Table of Contents

Aya 11 – 26: Bali Unastaajabu, Na Wao Wanafanya Maskhara

Maana

Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tuliowaumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unaonata.

Waulize ewe Muhammad, wale wanaokana ufufuo kuwa kuumba mbingu na ardhi bila ya nyenzo yoyote ni kugumu au kumrudisha mtu kwenye uhai baada ya kufa kwake, na hali Mwenyezi Mungu amemuumba kwa udongo tu uanonata?

Hakika yule ambaye ameuumba ulimwengu bila ya nyenzo yoyote, inakuwa wepesi zaidi kurudisha viungo vya mtu kwenye uhai.

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {57}

“Hakika kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu, lakini watu wengi hawajui.” (40:57)

Unaweza kuuliza: Kwenye Juz.15 (18: 22) Mwenyezi Mungu anasema: “Wala usiulize habari zao kwa yeyote yule.” Kuna njia gani ya kuafikiana Aya mbili hizi?

Jibu: maudhui ya Aya ile yanahusiana na watu wa pango; ambapo Mwenyezi Mungu alimkataza Nabii wake mtukufu kutomuuliza yeyote kuhusiana na wao, baada ya kumweleza habari zao. Na hii tuliyo nayo inahusiana na washirikina tu. Na makusudio ni kuwatahayariza na kuwapa hoja.

Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara.

Wewe Muhammad unawastaajabu washirikina kwa jinsi walivyomfanya Mwenyezi Mungu kuwa na washirika, pamoja na dalili za umoja zilizo wazwazi. Nao vile vile wanakushangaa wewe; bali wanakufanyia maskhara. Kwa sababu dalili za ushirikina ziko wazi kulingana na ufahamu wao na wala sio dalili za tawhid.

Hii inafahamisha kuwa ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili kweli ni jambo la ajabu. (38:5).

Ikiwa mtu atasema pamoja na yule mshairi: “Kila mtu dini yake anaitukuza, laitani usahihi ningejuzwa,” nasi tutajibu:

Kuna misingi na uhakika ulio wazi ambao hawawezi kutofautiana hata watu wawili; ambapo anaweza kuijua mjuzi na asiyekuwa mjuzi; mfano: Elimu ni bora kuliko ujinga, na utajiri ni bora kuliko ufukara.

Ikiwa wawili watatofautiana katika nadharia fulani, yule ambaye kauli yake itaishia kwenye misingi iliyo wazi basi huyo ndiye atakayekuwa na haki.

Na wanapokumbushwa hawakumbuki. Na wanapoona Ishara, wanafanya maskhara.

Kwa sababu mwenye kutii hawaa yake na kuiga mababa zake, huifumbia macho haki: Imam Ali (a.s.) anasema: “Yeyote anayeiacha haki, mazuri huwa mabaya kwake na mabaya huwa mazuri kwake, na hulewa ulevi wa upotevu.”

Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhahiri.

Haya wameyakari mara nyingi. Miongoni mwayo ni yale yaliyo katika Juz. 7 (6:7).

Ati tukishakufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa? Hata baba zetu wa zamani?
Maana yako wazi. umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz. 13 (13:5), Juz. 15 (17: 98), Juz. 18 (23: 82) na Juz. 20 (27:68)

Sema: Naam! Na hali nyinyi ni madhalili. Na hakika ni ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona!

Yaani sema ewe Muhammad, kuwaambia wale wanaopinga ufufuo: ndio, nyinyi mtafufuliwa kutoka kwenye makaburi yenu kwa neno moja tu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mtakusanywa kwake mkiwa madhalili na mtaiona adhabu mliyokuwa mkiikadhibisha kwa macho yenu.

Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo. Hii ndiyo Siku ya upambanuzi -baina ya haki na batili - mliyokuwa mkiikadhibisha.

Haki inapowajia wanapokuwa na fursa ya kuifanyia kazi, wanasema huu ni uwongo na uchawi, hauamini ila mjinga mwenye kuhadaliwa. Na wakati ukipita ukaja wakati wa malipo na kuonja ubaya wa matendo yao, watasema: Ole wetu, sisi tulikuwa kwenye mghafala wa haya, tumejidhulumu wenyewe.

