Table of Contents

Aya 49 – 64: Wenye Takua Na Waliopetuka Mipaka

Maana

Huu ni ukumbusho.

Yaani huko kutaja Mwenyezi Mungu (s.w.t.), katika Aya zilizotangulia, sifa za manabii, kama Ibrahi, Ismail, Daud, Suleiman na wengineo.

Na hakika wenye takua wana marudio mazuri.

Mwenye takua ana mwanzo mzuri duniani na thawabu za Mwenyezi Mungu na radhi zake akhera, nazo ni Bustani za milele zitazofunguliwa milango kwa ajili yao, wataingia kwa amani bila ya kuulizwa au kuzuiwa.

Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda mengi na vinywaji. Na pamoja nao wapo wenye kutuliza macho, walio mari- ka.

Starehe za vyakula na vinywaji na zaidi ya hayo kuna mahurulaini, hawamnyooshei jicho mtu yoyote isipokuwa waume zao. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo (37:41).

Haya ndiyo mliyoahidiwa kwa Siku ya Hisabu.

Alioyaahidi Mwenyezi Mungu hayawezi kuachwa.

Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyomalizika.

Ndio hivi! Na hakika wenye kupituka mipaka bila ya shaka watapata marejeo maovu kabisa; kinyume kabisa na wenye takua. Wale wana makazi ya amani na hawa wana makazi maovu.
Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nayo ni malalo movu mno.

Watakua ni kuni zake nayo itakuwa ni shuka zao.

Ndio hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha!

Katika tafsiri Ar-Razi imeelezwa kuwa hapa kuna maneno yaliyotangulizwa na mengine kuja nyuma. Asili yake ni: Haya ni maji ya moto na usaha basi nawauonje.

Na mengineyo ya namna hii.

Adhabu ya watu wa motoni haimalizikii na maji ya moto na usaha tu; bali kuna aina nyinginezo za adhabu zinazofanana kwa ukali na ugumu na zinatofautiana kwa aina; kama vile Zaqqum na nyinginezo ambazo hakuna jicho lililoziona wala sikio lililozisikia.

Hili ndilo kundi litakaloingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho kwao. Hakika hao wanaingia Motoni.

Wakosefu wataingia motoni makundi makundi. Likiingia kundi moja likikutana na waliotangulia watawaambia hakuna makaribisho kwenu! Mmekuja kwetu basi mmepata makazi mabaya.

Waseme: Lakini nyinyi! Hamna makaribisho! Nyinyi ndio mliotutan- gulizia haya, napo ni pahala paovu kabisa! Waseme: Mola wetu! Aliyetutangulizia haya mzidishie adhabu mara mbili Motoni.

Maneno haya yote ni ya wale waliofika wakiwajibu waliotangulia. Wamewapokea kwa shari nao wakawarudishia zaidi. Kusema kwao: ‘nyinyi ndio mliotutangulizia haya,’ ni ishara ya kuwa viongozi wa upotevu ndio watakaotangulia motoni kisha wafuatiliwe na wafuasi wao. Kusema kwao ‘haya’ ni hayo ya adhabu. Kisha wafuasi watamtaka Mwenyezi Mungu awaongezee adhabu wale waliowahadaa.

Haya yamekaririka kimaana kwenye Aya kadha, zikiwemo. Juz. 2 (2:166), Juz. 8 (7:37) na Juz. 22 (34:31).

Watasema: Mbona hatuwaoni wale watu ambao tukiwahisabu ni katika waovu?

Watakaosema ni wale waliopituka mipaka. Makusudioya watu waliohisabiwa kuwa ni katika waovu ni wale wanyonge. Wenye mabavu katika maisha ya dunia walikuwa wakipora mali za wanyonge kisha wakiwaona kama wanyama na vyombo vya kutumia.

Walalahoi ni wanyama na washari. Kwa nini? Kwa vile wao wanakula kutokana jasho lao; wala hawakeshi kwenye makasino, mabaa na madanguro. Ama wale mataghuti, wanaopituka mipaka, basi wao ndio walio bora kwa vile wanastarehe na kufuja mali za wanyonge. Wanyonge ni wapumbavu kwa vile hawaendi mwendo wa kujificha, lakini wapenda anasa hao ndio mabwana kwa vile wanajigeuza kila rangi.

