read

Sura Ya Sabini Na Saba: Al-Mursalat

Imeshuka Makka Ina Aya 50.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَالْمُرْسَلَاتِ عُرْفًا {1}

Naapa kwa wanaotumwa kwa wema!

فَالْعَاصِفَاتِ عَصْفًا {2}

Na wanaokwenda kwa kasi!

وَالنَّاشِرَاتِ نَشْرًا {3}

Na kwa wanotawanya mtawanyo kamili!

فَالْفَارِقَاتِ فَرْقًا {4}

Na wanaofarikisha mbali mbali!

فَالْمُلْقِيَاتِ ذِكْرًا {5}

Na wanaopeleka ukumbusho!

عُذْرًا أَوْ نُذْرًا {6}

Kuondoa udhuru au kuonya!

إِنَّمَا تُوعَدُونَ لَوَاقِعٌ {7}

Hakika mnayoahidiwa bila ya shaka yatakuwa!

فَإِذَا النُّجُومُ طُمِسَتْ {8}

Basi nyota zitakapofutwa.

وَإِذَا السَّمَاءُ فُرِجَتْ {9}

Na mbingu zitakapopasuliwa.

وَإِذَا الْجِبَالُ نُسِفَتْ {10}

Na milima itakapopeperushwa­

وَإِذَا الرُّسُلُ أُقِّتَتْ {11}

Na wajumbe watakapo­ wekewa wakati.

لِأَيِّ يَوْمٍ أُجِّلَتْ {12}

Kwa siku gani hiyo wamewekewa muda?

لِيَوْمِ الْفَصْلِ {13}

Kwa siku ya upambanuzi!

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الْفَصْلِ {14}

Na nini kitakachokujulisha ni nini siku ya upambanuzi?

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {15}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

أَلَمْ نُهْلِكِ الْأَوَّلِينَ {16}

Je, hatukuwaangamiza walio­tangulia?

ثُمَّ نُتْبِعُهُمُ الْآخِرِينَ {17}

Kisha tukawafuatilizia wengine?

كَذَٰلِكَ نَفْعَلُ بِالْمُجْرِمِينَ {18}

Ndio kama hivyo tutawafanya wakosefu!

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {19}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

أَلَمْ نَخْلُقْكُمْ مِنْ مَاءٍ مَهِينٍ {20}

Je, hatukuwaumba kwa maji ya kudharaulika?

فَجَعَلْنَاهُ فِي قَرَارٍ مَكِينٍ {21}

Kisha tukayaweka mahali makini pa utulivu?

إِلَىٰ قَدَرٍ مَعْلُومٍ {22}

Mpaka makadirio maalumu?

فَقَدَرْنَا فَنِعْمَ الْقَادِرُونَ {23}

Tukakadiria na Sisi ni wabora wa kukadiria.

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {24}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

أَلَمْ نَجْعَلِ الْأَرْضَ كِفَاتًا {25}

Je, hatukuifanya ardhi ni chombo?

أَحْيَاءً وَأَمْوَاتًا {26}

Kwa walio hai na wafu?

وَجَعَلْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ شَامِخَاتٍ وَأَسْقَيْنَاكُمْ مَاءً فُرَاتًا {27}

Na ndani yake tukaweka mil­ima mirefu na tukawanywe­sha maji matamu?

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {28}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

Aya 1 – 28: Naapa Kwa Wanotumwa Kwa Wema

Maana

Sura hii imeelezea kuhusu Akhera na adhabu yake na vituko vyake. hayo yametangulia kwenye Aya kadhaa; ndio maana tutafupiliza kwa kufasiri kilugha, bila ya kuingia ndani, kama tulivyofanya katika sura yingine.

Naapa kwa wanaotumwa kwa wema.

Imesekana kuwa wanaotumwa hapa ni malaika, kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu anawatuma malaika kwa ajili ya kufikisha wahyi kwa mitume na mengineyo ya kheri. Pia imesemekana makusudio ni upepo na tafsri iwe Naapa kwa zinazo­tumwa kwa kufuatana, yaani Mwenyezi Mungu anatuma Pepo kwa kufu­atana.

Na wanaokwenda kwa kasi na kwa wanotawanya mtawanyo kamili!

Malaika wanaeneza rehema za Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake au kwamba Pepo zinatawanya mawingu angani.

Na wanaofarikisha mbali mbali!

