read

Sura Ya Sabini Na Mbili: Al-Jinn

Imeshuka Makka Ina Aya 28.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

قُلْ أُوحِيَ إِلَيَّ أَنَّهُ اسْتَمَعَ نَفَرٌ مِنَ الْجِنِّ فَقَالُوا إِنَّا سَمِعْنَا قُرْآنًا عَجَبًا {1}

Sema: Nimepewa wahyi ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur’an ya ajabu!

يَهْدِي إِلَى الرُّشْدِ فَآمَنَّا بِهِ ۖ وَلَنْ نُشْرِكَ بِرَبِّنَا أَحَدًا {2}

Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu.

وَأَنَّهُ تَعَالَىٰ جَدُّ رَبِّنَا مَا اتَّخَذَ صَاحِبَةً وَلَا وَلَدًا {3}

Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu umetukuka; hakuji­fanyia mke wala mwana.

وَأَنَّهُ كَانَ يَقُولُ سَفِيهُنَا عَلَى اللَّهِ شَطَطًا {4}

Na kwa hakika mpumbavu miongoni mwetu alikuwa akise­ma juu ya Mwenyezi Mungu ya kupituka mipaka.

وَأَنَّا ظَنَنَّا أَنْ لَنْ تَقُولَ الْإِنْسُ وَالْجِنُّ عَلَى اللَّهِ كَذِبًا {5}

Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawatasema uwongo juu ya Mwenyezi Mungu.

وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِنَ الْإِنْسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا {6}

Na hakika walikuwako wanaume katika watu walio kuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume katika majini; kwa hivyo wakawazidisha mzigo.

وَأَنَّهُمْ ظَنُّوا كَمَا ظَنَنْتُمْ أَنْ لَنْ يَبْعَثَ اللَّهُ أَحَدًا {7}

Na hakika wao walidhani, kama mlivyodhani nyinyi, kuwa Mwenyezi Mungu hatam­tuma Mtume.

Aya 1 – 7: Kundi Moja La Majini

Maana

Sema: Nimepewa wahyi ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur’an ya ajabu!

Jinni ni uhakika na uhalisia, hatii shaka juu hilo mumin, kwa sababu Aya za Qur’an yenye hikima, zimethibitisha hilo, kwa njia isiyokubali shaka wala taawili (tafsiri nyingine). Tutazifanyia vipi taawili kauli zake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu na masanamu na sinia kubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiy­oondoka mahali pake.” Juz. 22 (34:13). “Akasema Afriti katika majini: mimi nitakuletea” Juz. 19 (27:39). “Sisi tumesikia Kitabu kilichoteremsh­wa baada ya Musa.” Juz. 26 (46:30). Pia Aya zilizo katika sura hii tuliyo nayo.

Je, tuziletee taawili ya virusi vya magonjwa, au redio na vinginevyo kati­ka vifaa vya elektroni?

Ukisema: Sayansi haikuthibitisha kuweko majini, nasi tutasema: Je, katika sayansi kuna linalopinga kuweko majini? Je, sayansi imemaliza kugundua vilivyomo ulimwenguni vyote, vya dhahiri na batini? Ni mtaalamu gani wa zamani au wa sasa anayejijua uhakika wake na akili yake? Au hata kuujua mwili wake wa hisia na wa dhahiri, ikiwemo mishipa na nywele?

Asiyejijua yeye mwenyewe hawezi kumjua mwenginewe; hasa yaliyo katika ulimwengu wa ghaibu.

Wahyi umethibitisha kuweko majini na Malaika, kwa hiyo ni wajibu kuamini kuweko; atakayekanusha, basi ni lazima athibitishe ukanusho wake kwa akili au wahyi; sawa na ilivyothibitishwa.

