Mwenye kurehemu.” Juz. 2 (2:143).

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚ لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّهِ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {30}

“Basi uelekze uso wako sawa sawa kwenye dini – ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo dini ya sawa sawa, lakini watu wengi hawajui.” Juz. 21 (30:30).

Huu ndio uhakika wa Uislamu na uhalisia wake, ulio katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na ujuzi wake. Hakuna kitu ndani yake isipokuwa kile anachokihitajia mtu kwa silika yake na maumbile safi aliyozaliwa nayo yanayomtofautisha na viumbe vingine vyote, lakini sio kujiingiza kwenye tamaa dhulma uchokozi n.k.

Hakika hii wameigundua wanafalsafa na wanafsihi wengi wa Ulaya. Wakautukuza Uislamu na wakamsifia Mtume (s.a.w.); si kwa lolote ila ni kwa msukumo wa heri, haki na uadilifu.

Lau tungelikuwa na nafasi tungelitaja kauli zao nyingi, lakini yasiyowezakana yote hayaachwi yote. Tutachagua kauli za baadhi yao; kama vile: Mjarumani Goeth, Mfaransa Amrtin, Mrusi Tolstoy na Mwingereza Bernad Show. Wote hawa kama unavyooona wanatofautiana katika uta- maduni, mwelekeo na jinsia zao.

Goethe alisoma Qur’an, akatambua yaliyomo ndani yake na akaitukuza. Alifanya hafla usiku wa Laylatul-qadr ambao Qur’an iliteremshwa. Alisoma Historia ya Mtume (s.a.w.), akatunga kasida ya Muhammad na akaandika tamthilia ya Muhammad (s.a.w.).

Miongoni mwa kauli zake ni: “Ikiwa Uislamu ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu na sio kwenye hawa na matamanio, basi tuishi kwenye Uislamu na tufeni kwenye Uislamu.”

Amrtin, Mshairi mkubwa wa Kifaransa, anasema: “Maisha ya Muhammad (s.a.w.) yote yanafahamisha kuwa hakudhamiria kudanganya au kuishi kwenye ubatilifu… Hakika yeye ni mwongozi wa watu kwenye akili na ni muasisi wa dini isiyokuwa na uzushi.”

Tolstoy, mwanafalsafa ya binadamu kutoka Urusi, anasema: “Katika mambo yasiyo na shaka ni kuwa Muhammad ameihudumia jamii kwa huduma tukufu. Inatosha kuwa ni fahari, kwamba yeye ameongoza mamia ya mamilioni kwenye nuru ya haki utulivu na amani na akaupa ubinadamu njia ya maisha. Hiyo ni kazi kuu ambayo haiwezi isipokuwa yule aliyepewa nguvu na ilhamu kutoka mbinguni.”

Mwanafisihi wa kimataifa kutoka Uingerza, Bernad Show anasema: “Ni lazima isemwe kuwa Muhammad ni mwokozi wa mtu… Mimi ninaamini kwamba lau hivi sasa angelitawala ulimwengu mtu mfano wake, angelifaulu kutatua matatizo kwa namna ambayo ingeuleta ulimwengu kwenye amani na raha…Hakika Muhammad ni mkamilifu zaidi ya watu waliopita na watakaokuja, wala haifikiriwi kupatikana mfano wake katika watakaokuja.”

Kauli ya Show kuwa Muhammad ni mkamilifu zaidi ya watu waliopita na watakaokuja, inamaanisha kuwa risala ya Muhammad (s.a.w.) haifikiwi na risala ya manabii waliotangulia; hata Isa na Ibrahim.

Na aliposema: “Wala haifikiriwi kupatikana mfano wake katika watakaokuja.” Maana yake ni kuwa hakuna yeyote baada ya Muhammad (s.a.w.) anayeweza kuleta jipya lenye faida au manufaa zaidi ya alilolileta Muhammad.

Vile vile anamaanisha kuwa mwito wa Muhammad hauhitajii dini wala sharia au nidhamu nyingine; bali hizo nyingine ndizo zinauhitajia.
Kila mmoja wetu anajua kuwa Bernad Show ni katika wanafikra wakubwa wa ulaya aliyetokea katika karne ya ishirini, karne ya maendeleo ya atom na anga; na kwamba ushahidi wake huu ni matokeo ya utafiti mrefu, fikra ya kina na upembuzi yakinifu.

Ushuhuda huu wa Bernad ni ibara au tafsiri nyingine ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ {107}

“Na hatukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote.” Juz. 17 (21:107).

Yaani walimwengu wote kila wakati na kila mahali. Vile vile tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَلَٰكِنْ رَسُولَ اللَّهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ {40}

“Bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa mitume.” Juz. 22 (33:40).

Vile vile ushahidi wa Show, ni dalili mkataa ya ukweli wa waislamu katika itikadi yao, kwamba Muhammad ni mkamilifu zaidi ya watu waliopita na watakaokuja, wala haifikiriwi kupatikana mfano wake katika watakaokuja; kama anavyosema.

Je, baada ya hayo yote wanasemaje vijana wanokana dini ya mababa na mababu zao, kuhusiana na kauli ya Bernad Show? Je, wao wana ujuzi zaidi, wana hamu zaidi ya ubinadamu kuliko yeye au wao wanazungumza kwa kutumia fikra za maadui wa Uislamu na ubinadamu bila ya kujitambua?

Katika Kitabu kilichohifadhiwa.

Wametofautiana katika kuhifadhiwa Kitabu. Kuna waliosema kimehifad- hiwa na mchanga na vumbi; kama ilivyoelezwa katika Tafsir Attabari. Wengine wakasema kimehifadhiwa katika Lawh mahfudh.