Malaika wanashuka na Aya za Mwenyezi Mungu ambazo zinafarikisha baina ya haki na batili; au Pepo zinafarikisha mvua pembe za ulimwengu.

Na wanaopeleka ukumbusho! Kuondoa udhuru au kuonya.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawatuma malaika na wahyi ili kuwaonya waja na wala wasiwe na udhuru. kwa tafsiri ya upepo ni kuwa makusudio ya ukumbusho ni mvua, kwa sababu inakumbusha kuhusu Mwenyezi Mungu na rehema yake; kwa hiyo mumin anamshukuru Mwenyezi Mungu inaposhuka mvua na kujiondolea udhuru wa uzembe alioufanya nyuma. Na kafiri anazidi uasi kwa kuwa mvua inazidisha utajiri wake, na hatimaye mvua au upepo humuonya na adhabu kali.

Huu ni muhtasari wa waliyoyasema wafasiri kuhusu Aya hizi saba. Tafsiri zote mbili (malaika na upepo), zinafaa, kwa sababu Mwenyezi Mungu anapeleka upepo; kama alivyosema:

وَهُوَ الَّذِي يُرْسِلُ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ ۖ {57}

“Na yeye ndiye azipelekaye pepo kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema yake.” Juz. 8 (7:57).

Vile vile amewapeleka malaika; kama alivyosema:

اللَّهُ يَصْطَفِي مِنَ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا {75}

“Mwenyezi Mungu huteua wajumbe miongoni mwa Malaika.” Juz. 17 (22:75).

Vyovyote iwavyo sisi hatutaulizwa kuhusu utafiti huu mbele ya Mwenyezi Mungu, wala kuujua hakuna mahusiano yoyote na maisha yetu, kwa sababu yoyote ile. Kwa hiyo bora hilo tuliachie ujuzi wake Mwenyezi Mungu Mtukufu, tukiamini kuwa yeye pekee ndiye msababishaji wa sababu.

Hakika mnayoahidiwa bila ya shaka yatakuwa!

Mnayoahidiwa ni siku ya kiyama. Maana ni kuwa Kiyama kitafika tu, hilo halina shaka.

Basi nyota zitakapofutwa, yaani kuondoka mwanga wake.

Na mbingu zitakapopasuliwa, sayari zake zitapasuliwa.

Na milima itakapopeperushwa, kuwa vumbi na kwenda na upepo.

Na wajumbe watakapowekewa wakati.

Wajumbe hapa ni malaika. Mwenyezi Mungu amewawekea wakati maalum wa kuja kutoa ushahidi kwa waja, kisha wawapeleke wanaomcha Mungu Peponi na wakosefu kwenye Jahannam.

Kwa siku gani hiyo wamewekewa muda hao mitume?

Kwa siku ya upamabanuzi!

Swali limekuja kwa kuikuza siku yenyewe na vitu vyake. Imeitwa siku ya upambanuzi, kwa vile watu watapambanuliwa kwa haki, bila ya upen­deleo.

Na nini kitakachokujulisha ni nini siku ya upambanuzi?

Yaani nini kitakachokufahamisha kuhusu siku hiyo ambayo vituko vyake havina mfano? Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha! Hili ni onyo kwa wenye kukad­hibisha siku ya malipo. Vile vile kwa mwenye kuiamini lakini asiifanyie kazi.

Je, hatukuwaangamiza waliotangulia? Kama vile kaumu ya Nuh, kwa vile waliwakadhibisha mitume?

Kisha tukawafuatilizia wengine? Kama kaumu ya Lut.

Ndio kama hivyo tutawafanya wakosefu! Waliomkadhibisha Muhammad (s.a.w.). Kwa vile sababu ni moja -kuipinga haki.

Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha!

Aya hii imekarika mara kumi katika sura hii kufuatana na maana ya Aya iliyo kabla yake.

Je, hatukukuwaumba kwa maji ya kudharaulika? Kisha tukayaweka mahali makini pa utulivu? Mpaka makadirio maalumu? Tukakadiria na Sisi ni wabora wa kukadiria.

Je, mnakana ufufuo na mnasema: Ni nani atakayefufua mifupa iliy­ochakaa, na hali nyinyi mnajua kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba kutokana na maji ya yaliyo duni, na mkawa kwenye viza vitatu kwa muda maalum, mkigura kutoka umbile moja hadi jingine, na muda huu akaupan­ga kwa umakini kabisa. Baada ya yote haya bado mnakufuru neema za Mwenyezi Mungu na mnakadhibisha uweza wa ufufuo, hisabu na malipo?

Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha! Je, hatukuifanya ardhi ni chombo? Kwa walio hai na wafu? Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameifananisha ardhi na chombo, kwa vile inakusanya na kuhifadhi. Maana ni kuwa ardhi inakusanya na kuhifadhi walio hai kwenye mgongo wake na wafu tumboni mwake.
Na ndani yake tukaweka milima mirefu yenye kuthibiti, ili ardhi isiyumbe na tukawanywesha maji matamu? Ambayo ni uhai wenu na wa ardhi, inayowapatia heri na baraka. Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha!

انْطَلِقُوا إِلَىٰ مَا كُنْتُمْ بِهِ تُكَذِّبُونَ {29}

Nendeni kwenye yale mliyokuwa mkiyakadhibisha!

انْطَلِقُوا إِلَىٰ ظِلٍّ ذِي ثَلَاثِ شُعَبٍ {30}

Nendeni kwenye kivuli chenye mapande matatu!

لَا ظَلِيلٍ وَلَا يُغْنِي مِنَ اللَّهَبِ {31}

Hayaleti kivuli, wala hayae­pushi mwako.

إِنَّهَا تَرْمِي بِشَرَرٍ كَالْقَصْرِ {32}

Hakika Moto huo unatoa macheche kama majumba!

كَأَنَّهُ جِمَالَتٌ صُفْرٌ {33}

Kama kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano!

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {34}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

هَٰذَا يَوْمُ لَا يَنْطِقُونَ {35}

Hii ni siku ambayo hawatatamka.

وَلَا يُؤْذَنُ لَهُمْ فَيَعْتَذِرُونَ {36}

Wala hawataruhusiwa kutoa udhuru.

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {37}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

هَٰذَا يَوْمُ الْفَصْلِ ۖ جَمَعْنَاكُمْ وَالْأَوَّلِينَ {38}

Hii ndiyo siku ya upambanuzi.Tumewakusanya nyinyi na waliotangulia.

فَإِنْ كَانَ لَكُمْ كَيْدٌ فَكِيدُونِ {39}

Ikiwa mnayo hila, nifanyieni!

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {40}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي ظِلَالٍ وَعُيُونٍ {41}

Hakika wenye takua watakuwa katika vivuli na chemchem.

وَفَوَاكِهَ مِمَّا يَشْتَهُونَ {42}

Na matunda wanayoyapenda

كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {43}

Kuleni na kunyweni kwa raha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyatenda.

إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ {44}

Hakika ndio kama hivyo tunavyowalipa watendao mema.

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {45}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

كُلُوا وَتَمَتَّعُوا قَلِيلًا إِنَّكُمْ مُجْرِمُونَ {46}

Kuleni na mjifurahishe kidogo tu. Hakika nyinyi ni wakose­fu!

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {47}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ ارْكَعُوا لَا يَرْكَعُونَ {48}

Na wakiambiwa: Rukuuni hawarukui.

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِلْمُكَذِّبِينَ {49}

Ole wao, siku hiyo wanaokad­hibisha!

فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَهُ يُؤْمِنُونَ {50}

Basi ni mazungumzo gani baada yake watakayoyaami­ni?

Aya 29 – 50: Kivuli Chenye Mapande Matatu

Maana

Nendeni kwenye yale mliyokuwa mkiyakadhibisha.

Waliikadhibisha adhabu ya Mwenyezi Mungu, bali waliidharau pamoja na yule aliyewapa ahadi hiyo. Kesho mazabania wa Jahannam watawaambia kwa madharau; kama vile wao walivyodharau mitume: Haya nendeni, hivi sasa, kwenye lile mlilolifanyia mzaha.

Nendeni kwenye kivuli chenye mapande matatu kinachotokana na moshi wa Jahannam: pande la kwan­za litawafunika kichwani, pande la pili kuliani kwao na la tatu kushotoni. Hayaleti kivuli, wala hayaepushi na mwako. ni kivuli jina tu, lakini hakiwakingi wanaojifunika nacho na moto bali kinawazidishia adhabu juu ya adhabu. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na kivuli cha moshi mweusi, si baridi wala starehe.” Juz. 27 (56:43-44).

