Table of Contents

Aya 77 – 83: Akasema Ni Nani Atakayeihuisha Mifupa?

Maana

Je, haoni mtu kuwa tumemuumba kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndiye mgomvi wa dhahiri!

Jana alikuwa ni tone la manii, lakini alipokuwa, kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, ni kiumbe aliye sawasawa mwenye ufahamu, alisahau asili yake na kuanza kumchokoza Mola wake kwa uasi na maneno mabaya.

Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: ‘Ni nani huyo atakayeihuisha mifupa nayo imemung’unyika?’

Anayepiga mfano ni yule anayekana ufufuo. Anapiga mfano wa kutowezekana ufufuo kwa kusema, vipi vitaweza kuungana viungo vya mifupa na kuwa na uhai tena baada ya kuchakafuka na kuwa mchanga unaotawanyika huku na huko? Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamrudi mwenye mfano huu kwa kusema kuwa unastaajabu nini na kukana ufufuo kwa kupiga mfano na unasahahu nafsi yako? Hujui kwamba Mwenyezi Mungu amekuumba kwa mchanga kisha kwa tone la manii? Mwenyezi Mungu amekuleta baada ya kuwa hauko; vile vile basi ana uwezo wa kukurudisha baada ya kuwa mifupa iliyomung’unyika.

Sema: Ataihuisha aliyeiumba mara ya kwanza. Na Yeye ni Mjuzi wa kila uumbaji.

Yaani sema ewe Muhammad kumwambia mpinzani: Kuna ajabu gani kwa mifupa iliyochakaa kupata uhai? Yule ambaye amelifanya tone la manii liweze kusikia, kuona, kuwa na fahamu na ubainifu, ndiye atakayeweza kuirudisha mifupa ilivyokuwa. Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz. 15 (17:49).

Yeye ambaye aliwajaalia moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa mnauwasha.

Mfano huu unaweka wazi fikra ya ufufuo. Ubainifu wa hilo ni kwamba wenye kupinga wameweka mbali fikra ya ufufuo si kwa lolote isipokuwa kwa kudhani kuwa vitu haviwezi kugeuka kuwa kinyume chake.

Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawajibu kuwa fikra hii ni dhana na njozi tu. Kwa sababu mageuko haya yanatokea waziwazi mkiyaona asubuhi na jioni, lakini hamatanabahi.

Mti mbichi unageuka kuwa kuni na ardhi kame inapata uhai na kumea miti mbalimbali ikipata maji. Sasa vipi mnakana kupata uhai mifupa na mnakubali kupata uhai ardhi iliyokufa na miti kugeuka kuwa moto. Yote haya ni mamaoja tu – kugeuka kitu kutoka kilivyo na kuwa kinyume chake.

Kwani aliyeziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwa nini! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.

Mwenye kuuleta ulimwengu bila ya kutokana na chochote ni rahisi kuleta mfano wake kufanya mfano wake saa yoyote anayotaka. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:99).

Hakika amri yake anapotaka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kinakuwa.

Alianza kuumba kwa neno ’Kuwa’ na atarudisha kwa neno hilo hilo.

Basi Ametakata na mawi yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake mtarejeshwa.

Ametakasika Mola wetu na shirk na Yeye peke yake ndiye mwanzishi na mrudishaji.