Baada ya hayo, ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimjulisha Nabii wake mtukufu kuwa kundi la majini walimsikiliza akisoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, wakakifahamu na kuzingatia maana yake; wakapigwa na mshangao kutokana na mpangilio na maana yake makuu; wakaambiana: jamani mnaionaje hii Qur’an? Je, mmeshawahi kusikia kitu mfano wake? Hakika ni muujiza na kwamba Inaongoza kwenye uwongofu, inaelekeza, kutoa mwongozo, kuaamrisha na kupendekeza kwenye kila heri. Pia inafa­hamisha, kukataza na kuonya kila shari.

Kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu,

kwa sababu Yeye ni Muweza wa kila kitu. Na mwenye uweza wa kila kitu basi hahitajii washirika, na kama atataka msaada maana yake ni kuwa anashindwa, na mwenye kushindwa hawezi kuwa Mungu.

Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu umetukuka; hakujifanyia mke wala mwana.

Ametakata Mola wetu na kujifanyia watoto na ametakata kuwagusa wanawake. Vipi awe hivyo na hali Yeye ni mwenye kujitosha mwenye kusifika.

Na kwa hakika mpumbavu miongoni mwetu alikuwa akisema juu ya Mwenyezi Mungu ya kupituka mipaka.

Makusudio ya mpumbavu hapa ni mjinga asiyejua. Hapa kuna ishara kwamba katika majini kuna kikundi kikiamini utatu: Mungu, mwana na mkewe. Hakuna mwenye shaka kwamba hii ni kupituka mipaka na ni upumbavu.

Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawatasema uwongo juu ya Mwenyezi Mungu.
Viongozi wa dini katika majini walikuwa wakiwaambia wafuasi wao ubatilifu na upotevu; miongoni mwayo ni kuwa Mwenyezi Mungu ana mke na watoto. Basi wafuasi wao wenye akili za juu wakawa wanawaami­ni kwa kuona kuwa hakuna yeyote anayeweza kujasiri kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo na kumsifia kwa sifa zisizokuwa zake. Lakini waliposikia Qur’an wakaamini kwamba viongozi wao wanamzulia Mwenyezi Mungu na kumsifu kwa sifa zisizoafikiana naye.

Jambo la kuangalia hapa ni kuwa majini walisikia hikima ya Qur’an kwa mara ya kwanza, wakaielewa na kuwaidhikia nayo. Na sisi tunasikia Qur’an na kuisoma mara kwa mara na hakuna nyumba yoyote ya mwisla­mu isiyokuwa na msahafu, lakini hatunufaiki na mawaidha yake wala kuongoka kwa mwongozo wake. Je, majini wana nafsi safi au wana akili timamu zaidi au ni kuwa katika maisha yao hawana matamanio na vishaw­ishi?1

Na hakika walikuwako wanaume katika watu walio kuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume katika majini; kwa hivyo wakawazidisha mzigo.

Wametofutiana katika kufasiri Aya hii. Lillo karibu zaidi na ufahamu ‧ tofauti na walivyosema wafasiri wengi ‧ ni kuwa makusudio ya wanaume katika watu ni wale wenye akili za juu juu, na wanaume katika majini ni wale watu wanaowavunga wenzao kuwa wana mawaasiliano na majini na wanaweza kuwaita wakati wowote wanapotaka na kuwatumia watakavyo.

Kwa hiyo maana ni kuwa watu wasiokuwa na akili walikuwa wakitaka hifadhi kwa watu waliokuwa wakidai kuwa na mawasiliano na majini ili wajikinge na hatari ya majini, au wawafahamishe yatakayotokea au wawakurubishie yaliyo mbali au kulipeleka mbali lililo karibu. Ama kuwazidishia mzigo ni kuwa wavungaji walikuwa wakiwataka malipo wasiyoyaweza.

Na hakika wao walidhani, kama mlivyodhani nyinyi, kuwa Mwenyezi Mungu hatamtuma Mtume.

Wao ni makafiri katika watu na nyinyi ni nyinyi majini. Maana ni kuwa waumini wa kijini waliwaambia makafiri katika kaumu yao kuwa nyinyi mna wanaofanana nanyi katika watu wasioamini ufufuo na hisabu.

