Table of Contents

Aya 30 – 40: Suleiman

Maana

Na Daudi tukamtunukia Suleiman, mbora wa waja. Kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu.

Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu kumeandikwa kuhusu Suleiman: “Suleiman ni jina la Ibrania na maana yake ni mtu wa amani. Ni mtoto wa mfalme Daud aliyerithi kiti chake cha ufalme, ingawaje alikuwa na ndugu zake wengine sita wa mama mbalimbali. Suleiman ni mtoto wa Bath-sheba aliyekuwa mke wa Uria. Daud alimpenda sana Suleiman kwa vile alikuwa ni mtoto wa mkewe anayempenda zaidi. Na Daud alimwahidi Bath-sheba kuwa atakuwa mfalme baada yake.”

Wameeleza kwa muhtasari hao waliochangia kuweka Kamusi hiyo kutoka kwenye Biblia kitabu cha Wafalme 1 na Samweli 2. Maana yake ni kuwa Tawrat inamuelezea Daud kuwa hafuati amri ya Mwenyezi Mungu wala kutumia wahyi wake, isipokuwa anafuata wahyi wa mwanamke aliyempora kwa mumewe aliyemuua kwa upanga mkali.
Na kwamba yeye mwanamke ndiye muamrishaji na mkatazaji kwake yeye Suleiman na kwa wananchi wake. Ikiwa leo mwanamke anatafuta usawa na mwanamume, basi Tawrat inawafanya wafalme na watawala ni watiifu wa hawaa za wanawake na matamanio yao. Hayo si ajabu, kwani hadi leo jinsia hiyo ndio nyenzo bora ya mayahudi ya kupata faida na kufikia matakwa yao.

Alipopelekewa jioni farasi wasimamao kidete, wepesi wakimbiapo Basi akasema: Navipenda vitu vizuri kwa kumkumbuka Mola wangu. Kisha wakafichikana nyuma ya boma: Nirudishieni! Akaanza kuwapapasa miguu na shingo.

Wafasiri hapa wana kauli nyingi. Yenye nguvu zaidi ni ile isemayo kwamba siku moja wakati wa jioni alitaka aonyeshwe farasi wa maandalizi ya vita. Siku hizo ilikuwa ndio silaha ya kumtisha adui.

Kwa maneno mengine ni kuwa alitaka aone gwaride la askari, na akaamrisha kuletwa farasi mbele ya macho yake na akasema haya ninayafanya kwa amri ya Mola wangu sio kwa mapendeleo ya nafsi yangu. Mpaka walipopita akawafurahia. Walipopotea machoni mwake aliaamrisha warudishwe; akawa anawapapasa miguuni na shingoni akiwafurahia na kuwaridhia.

Kwa hiyo makusudio ya kupenda vitu vizuri ni kule kuonyeshwa farasi na kupita machoni kwake. Ama kusema kwake “Kwa kumkubuka Mola wangu,” maana yake ni kuwa ninayafanya haya kwa amri ya Mola wangu sio kwa amri yangu.

Na tulimtia kwenye mtihani Suleiman, na tukauweka mwili juu ya kiti chake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimpa mtihani Suleiman wa maradhi sugu na akamweka kitandani kama mwili bila roho; sawa na walivyojaribiwa manabii wengineo kwa aina ya majaribu.

Aya inaashiria kwamba mtihani huo ulikuwa ni malipo ya jambo fulani lililomtokea Suleiman, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakulibainisha jambo hilo. Waliyoyataja wafasiri kubainisha jambo hilo hayana msingi wowote. Vyovyote iwavyo ni kuwa Suleiman alitubia kutokana na yaliyotokea; kama walivyotubia manabii wengine na akamtakabalia toba yake kama alivyowatakabalia manabii wengine.

Kisha akarejea kwa kutubu, akasema: Mola wangu! Nighufuirie.