Hali hii mara nyingi inatokea. Mjinga anahangaikia litakalomdhuru, lakini anapopewa nasaha na mwenye akili na kumhadharisha na mwisho mbaya, yeye humdharau na anafura kichwa.

Yakimfika na kutokuwa na pa kukimbilia na kutambua kuwa amehasirika anahangaika na majuto na kusema: laitani nisingelikuwako.

Wakusanyeni waliodhulumu, na wenzao, na hao waliokuwa wakiwaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu.

Aya inaashiria kugawanyika wakosefu; kwamba mshirikina atafufuliwa na washirikina wenzake mahali pamoja kwenye Jahannam wakiwa pamoja na masanamu waliyokuwa wakiyaabudu. Vile vile mwizi pamoja na wezi. Kila aina kwa aina yake; sawa na walivyokuwa duniani.

Waongozeni njia ya Jahannamu!

Ikishamalizika hisabu Malaika wataambiwa: Haya wapelekeni haraka kwenye moto mbaya.

Na wasimamisheni. Hakika hao wataulizwa:

Kabla ya Malaika kuwapeleka kwenye Jahannam watawazuia ili waulizwe yale waliyokuwa wakiyafanya. Katika badhi ya mapokezi imeelezwa kuwa siku hiyo mtu ataulizwa kuhusu alivyomaliza umri wake, mali yake alivyoipata na kuitumia na elimu yake alivyoifanyia kazi.

Ama kulinganisha baina ya Aya hii na ile isemayo:

فَيَوْمَئِذٍ لَا يُسْأَلُ عَنْ ذَنْبِهِ إِنْسٌ وَلَا جَانٌّ {39}

“Siku hiyo hataulizwa dhambi zake mtu wala jini.” (55:39)

Tumekuelezea mara nyingi. Kwa ufupi ni kuwa siku ya mwisho itakuwa na hali ya kuulizwa na ya kutoulizwa. Tazama juzuu hii tuliyo nayo (36:65).

Mna nini? Mbona hamsaidiani?

Yaani kesho wataambiwa wakosefu; kwa nini leo hamsaidiani na kule duniani mlikuwa na mshikamano dhidi ya haki na watu wake. Lengo la swali hili ni kutahayariza.

Bali leo, watasalimu amri.

Watafuata amri ya Mwenyezi Mungu na hawatakuwa na hila yoyote.

وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ {27}

Watakabiliana wao kwa wao kuulizana.

قَالُوا إِنَّكُمْ كُنْتُمْ تَأْتُونَنَا عَنِ الْيَمِينِ {28}

Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kuume.

قَالُوا بَلْ لَمْ تَكُونُوا مُؤْمِنِينَ {29}

Watasema: Bali nyinyi wenyewe hamkuwa waumini.

وَمَا كَانَ لَنَا عَلَيْكُمْ مِنْ سُلْطَانٍ ۖ بَلْ كُنْتُمْ قَوْمًا طَاغِينَ {30}

Na hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi mlikuwa waasi.

فَحَقَّ عَلَيْنَا قَوْلُ رَبِّنَا ۖ إِنَّا لَذَائِقُونَ {31}

Basi kauli ya Mola wetu imekwishatuthibitika. Hakika bila ya shaka tutaonja.

فَأَغْوَيْنَاكُمْ إِنَّا كُنَّا غَاوِينَ {32}

Tuliwapoteza kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu.

فَإِنَّهُمْ يَوْمَئِذٍ فِي الْعَذَابِ مُشْتَرِكُونَ {33}

Basi hakika wao siku hiyo watashirikiana katika adhabu.

إِنَّا كَذَٰلِكَ نَفْعَلُ بِالْمُجْرِمِينَ {34}

Hivyo ndivyo tutakavyowafanyia wakosefu.

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَٰهَ إِلَّا اللَّهُ يَسْتَكْبِرُونَ {35}

Wao walipokuwa wakiambiwa: Hapana Mola ila Mwenyezi Mungu (La ilaha illa Llahu) tu, wakijivuna.

وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَجْنُونٍ {36}

Na wakisema: Hivi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mshairi mwendawazimu?

بَلْ جَاءَ بِالْحَقِّ وَصَدَّقَ الْمُرْسَلِينَ {37}

Bali ameleta haki, na amewasadikisha Mitume.