وَأَنَّا لَمَسْنَا السَّمَاءَ فَوَجَدْنَاهَا مُلِئَتْ حَرَسًا شَدِيدًا وَشُهُبًا {8}

Nasi tuliigusa mbingu, tukaiona imejaa walinzi wenye nguvu na vimondo.

وَأَنَّا كُنَّا نَقْعُدُ مِنْهَا مَقَاعِدَ لِلسَّمْعِ ۖ فَمَنْ يَسْتَمِعِ الْآنَ يَجِدْ لَهُ شِهَابًا رَصَدًا {9}

Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza, lakini sasa anayetaka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia!

وَأَنَّا لَا نَدْرِي أَشَرٌّ أُرِيدَ بِمَنْ فِي الْأَرْضِ أَمْ أَرَادَ بِهِمْ رَبُّهُمْ رَشَدًا {10}

Nasi hatujui kama wanataki­wa shari wale wanaokaa kwenye ardhi au Mola wao anawatakia uwongofu.

وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ كُنَّا طَرَائِقَ قِدَدًا {11}

Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine kati­ka sisi ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali.

وَأَنَّا ظَنَنَّا أَنْ لَنْ نُعْجِزَ اللَّهَ فِي الْأَرْضِ وَلَنْ نُعْجِزَهُ هَرَبًا {12}

Nasi tulijua kuwa hatu­tomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumshinda kwa kukimbia.

وَأَنَّا لَمَّا سَمِعْنَا الْهُدَىٰ آمَنَّا بِهِ ۖ فَمَنْ يُؤْمِنْ بِرَبِّهِ فَلَا يَخَافُ بَخْسًا وَلَا رَهَقًا {13}

Nasi tulipousikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake hao­gopi kupunjwa wala kudhulu­miwa.

وَأَنَّا مِنَّا الْمُسْلِمُونَ وَمِنَّا الْقَاسِطُونَ ۖ فَمَنْ أَسْلَمَ فَأُولَٰئِكَ تَحَرَّوْا رَشَدًا {14}

Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo katika

وَأَمَّا الْقَاسِطُونَ فَكَانُوا لِجَهَنَّمَ حَطَبًا {15}

Na ama walioacha haki, hao wamekuwa kuni za Jahannamu.

وَأَنْ لَوِ اسْتَقَامُوا عَلَى الطَّرِيقَةِ لَأَسْقَيْنَاهُمْ مَاءً غَدَقًا {16}

Na lau kama wangelisimama sawasawa juu ya njia tungeli­wanywesha maji kwa wingi.

لِنَفْتِنَهُمْ فِيهِ ۚ وَمَنْ يُعْرِضْ عَنْ ذِكْرِ رَبِّهِ يَسْلُكْهُ عَذَابًا صَعَدًا {17}

Ili tuwajaribu kwa hayo, na anayepuuza kumkumbuka Mola wake atamsukuma kwenye
adhabu ngumu

Aya 8 – 17: Tulizigusa Mbingu

Maana

Nasi tuliigusa mbingu, tukaiona imejaa walinzi wenye nguvu na vimondo.

Neno kugusa tumelitarjumu kutokana na neno la kiarabu lamd ambalo asili yake ni kugusa kwa mkono, lakini mara nyingi linatumika kwa kutaka; hasa likinyumbuliwa na kuwa iltimas.

Aya hii inarudi madai ya makuhani na wanaodai kuwa na mawasiliano na majini yaliyooelezwa kwenye Aya zilizotangulia hii. Inavunja madai yao kwa kukiri majini wenyewe kuwa hawana uwezo wa kufika mbinguni kusikiliza, kwa sababu ina ulinzi mkali na vimondo.

Ni sawa liwe hili ni uhakika au ni kinaya cha kutojua majini ghaibu, laki­ni lengo la kwanza ni kutanabaisha kuwa makuhani na wanaodai kuwasil­iana na majini wanamzulia Mwenyezi Mungu na majini, kwa sababu ilimu ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu peke yake:

 وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُطْلِعَكُمْ عَلَى الْغَيْبِ {179}

“Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwafunulia mambo ya ghaibu,” Juz. 4 (3:179)

وَعِنْدَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ {59}

“Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye.” Juz. 7 (6:59).

