Aya 9 – 17: Nuh
Maana
Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliashiria kwamba Muhammad (s.a.w.) aliwaonya watu wake, lakini hayakufaa maonyo. Katika Aya tulizonazo anaashiria kuwa hali ya Muhammad (s.a.w.) na watu wake, katika hilo, ni kama hali ya Nuh, na watu wake:
Kabla yao kaumu ya Nuh walikadhibisha; wakamkadhibisha mja wetu.
Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu: “wakamkadhibisha ni tafsiri ya kauli yake: “Walikadhibisha.” Kama kwamba muulizaji aliuliza: hawa jamaa walimkadhibisha nani? Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akajibu kuwa wao walimkadhibisha mja wetu Nuh, na wakasema ni mwendawazimu; sawa na walivyosema makuraishi kumwambia Mtume mtufu (s.a.w.).
Shutuma hii ni ya kawaida kwa wale wanaoshindwa kujibu.
Na akakaripiwa.
Hapa Mwenyezi Mungu anaashiria yale aliyosema katika kauli yake:
قَالُوا لَئِنْ لَمْ تَنْتَهِ يَا نُوحُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمَرْجُومِينَ {116}
Walimkemea, wakamzuia kufikisha na wakamtisha kumpiga mawe na kumuua kama ataendelea.
Basi akamwomba Mola wake Mlezi: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!
Watu wa Nuh walipodhikika naye, naye akadhikika nao, alimkimbilia Mola wake na kusema kuwa nimemaliza mbinu zote na kazi yangu ya tabligh imefika ukomo, sasa iliyobaki ni amri yako kwa watu hawa makafiri waovu, basi waadhibu na uinusuru dini yako na mjumbe wako.
Kwa hakika Nuh hakuwaapiza watu wake ila baada ya kukata tamaa nao. Aliendelea kuwalingania kiasi cha miaka elfu kupungua hamsini bila ya mafanikio; kama ilivyoelezwa katika Juz.20 (29:14).
Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika. Na tukaipasua ardhi kwa chemchem.
Dua ya Nuh iliitikiwa na Mwenyezi Mungu, akawagharikisha kwa maji yanayotoka mbinguni na yanayotoka ardhini, yakakutana maji kwa jambo liliokadiriwa.
Yaani mvua na chemchem zikachanganyika ikawa ni bahari kubwa kila upande. Hakuna aliyesalimika isipokuwa aliyekuwa katika Jahazi (safina).
Tufani na maangamizi haya yalikuwa ni kwa amri iliyokadiriwa. Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Kwa jambo lililokadiriwa,’ iko katika maana ya kauli yake:
وَكَانَ أَمْرُ اللَّهِ قَدَرًا مَقْدُورًا {38}
Na tukamchukua kwenye ile ya mbao na misumari
Aliyechukuliwa ni Nuh. Maana ni kuwa safina ilikuwa kama majahazi mengineyo, ilitengenezwa kwa mbao na misumari, lakini inakwenda kwa macho yetu, kwa hifadhi na kuilinda. Kwa hiyo ikaokoka na hatari; vinginevyo isingeweza kuhimili mikikimikiki ya tufani.
Ni malipo kwa alivyokuwa amekanushwa.
Neno ‘malipo’ linaashiria sababu zilizowajibisha tufani na kuangamia makafiri.
Na hakika tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anayekumbuka?
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliiacha habari ya safina iwe ni somo na mawaidha kwa yule anayewaidhika kwa mazingatio.
Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo?
Ni kweli kabisa tufani iliangamiza. Ama Nuh, mwenye kutoa bishara na maonyo, alikuwa ni mkweli katika aliyoyafikisha na kuyatolea maonyo.
Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliiteremsha Qur’an kwa ajili ya ukumbusho na maonyo, na ameyafanya mepesi maana yake kufahamika ili wanufaike nayo, sio watajirike kwa matamshi yake, kuzifanyia dawa Aya zake, au kuzipotoa na kuziuza kwa thamani ndogo.
Basi je yupo anayekumbuka?
Je, watazingatia na kupata onyo, kwa yaliyokuja katika Qur’an, wale wanaoifanyia biashara dini na kuyabadilisha maneno sehemu zake kwa kufuata matamanio yao na malengo yao?
Kisa cha Nuh kimetangulia katika sura Hud, iliyo kwenye Juzuu ya 12, na nyinginezo.
كَذَّبَتْ عَادٌ فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ {18}
إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي يَوْمِ نَحْسٍ مُسْتَمِرٍّ {19}
تَنْزِعُ النَّاسَ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ مُنْقَعِرٍ {20}
فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ {21}
وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِنْ مُدَّكِرٍ {22}
كَذَّبَتْ ثَمُودُ بِالنُّذُرِ {23}
فَقَالُوا أَبَشَرًا مِنَّا وَاحِدًا نَتَّبِعُهُ إِنَّا إِذًا لَفِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ {24}
أَأُلْقِيَ الذِّكْرُ عَلَيْهِ مِنْ بَيْنِنَا بَلْ هُوَ كَذَّابٌ أَشِرٌ {25}
سَيَعْلَمُونَ غَدًا مَنِ الْكَذَّابُ الْأَشِرُ {26}
إِنَّا مُرْسِلُو النَّاقَةِ فِتْنَةً لَهُمْ فَارْتَقِبْهُمْ وَاصْطَبِرْ {27}
وَنَبِّئْهُمْ أَنَّ الْمَاءَ قِسْمَةٌ بَيْنَهُمْ ۖ كُلُّ شِرْبٍ مُحْتَضَرٌ {28}
فَنَادَوْا صَاحِبَهُمْ فَتَعَاطَىٰ فَعَقَرَ {29}
فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ {30}
إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ صَيْحَةً وَاحِدَةً فَكَانُوا كَهَشِيمِ الْمُحْتَظِرِ {31}
وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِنْ مُدَّكِرٍ {32}