Table of Contents

Aya 69 – 82: Walipotea Kabla Yao Watu Wengi Wa Zamani

Maana

Hakika waliwakuta baba zao wamepotea. Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao.

Wanazungumziwa washirikina wa kiarabu waliofuata nyayo za mababu zao bila ya kufanya utafiti wowote au mazingatio. Aya inaashiria kwamba mpotevu na mpotezaji wako sawa katika maasi na kustahili adhabu. Ama yule anayefuata uongofu na utengenevu anakuwa katika amani na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Hilo linafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Husema: Bali tuta- fuata yale tuliyowakuta nayo baba zetu. Je, hata kama baba zao walikuwa hawafahamu chochote wala hawakuongoka?” Juz. 2 (2:170). Maana yake ni kuwa, lau baba zao wangelikuwa kwenye uongofu, ingelifaa kuwafuata. Kwa maelezo zaidi tazama Juz.2 (2:168 – 170) kifungu cha ‘Kufuata na misingi ya itikadi.’

Na hakika walikwishapotea kabla yao wengi wa watu wa zamani. Na hakika tuliwapelekea waonyaji.

Ikiwa watakukadhibisha ewe Muhammad na kupotea na haki, basi walikwishapotea kabla yao wengi katika umma, ingawaje Mwenyezi Mungu aliwapeleka mitume na wabashiri; wakawatimizia hoja na kuwabainishia mapenzi yake na machukivu yake, wakaacha hayo wakafuata yale. Basi likastahili kwao neno la adhabu. Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale walioonywa walivyohizika na kubomolewa; isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliosafishwa, amewaokoa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na adhabu yake na akawalipa ujira wake na thawabu zake.

Na hakika Nuh alituita, na Sisi ni bora wa waitikiaji.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaashiria yale yaliyoelezwa kwenye Aya nyingine: “Na akasema Nuh: Mola wangu! Usiache Katika ardhi mkazi yeyote katika makafiri” (71:26).

Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa.

Mwenyezi Mungu alimnusuru Nuh na watu wake kutokana na mataghuti. Akawangamiza wote bila ya kubakia, kwa kuitikia maombi ya Nabii wake Nuh. Kwa hiyo akamuokoa yeye na walikouwa pamoja naye na udhia wa ukafiri muovu na kumuhifadhi na msiba na majanga.

Sam, Yafith Na Ham

Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia, peke yao baada ya tufani.

Katika Tafsir Tabariy imesemwa: “Dhuria wa Nuh ndio waliobakia katika ardhi baada ya kuangamia kaumu yake. Na watu wote baada yake, mpaka leo, ni wa kizazi cha Nuh.
Waajemi na waarabu wanatokana na watoto wa Sam bin Nuh,Waturuki na Waslovenia ni watoto wa Yafith na weusi ni watoto wa Ham. Ulama na mapokezi yameeleza hivyo.”

Tabari alifariki mwaka 310 (A.H.), yaani zaidi ya miaka elfu moja iliyopita. Waliomtangulia na waliokuja baada yake walimbandika jina la sheikh wa wafasiri.

Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu imeandikwa: “Sam ni jina la kiebrania likiwa na maana ya isimu (jina). Yeye ndiye mtoto mkubwa wa Nuh. Kizazi chake ni waarabu, Waarmenia, waashwar na wayahudi. Ndio maana lugha zao wote hao zinatiwa Saamiya, kwa kunasibishwa naye; mfano: lugha ya kiarabu na kiebrania…Yafith huenda maana yake ni uzuri… kizazi chake ni wakazi wa kuanzia magharibi mwa Najad, kusini mwa Bahari ya Kazwin (Caspian sea) na Bahari nyeusi (Black sea) hadi fukwe na visiwa vya Bahri ya kati (Mediterranean Sea) katika asili ya wahindi wa Ulaya–katika hawa wanaingia waturuki na waslovania aliowaashiria Tabariy-Na ham ni jina la kiebrania yaani mwenye kuchemka naye ni mdogo wa watoto wa Nuh”

Na tukamwachia kwa walio baadaye.

Yaani tukamwachia utajo wa sifa katika uhai wake

Amani kwa Nuh ulimwenguni kote!

Yeye yuko kwenye amani ya Mungu kwa kutotajwa na mabaya. Mitume walikuwa wakimwomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwa na utajo mzuri kwa watu wakiondoka. Ibrahim (a.s.) alisema:

وَاجْعَلْ لِي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الْآخِرِينَ {84}

“Na unijaalie kutajwa kwa wema na wengine” Juz. 19 (26:84).

Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

Yaani atawafanyia wema Mwenyezi Mungu kwa vile hapotezi amali ya yeyote mwenye kutenda, awe mume au mke.

Hakika yeye ni katika waja wetu walio waumini.

Kwa sababu alifanya wema katika matendo yake, akapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa jihadi yake ya haki. Hii ndio nembo na dalili ya mumin.

Kisha tukawagharikisha wale wengine duniani na akhera watakuwa na adhabu chungu kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.

وَإِنَّ مِنْ شِيعَتِهِ لَإِبْرَاهِيمَ {83}

Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake.

إِذْ جَاءَ رَبَّهُ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ {84}

Alipomjia Mola wake kwa moyo ulio salama.

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَاذَا تَعْبُدُونَ {85}

Alipomwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?

أَئِفْكًا آلِهَةً دُونَ اللَّهِ تُرِيدُونَ {86}

Je, kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu?

فَمَا ظَنُّكُمْ بِرَبِّ الْعَالَمِينَ {87}

Mnamdhania nini Mola wa walimwengu wote?

فَنَظَرَ نَظْرَةً فِي النُّجُومِ {88}

Kisha akapiga jicho kutazama nyota.

فَقَالَ إِنِّي سَقِيمٌ {89}

Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa!

فَتَوَلَّوْا عَنْهُ مُدْبِرِينَ {90}

Nao wakamuacha, wakampa kisogo.

فَرَاغَ إِلَىٰ آلِهَتِهِمْ فَقَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ {91}

Basi akaiendea miungu yao kwa siri.

مَا لَكُمْ لَا تَنْطِقُونَ {92}

Akaiambia: Mbona hamli? Mna nini hata hamsemi?

فَرَاغَ عَلَيْهِمْ ضَرْبًا بِالْيَمِينِ {93}

Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kuume.

فَأَقْبَلُوا إِلَيْهِ يَزِفُّونَ {94}

Basi wakamjia upesi upesi.

قَالَ أَتَعْبُدُونَ مَا تَنْحِتُونَ {95}

Akasema: Je, mnaviabudu vitu mnavyovichonga?

وَاللَّهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ {96}

Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba nyinyi na mnavyovifanya!

قَالُوا ابْنُوا لَهُ بُنْيَانًا فَأَلْقُوهُ فِي الْجَحِيمِ {97}

Wakasema: Mjengeeni jengo, kisha mtupeni motoni.

فَأَرَادُوا بِهِ كَيْدًا فَجَعَلْنَاهُمُ الْأَسْفَلِينَ {98}

Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini.

وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَىٰ رَبِّي سَيَهْدِينِ {99}

Na akasema: Hakika mimi nakwenda kwa Mola wangu atakayeniongoza.