Umetangulia mfano wake katika Juz. 14 (15:17-18), Juz. 12 (37: 6-7) na Juzuu hii tuliyo nayo (67:5).

Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusik­iliza, lakini sasa anayetaka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia!

Dhahiri ya Aya hii inafahamisha kuwa majini, kabla ya kuja Mtume (s.a.w.), waliwahi kupanda sehemu fulani mbinguni, na kwamba walikuwa wakisikia sauti au maneno, kisha wakazuliwa zama za Mtume Muhammad (s.a.w).

Hii haimaanishi kwamba wao walikuwa wakifichua habari za ghaibu mbinguni, hapana! Isipokuwa walisikia kitu tu mbinguni, na si lazima kitu hicho kiwe ni ghaibu; bali haiwezekani kabisa kuwa ni katika aina za ghaibu, kwa sababu ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu tu peke yake kwa nukuu ya Qur’an.

Mbinguni ni makazi ya Malaika lakini pamoja na hivyo:

قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنْتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ {32}

“Wakasema: Utakatifu ni wako hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundis­ha.” Juz. 1 (2:32).

Je, yuko aliye mtukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi kuliko Muhammad (s.a.w.), lakini pamoja na hayo alisema:

 وَلَوْ كُنْتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ {188}

“Na lau kama ningelijua ghaibu ningejizidishia kheri nyingi, wala isinge­nigusa dhara.”
Juz. 9 (7:188).

Ikiwa mtukufu wa viumbe wa Mwenyezi Mungu hajui ghaibu hata katika mambo yanayomuhusu yeye mwenyewe, vipi majini watajua heri au shari itakayowatokea watu baadae?

Nasi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanaokaa kwenye ardhi au Mola wao anawatakia uwongofu.

Hii ni kauli ya majini; maana yake ni kuwa vipi anadhania mpumbavu kwamba sisi tuna ilimu ya ghaibu na kujua heri au shari itakayotokea mbele; na kwamba sisi tunawapa hayo makuhani, na hali sisi hatujui aliy­oyakadiria Mwenyezi Mungu kwa yeyote katika watu wa ardhi wala kwa watu wetu?

Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine katika sisi ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali.

Majini wanajisimulia wao wenyewe kuwa miongoni mwao wamo wema na waovu, na kwamba wao wamegawanyika mataifa na madhehebu mbal­imbali, sawa na walivyo watu.

Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumshinda kwa kukimbia.

Baada ya majini kuisikia Qur’an waliamini kuwa Mwenyezi Mungu ambaye imetukuka hikima yake, hashindwi na atakayemtaka wala ham­ponyoki atakayemkimbia.

Nasi tulipousikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa.

Makusudio ya mwongozo ni Qur’an. Maana ni kuwa majini waliisikia Qur’an wakaiamini kwa ujumla na kwa ufafanuzi, wakiwa na yakini na uadilifu wa Mwenyezi Mungu, kwamba mwenye kufanya mema akiwa na imani basi hahofii kudhulumiwa wala kupunjwa.
Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo katika sisi wanaoacha haki.

Hili ni fungu la pili la majini baada ya uislamu. Ama fungu la kwanza lil­ioelezwa kwenye Aya 11 ya sura hii tuliyo nayo, wema na walio kinyume, hilo ni kwa mtazamo wa kabla ya kusilimu. Hakuna tofauti katika hilo isipokuwa namna ya kuita tu, wema waliitwa hivyo kabla ya uislamu na wakaitwa waislmu baada ya uislamu.

Basi waliosilimu, hao ndio waliotafuta uwongofu.

Waliosilimu waliutafuta uwongofu wakaupata na wakajichagulia heri wakawa wazuri kwayo.