Hakika Moto huo unatoa macheche kama majumba! Kama kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano!

Yaani moto wa Jahannam utaruka na kujaa hewani, kila cheche itakuwa kubwa kama jumba na rangi kama ya ngamia wa rangi ya manjano.

Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha! Hii ni siku ambayo hawatatamka, wala hawataruhusiwa kutoa udhu­ru.

Siku ya Kiyama kuna sehemu baadhi ya watu watapewa idhini kusema, na wengine hawatapewa idhini. Tazama Juz. 23 (36:65). Imesemekana maana ni kuwa wakosefu hawatatamka yatakayowafaa wala hawatakuwa na udhuru kwa Mwenyezi Mungu.

Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha! Hii ndiyo siku ya upambanuzi.

Itapambanuliwa haki kwa viumbe.

Tumewakusanya nyinyi na waliotangulia, waliofanya makosa kama nyinyi na tumewakusanya nyote sehemu moja ili tuangalie hisabu, kisha mpelekwe kwenye makao mamoja ambayo ni Jahannam iliyo makao mabaya.

Ikiwa mnayo hila, nifanyieni!

Huu ndio mwisho wenu, ikiwa mna hila au nyenzo yoyote ya kuwazuia na adhabu basi ileteni. Hapa kuna kutahayariza kutokana na vitimbi vyao na hadaa yao katika maisha ya dunia.

Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha!

Hakika wenye takua watakuwa katika vivuli na chemchem na matun­da wanayoyapenda.

Hii ndio ada ya Qur’an Tukufu, inakutanisha adhabu ya wakosefu na thawabu kwa wanaomcha Mungu, kwa lengo la kupendekeza na kuhad­harisha. Wakosefu watakuwa na vivuli vya Jahannam na wenye takua watakua na vivuli vya Peponi, chemchem zinazopita na matunda aina kwa aina pamoja na takrima za hali ya juu; miongoni mwazo ni kauli ya malai­ka:

Kuleni na kunyweni kwa raha kwa sababu ya mliyokuwa mkiya­tenda.

Umetangulia mfano wake kwa herufi zake katika Juz. 27 (52:19).

Hakika ndio kama hivyo tunavyowalipa watendao mema.

Hii ndio desturi yetu katika viumbe:

 إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا {30}

“Hakika sisi hatupotezi ujira wa anayefanya mazuri.” 15 (18:30).

Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha!

Kuleni na mjifurahishe kidogo tu.
Maneno yanaelekezwa kwa wakosefu. Makusudio yake ni kuhadharisha na kutoa ahadi. Maana yake ni stareheni kwenye dunia, vile mtakavyo, lakini hizo ni siku chache, kisha zitaondoka starehe kama mawingu yanay­opita, hakika nyinyi ni wakosefu! Desturi ya Mwenyezi Mungu kwa wakosefu ni kuwapa muda kidogo, kisha awaonjeshe adhabu ya moto.

Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha!

Na wakiambiwa: Rukuuni hawarukui.

Mtume akiwaamuru kumnynyenyekea Mwenyezi Mungu wanapandwa na kiburi.

Sheikh Abdul-Qadir Al-Maghribi, katika kufasiri Aya hii anasema: “Imepokewa kuwa Mtume (s.a.w.) alimuuliza Hind, mke wa Abu Sufyan, bada ya kusilimu siku ya kuiteka Makka: Unauonaje Uisalmu? Akasema: “Ni mzuri isipokuwa mambo matatu: Kuinama ‧ yaani kurukui na kusuju­di katika Swala-ushungi, na huyu mtumwa mwesi kupanda Al-Kaa’ba ‧ akimkusudia Bilal na adhana yake kutoka juu ya Al-Kaa’ba.” Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Hakuna Swala bila ya kuinama, ushungi ni sitara nzuri kabisa, ama huyu mweusi basi ndio mja bora zaidi.”

Ole wao, siku hiyo wanaokadhibisha!

Basi ni mazungumzo gani baada yake watakayoyaamini?

Utukufu wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) umejitokeza kwenye Qur’an yote, kama ulivyojitokeza katika ulimwengu. Basi ambaye hatakinai wala kun­ufaika na Qur’an, huyo hawezi kukinaishwa na kitu chochote. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 9 (7:185).