Ilivyo hasa ni kuwa manabii wanatubia kwa kuacha yaliyo bora si kwa kuwa wamefanya maasi. Hayo tumeyabainisha katika Juz. 1 (2:35-39) kifungu cha Isma.

Na unipe ufalme usiomwelekea yeyote baada yangu. Hakika Wewe ndiye mwingi wa kupa.

Alitaka ufalme wa aina yake kiaina si kiwingi; na kwa aina yake ya muujiza; kama vile kuutumikisha upepo, ndege na majini. Basi Mwenyezi Mungu akamwitikia dua yake kwa ushahidi wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Basi tukaufanya upepo umtumikie, ukienda kwa amri yake, popote alipotaka kufika.

na mashetani, wote wajenzi wakijenga anavyotaka Suleiman; kama vile mihirabu n.k. Na wapiga mbizi baharini wakitafuta lulu na johari Na wengine katika mashetani wafungwao kwa minyororo kwa vile walitoka kwenye amri yake na utii wake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 22 (34: 12-13).

Huku ndiko kutoa kwetu. Basi toa au zuia, bila ya hisabu. Naye kwa hakika anao ukuruba na marejeo mazuri kwetu.

Na kutoa kwa Mwenyezi Mungu hakupunguzi kinachotolewa. Ndio maana Mwenyezi Mungu alimwamrisha Suleiman kutoa kwa ujumla bila ya kipimo akitaka.

Katika Nahjul-Balagha kumeandikwa: “Mwenye uhakika wa kurudishiwa vizuri huwa mkarimu wa kutoa.” Pamoja na hayo lakini Suleiman ni kiumbe dhaifu, kama binadamu wengine: “Anaumizwa na chawa, hufa kwa kusongwa koo na jasho humfanya anuke.”

وَاذْكُرْ عَبْدَنَا أَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الشَّيْطَانُ بِنُصْبٍ وَعَذَابٍ {41}

Na mkumbuke mja wetu Ayyub. Alipomwita Mola wake akasema: Kwa hakika Shetani amenifikishia tabu na adhabu.

ارْكُضْ بِرِجْلِكَ ۖ هَٰذَا مُغْتَسَلٌ بَارِدٌ وَشَرَابٌ {42}

Piga-piga ardhi kwa mguu wako! Hapa mahali baridi pa kuogea na kinywaji.

وَوَهَبْنَا لَهُ أَهْلَهُ وَمِثْلَهُمْ مَعَهُمْ رَحْمَةً مِنَّا وَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ {43}

Na tukampa ahali zake na wengine kama wao pamoja nao, kuwa ni rehema itokayo kwetu, na iwe kumbusho kwa watu wenye akili.

وَخُذْ بِيَدِكَ ضِغْثًا فَاضْرِبْ بِهِ وَلَا تَحْنَثْ ۗ إِنَّا وَجَدْنَاهُ صَابِرًا ۚ نِعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ {44}

Na shika kitita cha vijiti mkononi mwako, kisha ndio upige kwacho, wala usivunje kiapo. Hakika tulimkuta mwenye subira, mbora wa waja, kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu.

وَاذْكُرْ عِبَادَنَا إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ أُولِي الْأَيْدِي وَالْأَبْصَارِ {45}

Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim na Is-haqa na Ya’qub waliokuwa na nguvu na busara.

إِنَّا أَخْلَصْنَاهُمْ بِخَالِصَةٍ ذِكْرَى الدَّارِ {46}

Sisi tumewahusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa makao;

وَإِنَّهُمْ عِنْدَنَا لَمِنَ الْمُصْطَفَيْنَ الْأَخْيَارِ {47}

Na hakika wao kwetu sisi ni wateuliwa walio bora.

وَاذْكُرْ إِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَذَا الْكِفْلِ ۖ وَكُلٌّ مِنَ الْأَخْيَارِ {48}

Na mkumbuke Ismail na Alyasaa na Dhulkifl, na wote hao ni katika walio bora.