Na ama walioacha haki, hao wamekuwa kuni za Jahannamu.

Sheikh Ismail Haqi, katika tafsiri yake: uhul-bayaa anasema: “Alqasie ni yule aliyoiacha haki na uqsie ni yule anayeiendea haki. Jina qasie limetu­mika sana kuitwa kundi la Muawiya, kutokana Hadith ya Mtume alipokuwa akimwambia Ali bin Abi Twalib: Utapigana na nakithin, na qasitia na mariqiia (wavunja ahadi, walioiacha haki na waliochomoka). Kwa hiyo waliovunja ahadi ni watu wa Aisha waliovunja baia, walioiacha haki ni watu wa Muawiya, kwa vile waliiacha haki pale walipopigana na Imam wa haki na waliochomoka ni makhawariji, kwa sababu walitoka kwenye dini ya Mwenyezi Mungu, wakahalalisha kupigana na khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.).

Na lau kama wangelisimama sawasawa juu ya njia tungeliwanywesha maji kwa wingi.

Haya ni maneno mengine wakikusudiwa majini na watu. Makusudio ya njia hapa ni sharia ya haki na uadilifu. Maji mengi ni kinaya cha raha na ukunjufu wa riziki, kwa sababu maji ni asili ya uhai. Maana ni kuwa lau watu wangelimwamini Mwenyezi Mungu kwa ukweli, wakatumia sharia kwa uadilifu na wakajiepusha na dhulma na uadui, basi wangeliishi katika ukunjufu, raha na amani.

Ili tuwajaribu kwa hayo.

Yaani hayo ya raha. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawapa neema kisha aangalie, wakizidi imani na ikhlasi kwayo basi watakuwa wema duniani na Akhera na wakiibadilisha basi atakuwa anawangoja.

Na anayepuuza kumkumbuka Mola wake atamsukuma kwenye adhabu ngumu.

Kila anayekumbushwa haki akaidharau, Mwenyezi Mungu atamwadhibu adhabu chungu.

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّهِ أَحَدًا {18}

Na hakika misikiti yote ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuombe yeyote pamoja na
Mwenyezi Mungu.

وَأَنَّهُ لَمَّا قَامَ عَبْدُ اللَّهِ يَدْعُوهُ كَادُوا يَكُونُونَ عَلَيْهِ لِبَدًا {19}

Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu aliposimama kum­womba, wao walikuwa karibu kumzonga!

قُلْ إِنَّمَا أَدْعُو رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِهِ أَحَدًا {20}

Sema: Hakika mimi namwom­ba Mola wangu tu, wala simshirikishi na yeyote.

قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا {21}

Sema: Mimi sina mamlaka ya kuwadhuru wala kuwaon­goza.

قُلْ إِنِّي لَنْ يُجِيرَنِي مِنَ اللَّهِ أَحَدٌ وَلَنْ أَجِدَ مِنْ دُونِهِ مُلْتَحَدًا {22}

Sema: Hakika hapana yeyote awezaye kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitap­ata pa kukimbilia isipokuwa kwake Yeye tu.

إِلَّا بَلَاغًا مِنَ اللَّهِ وَرِسَالَاتِهِ ۚ وَمَنْ يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا {23}

Ila kwa kufikisha Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu
humo milele.

حَتَّىٰ إِذَا رَأَوْا مَا يُوعَدُونَ فَسَيَعْلَمُونَ مَنْ أَضْعَفُ نَاصِرًا وَأَقَلُّ عَدَدًا {24}

Hata watakapoyaona wanayoahidiwa, ndipo watakapojua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi.

قُلْ إِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ مَا تُوعَدُونَ أَمْ يَجْعَلُ لَهُ رَبِّي أَمَدًا {25}

Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayoahidiwa, au Mola wangu atayawekea muda mrefu.

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا {26}

Ni Mwenye kujua ghaibu, wala hamdhihirishii yeyote ghaibu yake.

إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِنْ رَسُولٍ فَإِنَّهُ يَسْلُكُ مِنْ بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ رَصَدًا {27}

Isipokuwa Mtume aliyemridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.

لِيَعْلَمَ أَنْ قَدْ أَبْلَغُوا رِسَالَاتِ رَبِّهِمْ وَأَحَاطَ بِمَا لَدَيْهِمْ وَأَحْصَىٰ كُلَّ شَيْءٍ عَدَدًا{28}

Ili ajue kwamba wao wame­fikisha ujumbe wa Mola wao, Na anajua vyema yote waliyo nayo na amedhibiti idadi ya kila kitu.

Aya 18 – 28: Hakika Miskiti Ni Ya Mwenyezi Mungu

Maana

Na hakika misikiti yote ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuombe yey­ote pamoja na Mwenyezi Mungu.

Wametofautiana kuwa kauli hii ni ya Mwenyezi Mungu au ni ya majini? Vyovyote iwavyo maana ni moja, kwamba sehemu zote za kuabudu ni kwa ajili ya kumwabudu Mwenyezi Mungu na kumtii Yeye tu; iwe zime­jengwa na kuimarishwa na waislamu au wengineo.

Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu aliposimama kumwomba, wao walikuwa karibu kumzonga!

Makusudio ya mja wa Mwenyezi Mungu hapa ni Muhammad (s.a.w.), aliyemuomba, ni Mwenyezi Mungu; na waliomzonga ni maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Maana ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alipotoa mwito wa haki vilijitokeza vikundi vya upotevu na kumzonga kutokana na wingi wao; kama nywele au sufu zinapojizonga zonga. Katika hilo Imam Ali (a.s.) anasema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliingia kwenye kila majonzi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Ndugu zake wa karibu walimbadilikia na wa mbali wakaungana dhidi yake.
Waarabu walilegeza hatamu zao dhidi yake na wakamvalia njuga kumpiga vita, mpaka wakamjia maadui kutoka sehemu mbali mbali.

Linalofahamisha kuwa haya ndio makusudio yake ni kauli yake Mwenyezi Mungu moja kwa moja:

Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu tu, wala simshirikishi na yeyote.

Sema ewe Muhammad kuwaambia wale walioungana kukupiga vita: Je, nimewakosea nini? Je, nimewataka ujira au nimetaka cheo? Hapana isipokuwa ninamwabudu Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhlasi. Yeye ndiye aliyoyeumba ulimwengu wote pamoja na ardhi yake na mbingu yake, je hii ni dhambi isiyosameheka?

Sema: Mimi sina mamlaka ya kuwadhuru wala kuwaongoza; yaani kuwanufaisha. Maana ni kuwa sema ewe Muhammad kuwaambia washirikina: Mimi ni mtu kama nyinyi tu sidai kuwa na uweza wa hatima yenu, wala madhara na manufaa yenu; amri yote ni ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Sema: Hakika hapana yeyote awezaye kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipokuwa kwake Yeye tu. Ila kwa kufikisha Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) akizembea kufikisha ujumbe alioaminiwa nao basi atakuwa hana pa kumkimbia Mwenyezi Mungu.

Aya hii ni miongoni mwa makumi ya Aya yanayofahamisha kwa uwazi kuwa Uislamu unakataa fkra ya kuweko wasta (wa katikati) baina ya Mwenyezi Mungu na mja wake, na inamweka mja mbele ya Mola wake moja kwa moja; azungumze naye, amnong’oneze vile atakavyo na ajiku­rubishe kwake kwa kufanya heri bila ya kuweko muombezi wala mgombezi.

Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele.

Hili ni onyo, hadhari na kiaga kwa waasi waliopituka mipaka, kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anapasa kutiiwa, hata kama hakutoa tahadhari na onyo; sikwambii tena akitoa onyo na tahadhari kama hii.

Hata watakapoyaona wanayoahidiwa, ndipo watakapojua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi.