Tuonavyo sisi ni kuwa hakuna haja ya mzozo huu, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebaainisha maana ya hifadhi hii kwa kusema:

Hapana akigusaye ila waliotakaswa. Ni uteremsho unaotoka kwa Mola wa walimwengu wote.

Yaani Qur’an ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu sio kutoka kwa shetani, wala si uchawi au ngano za watu wa kale; kama wanavyodai walahidi.

Wameafikiana wana fikh wa madhehbu kuwa ni haramu kugusa maandishi ya Qur’an isipokuwa kwa aliyetwahara mwenye udhu. Wakatofautiana katika kuiandika na kuisoma kwa asiyekuwa twahara.

Hanafi wamesema haifai kuiandika, lakini inajuzu kuisoma kwa moyo. Shafii wakasema haijuzu kuiandika wala kuisoma isipokuwa kama ni kwa kukusudia dhikri; kama kusoma Bismillah kwenye chakula. Maliki nao wakasema haijuzu kuiandika, lakini inajuzu kusoma kwa moyo au kwa kuiangalia. Hambali wamesema haijuzu kuiandika, lakini inajuzu kuichukua kwa kuiziba na kizuizi.

Shia Imamiyah wamesema si haramu kwa mwenye janaba kusoma Qur’an na inajuzu kuandika, isipokuwa sura nne za Azaim, zenye sijda ya wajib, ambazo ni: Alaq. Annajm, Alif lamim Sajjda na Sajda (96, 53, 41 na 32).

Je, ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayafanyia udanganyifu?

Makusudio ya maneno hapa ni Qur’an. Kauli hii inaelekezwa kwa wanafiki ambao walifanya udanganyifu; wakadhihirisha kuikubali Qur’an na nyoyoni wanaikataa.

Na mnafanya riziki yenu kuwa mnakadhibisha?

Makusudio ya riziki hapa ni neema na kukadhibisha ni kuikataa. Maana ni kuwa Qur’an ni neema kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu enyi wadanganyifu, vipi mnaikabili kwa kuikana na kuikufuru.

Kundi katika wafasiri wamesema: mvua iliponyesha walikuwa wakisema: hii ni kazi ya maumbile, kwa hiyo ikawa huko ni kukufuru neema ya Mwenyezi Mungu, na ndio wakateremshiwa Aya hii.

Lakini kauli hii iko mbali na maana. Kwa sababu mazungumzo yanahusiana na Qur’an si mvua.

Basi mbona itakapofika kwenye koo, na nyinyi wakati huo mnatazama!

Itakapofika kwenye koo ni roho. Hilo limefahamika kutokana na mfumo wa maneno unavyokwenda. Nyinyi wanaambiwa waliokaribu na anayekata roho, awe ni katika jamaa zake au la.

Maana ni mtakuwaje nyinyi wanafiki mmoja wenu akifikiwa na mauti na roho ikafika kooni huku mnamwangalia mkitamani aendelee kuishi, je mtakuwa na uwezo na kumrudishia uhai na afya yake?

Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi, lakini hamuoni.

Naye ni huyo anayekata roho. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anayajua yanayompitia mwenye kukata roho, na jinsi nyinyi mnavyoshindwa kumwokoa na mnavyoona uchungu kumkosa, lakini nyinyi hamjui kuwa Mwenyezi Mungu yuko kila mahali kwa ilimu yake na uweza wake.

Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka, kwanini hamuirudishi, ikiwa nyinyi mnasema kweli?

Ikiwa nyinyi mko huru, kama mnavyodai, na hamtaulizwa lolote wala hakuna yoyote anayeweza kuwalazimisha kitu, basi kwanini hamyazuii mauti na mkazirudisha roho kwenye mili yenu? Kwa sababu mnavyomaanisha ni kuwa Mwenyezi Mungu hamiliki mauti, uhai, ufufuo wala hisabu.

Basi akiwa miongoni mwa waliokaribishwa, itakuwa ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema.

Mwanzoni mwa sura hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewagawanya watu siku ya kiyama kwenye aina tatu, waliotangulia wenye kukaribishwa, watu wa kuume na wa kushoto.

Katika Aya hii anataja kuwa mwenye kukata roho akiwa ni katika waliotangulia basi atakuwa mwenye amani na neema ya milele. Aliyowaandalia wenye kutangulia ameyataja katika Aya ya 12 na zinazofuatia katika sura hii tuliyo nayo.

Na akiwa katika watu wa kuume, basi ni Salama kwako uliye miongoni mwa watu wa kuume.

Akiwa mkata roho ni katika aina ya pili ambayo ni watu wa upande wa kuume, basi malaika watampa bishara ya salama na raha. Mwenyezi Mungu ameyataja aliyowaandalia hawa katika Aya 27 na zinazofutia katika sura hii tuliyo nayo.

Na ama akiwa katika waliokadhibisha wapotovu, basi karamu yake ni maji yanayochemka, na kutiwa Motoni.

Anayekata roho akiwa ni katika aina ya tatu ambao ni watu wa kushoto, basi makazi yake ni Jahannam ambayo ni makazi mabaya kabisa. Maandalizi ya hawa, Mwenyezi Mungu ameyataja katika Aya 41 na zinazofuatia katika sura hii tuliyo nayo.

Hakika hii ndiyo haki yenye yakini isiyokuwa na shaka yoyote. Katika baadhi ya vitabu vya kisufi imeelezwa kuwa utambuzi uko mafungu matatu: Utambuzi wa ilimu ya yakini; kama kujua kuweko moto kutokana na moshi unaofuka, kujua kwa jicho la yakini; kama kuuona moto wenyewe hasa na kujua kwa haki ya yakini; kama kuungua kwenye huo moto.

Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.

Imetangulia kwa herufi zake katika Aya ya 75 ya sura hii.