read

Sura Ya Sabini Na Sita: Al-Insan

Imeshuka Makka Ina 31. Imesemekana isiyokuwa hivyo.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنْسَانِ حِينٌ مِنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُنْ شَيْئًا مَذْكُورًا {1}

Je, kilimpitia binaadamu kipin­di katika zama ambacho hakuwa kitu kinachotajwa?

إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ مِنْ نُطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا {2}

Hakika tumemuumba mtu kutokana na tone la manii lililochanganyika, tumfanyie mtihani. Tukamfanya ni mwenye kusikia, mwenye kuona.

إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا {3}

Hakika tumemwongoza njia, ama awe ni mwenye kushuku­ru, au mwenye kukufuru.

إِنَّا أَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ سَلَاسِلَ وَأَغْلَالًا وَسَعِيرًا {4}

Hakika tumewaandalia makafiri silsili na pingu na Moto mkali.

إِنَّ الْأَبْرَارَ يَشْرَبُونَ مِنْ كَأْسٍ كَانَ مِزَاجُهَا كَافُورًا {5}

Hakika watu wema watakuny­wa katika glasi zilizochanganyi­ka na kafuri.

عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا {6}

Ni chemchem watakayoinywa waja wa Mwenyezi Mungu, wakiitiririsha mtiririko.

Aya 1 – 6: Je, Kilimpitia Binadamu Kipndi

Maana

Je, kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho hakuwa kitu kinacho tajwa?

Wamesema wafasiri kuwa herfi hal, tuliyoifasiri kwa maana ya je, ni ya uhakika, kwa maana ya hakika kilimpitia…

Aya hii iko katika picha ya swali na maana yake ni kusisitiza na kuhakik­isha. Lengo la Aya ni kuwa mtu anatakikana afikirie akilini mwake na kuji­uliza kuhusu uweza uliyomfanya yeye aweko baada ya kutokuweko. Ni kitu gani kimemfanya apatikane? Amepita vipi kutoka hali moja hadi nyingine? Je, anakwenda wapi?

Katika hili Imam Ali (a.s.) anasema: “Amrehemu Mwenyezi Mungu mja aliyejua ametoka wapi, yuko wapi na anakwenda wapi.” Hili ndilo lengo la Aya hii. Ufuatao ni ufupi wa ufafanuzi wa yaliyoashiriwa na Aya hii na nyingine zinazofuatia katika hali ya kutoka mtu kwenye ngazi moja hadi nyingine mpaka kukamilika kwake. Ama kuhusu yuko wapi na anakwen­da wapi tumekwisha fafanua huko nyuma katika kufasiri Aya za dunia na Akhera:­

1. Je, kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho hakuwa kitu kinachotajwa?

Ulipita muda mrefu sana ambao mtu hakuwa na atahari yoyote ya kuweko: “Je hakumbuki mtu ya kwamba tulimuumba kabla na hali hakuwa cho­chote?” Juz. 16 (19:67). Wataalamu wanasema kuwa mtu alipatikana hapa ardhini tangu miaka milioni 5: ” Na Mola wako anawajua vilivyo waliomo mbinguni na waliomo ardhini.” Juz. 15 (17:55).

2. Kisha Mwenyezi Mungu akamuumba Adam, baba wa watu, kutokana na udongo:

“Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kutokana na udongo.” Juz. 3 (3:59). Hapa aligura mtu kutoka hali ya kukosekana hadi kupatikana akiwa mchanga usiokuwa na uhai.

3. Hakika tumemuumba mtu kutokana na tone la manii lililochanganyika, tumfanyie mtihani.

Hii ni ishara ya kugura mtu kutoka udongo hadi kuwa majimaji, ambayo ni tone la manii lililokuwa kutokana na mfungamano wa aina mbali mbali ali­zoziashiria Imam Ali (a.s.) kwa kauli yake: “Na jinsi yenye mchanganyiko wa udongo wa rangi tofauti, na vitu vyenye kufanana na kuafikiana, na vitu vilivyo kinyume visivyoafikiana, na viliyochanganyika vinavyobainika.”

Mingoni mwa atahari za udongo wa rangi tofauti ni tunavyomuona mtu akiwa na macho meusi na uso mweupe, katika vyenye kufanana na kuafikiana ni mifupa ya mikono na miundi na katika athari ya vilivyo kinyume visivyoafikiana ni mapenzi na chuki, tamaa na kukinai, kun­yenyekea na kutakabari, mapambano ya akili na matamanio n.k. Hapa ndio tunapata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Tumfanyie mti­hani,’ pale anapopata mapambano makali mtu baina ya dhamiri yake na matamanio yake.

4. Tukamfanya ni mwenye kusikia, mwenye kuona.

Hii ni ishara ya kugura mtu kutoka tone la manii lililopata uhai ndani ya tumbo lake baada ya kupita siku kadhaa akiwa kwenye giza lisilokuwa na usikizi wala uoni hadi kwenye mng’ao pamoja na usikizi na uoni, lakini bila ya akili wala utambuzi, sawa na mnyama.