Siku ya hukumu vifuniko vyote vitafunuka na wahaini wataona makazi yao katika moto wa Jahannam, wala hawatumuona yeyote katika wale waliokuwa wakiwaita ni waovu. Watashangaa na kuulizana wako wapi? Hawatachukua muda ila watajua kuwa wako mbele za mfalme muweza. Basi roho zitawatoka kwa majuto na hilo litawazidishia maumivu.

Je, tuliwafanyia maskhara, au macho yamewakosa?

Haya ni maneno ya waliopetuka mipaka watajifanyia masikhara wenyewe Siku ya Kiyama, kwa sababu walikuwa wakiwafanyia masikhara wale walioamini.

Hakika hayo ya kuhasimiana watu wa Motoni ni kweli.

Kuhasimiana kwenyewe ni huko kukaribishana motoni. Na hilo bila shaka litakua tu.

قُلْ إِنَّمَا أَنَا مُنْذِرٌ ۖ وَمَا مِنْ إِلَٰهٍ إِلَّا اللَّهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ {65}

Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana Mola ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenza nguvu.

رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا الْعَزِيزُ الْغَفَّارُ {66}

Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake, Mwenye nguvu, Mwingi wa maghufira.

قُلْ هُوَ نَبَأٌ عَظِيمٌ {67}

Sema: Hii ni habari kubwa kabisa.

أَنْتُمْ عَنْهُ مُعْرِضُونَ {68}

Nyinyi mnaipuuza.

مَا كَانَ لِيَ مِنْ عِلْمٍ بِالْمَلَإِ الْأَعْلَىٰ إِذْ يَخْتَصِمُونَ {69}

Sikuwa na ilimu ya wakuu watukufu walipokuwa wakishindana.

إِنْ يُوحَىٰ إِلَيَّ إِلَّا أَنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُبِينٌ {70}

Sikupewa wahyi isipokuwa kwamba mimi ni mwonyaji tu aliye dhahiri.

إِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي خَالِقٌ بَشَرًا مِنْ طِينٍ {71}

Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo.

فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِنْ رُوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ {72}

Na nitakapomkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi muangukieni kwa kusujudu.

فَسَجَدَ الْمَلَائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ {73}

Wakasujudu Malaika wote pamoja.

إِلَّا إِبْلِيسَ اسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ {74}

Isipokuwa Ibilisi alijivuna na akawa katika makafiri.

قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَنْ تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ ۖ أَسْتَكْبَرْتَ أَمْ كُنْتَ مِنَ الْعَالِينَ {75}

Akasema: Ewe Iblisi! Kipi kilichokuzuia kumsujudia yule niliyemuumba kwa mikono yangu? Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu?

قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِنْهُ ۖ خَلَقْتَنِي مِنْ نَارٍ وَخَلَقْتَهُ مِنْ طِينٍ {76}

Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo.

قَالَ فَاخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌ {77}

Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni mwenye kufukuzwa.

وَإِنَّ عَلَيْكَ لَعْنَتِي إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ {78}

Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka Siku ya Malipo.

قَالَ رَبِّ فَأَنْظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ {79}

Akasema: Mola wangu! Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.

قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنْظَرِينَ {80}

Akasema: Basi hakika wewe ni katika waliopewa muda,

إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ {81}

mpaka siku ya wakati maalumu.

قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ {82}

Akasema: Naapa kwa utukufu wako, bila ya shaka nitawapoteza wote.

إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ {83}

Isipokuwa wale waja wako miongoni mwao waliosafishwa.

قَالَ فَالْحَقُّ وَالْحَقَّ أَقُولُ {84}

Akasema: Ni haki! Na ndio haki niisemayo.

لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنْكَ وَمِمَّنْ تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ {85}

Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wewe na kwa hao wote wenye kukufuata miongoni mwao.

قُلْ مَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُتَكَلِّفِينَ {86}

Sema: Siwaombi ujira juu ya haya, wala mimi si katika wanaojifanya.

إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِلْعَالَمِينَ {87}

Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote.

وَلَتَعْلَمُنَّ نَبَأَهُ بَعْدَ حِينٍ {88}

Na bila ya shaka mtajua habari zake baada ya muda.