Washirikina walikuwa wakiwaona dhaifu wasisidizi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na wakiwaona ni wachache, wakimwambia: sisi ni zaidi yako wewe kwa mali na watu. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawaambia kesho mtajua ni nani aliye na nguvu na ninani aliye dhalili. Amesema kweli Mwenyezi Mungu mtukufu, hazikupita siku Uislamu ukawa na nguvu na akawainua waislamu kwa uweza wake na makafiri watakuwa na adhabu ya kuungua huko Akhera.

Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayoahidiwa, au Mola wangu atayawekea muda mrefu.

Washirikina waliposikia kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘ndipo watakapojua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi,’ wal­imuuliza Mtume (s.a.w.): yatakuwa lini hayo; ndio Mwenyezi Mungu akamwamrisha Nabii wake awaambie ilimu yake iko kwa Mola wangu na wala sijui iko karibu au iko mbali.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Au atayawekea muda inafupishwa na neno mbali; kama ilivyo katika kauli yake:

 وَإِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ أَمْ بَعِيدٌ مَا تُوعَدُونَ {109}

“Wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyoahidiwa. Juz. 17 (21:109).

Ni Mwenye kujua ghaibu, wala hamdhihirishii yeyote ghaibu yake, isipokuwa Mtume aliyoemridhia.

Ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu na yule aliyemwamini kwa wahyi wake na akamchagua kupeleka ujumbe wake kwa waja wake, huyo anaweza kujua ghaibu aliyojulishwa na Mwenyezi Mungu: “Utakatifu ni wako hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha.” Juz. 1 (2:32).

Kundi la wafasiri, akiwemo Ar-Razi na Al-Maraghi wamesema asiyekuwa Mtume anaweza kujua ghaibu na kuitolea habari, lakini kauli hii haifikia­ni na dhahiri ya kauli yake isipokuwa Mtume aliyemridhia.

Ndio, ni kweli kuwa kuna baadhi ya watu wanaweza kutabiri mambo yata­kayotokea mbele na wakawa wakweli katika nyingi ya dhana zao, lakini hayo wanayatoa kutokana na vigezo na alama zinazowadhihirikia kwa ufahamu na ilimu. Sasa ni wapi na wapi haya na ilimu ya ghaibu ambayo haidhihirishi Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa mitume na manabii?

Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.

Yanayokuja haraka kwenye ufahamu wetu kutokana na Aya hii, ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawalinda manabii wakiwa wanatekeleza ujumbe wake na anawahifadhi na kila kikwazo cha kufikisha ujumbe kwa njia yake; ni sawa kizuizi hicho kiwe kinatoka ndani, kama vile kupuuza na kusahau, au kiwe kinatoka nje, kama vile ushawishi wa maadui nk. Kwa maneno mengine ni kuwa Aya hii inathibitisha umasumu wa manabii kati­ka utekelezaji wa wahyi.

Ili ajue yaani ifichuke ilimu ya Mwenyezi Mungu na uhakika wake, kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao, kwa uhalisia wake na Yeye anayajua vyema yote walio nayo. Yaani kila waliyosema manabii; haimpiti hata herufi moja. Fauka ya hayo ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amevizunguka kwa ujuzi viumbe vyake vyote - vidogo na vikub­wa.

Na amedhibiti idadi ya kila kitu. Atashindwaje kuwadhibiti wajumbe wake kwenye kauli zao na pumzi zao na hali wao wanafikisha risala yake kwa waja wake? Lengo la msisitizo huu ni kutanabahisha kwamba manabii wamelindwa; hawakosei katika kufikisha wahyi ‧ hawapunguzi herufi wala kugeuza herufi kwa herufi nyingine.

وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ {3}

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ {4}

“Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni wahyi uliotolewa.” Juz. 27 (53: 3-4).
  • 1. Inawezekana kuwa hiyo ni kwa wale majini wa mwanzo mwanzo mwa Uislamu, kwani hata waislamu wa mwanzo pia walikuwa wakiifanyia kazi Aya mara tu walipoisikia. ‧Mtarjumu.