5. Hakika tumemwongoza njia, ama awe ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaashiria kugura mtu kutoka kwenye maisha ya mnyama hadi kwenye maisha ya ubinadamu; yaani baada ya kutimia kwake kuwa mwili ulio na hisia, Mwenyezi Mungu akampa akili na utam­buzi ili aweze kupambanua baina ya haki na batili na uongofu na upotevu. Vile vile amempa uhuru ili kwa akili yake na uhuru wake aweze kubeba majukumu na kustahiki thawabu na adhabu, baada ya kubainishiwa na kupewa hoja.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameuletea ibara ya shukrani, uongofu, kwa sababu ni kumtii Mwenyezi Mungu, na uovu akauita ukafiri kwa sababu ni kumuasi yeye.

Kwa ufafanuzi zaidi wa hayo tutaashiria hali ya uwiano baina ya mtu na viumbe vingine wa ardhini kwa ujumla: Viumbe hivi vinagawanyika kwenye viumbe vilivyotulia, vizisivyokuwa na uhai wala kukua; kama vile mchanga, miamba na madini, na viumbe vingine vyenye uhai. Vyenye uhai navyo vinagawanyika mafungu matatu:

1. Uhai wa mimea; hii ina harakati na kukua bila ya kuwa na hisia wala utambuzi. Kwa hiyo mimea haisikii wala haioni, pia haina akili.

2. Ni maisha ya wanyama; miongoni mwa sifa za wanyama ni kuwa na harakati, kukua, kuhisi, kusikia na kuona, lakini bila ya kuwa na akili wala utambuzi kwa aghlab, au utambuzi wa kimafungu sio wa kiujumla

3. Ni maisha ya kiutu; miongoni mwa sifa za mtu ni kuwa na harakati, kukua, kusikia kuona, fauka ya hayo anakuwa na utambuzi wa kimafungu na wa kiujumla; kwa hiyo anajua mengi yaliyokuwa na yatakayokuwa. Ni kwa utambuzi huu na maarifa haya ndio akawa tofauti na viumbe wengine wote wa ardhini.

Kwa hiyo basi mtu anakuwa na uwiano na vitu vilivyotulia, kwa vile yeye alikuwa mchanga, anaoana na mimea kwa vile alikuwa tumboni mwa mama yake akikua pole pole na kutaharaki bila ya kusikia wala kuona, na anawiana na wanyama kwa sababu alipokuwa mtoto alikuwa na hisia, kusikia na kuona, lakini bila ya utambuzi na akili. Kisha akatofautiana na vyote kwa akili na utambuzi. Kuanzia hapa ndio akawa anabeba majuku­mu na kustahiki thawabu na adhabu, kinyume na viumbe wengine.

Hapa inatakikana kujiuliza: Ni nani aliyemgurisha mtu kutoka kipindi cha kutokuwepo, hadi kwenye mchanga uliotulia, na kutoka hapo hadi mmea unaotaharaki, hadi kufikia mnyama mwenye usikizi na hatimae binadamu kamili mwenye akili inayompa habari ya yaliyopita na yatakayokuja, akaweza kutengeneza maendeleo, na kutawala viumbe vingi, hata mnyama mwenye usikizi na uoni? Je, hali hii na mengineyo yasiyokuwa na idadi yana tafsiri nyingine zaidi ya kuweko muumba mwenye uwezo ambaye akili zinashindwa kumuwazia na ndimi haziwezi kumsifia?

Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria majukumu ya mtu kwa kauli yake: “Hakika tumemwongoza njia, ama awe ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru,” amefuatilia kutaja aliyowaandalia makafiri kwa kusema:

Hakika tumewaandalia makafiri silsili na pingu na Moto mkali.

Silisili ni za miguu na pingu ni za mikono na moto ni wa mwili.

Hakika watu wema watakunywa katika glasi zilizochanganyika na kafuri.

Glasi ni chombo cha kioo cha kunywea. Pia neno hili hutumika kwa kiny­waji chenyewe, na haya ndiyo maana yaliyokusudiwa hapa. Wafsiri wengi wamesema kuwa kinywaji cha watu wa peponi kina harufu nzuri, kama harufu ya kafuri, na sisi tunasema kuwa mchanganyiko wa kafuri ni uhakika, kama inavyofahamisha dhahiri ya Aya. Ikiwa ladha ya kafuri duniani inachukiza, basi sio lazima ya Peponi nayo iwe hivyo hivyo. Pombe ya dunia inaleta uzito kichwani na maumivu, lakini kinywaji cha pombe ya Peponi:

لَا فِيهَا غَوْلٌ وَلَا هُمْ عَنْهَا يُنْزَفُونَ {47}

“Hakina madhara, wala hakiwamalizikii.” Juz. 23 (37:47).

Ibn Abbas anasema: “Kila lilichotajwa na Mwenyezi Mungu katika Qur’an kuhusu vilivyo Peponi, hakiko duniani isipokuwa jina tu.”

Ni chemchem watakayoinywa waja wa Mwenyezi Mungu, waki­itiririsha mtiririko.

Yaani itapita kadiri watakavyo, ni kiasi cha kutaka tu. Aya kadhaa zimekwishapita zinazosifia aliyowaandalia Mwenyezi Mungu waja wake wenye takua, na kwamba wao watastarehe humo starehe ambazo hakuna jicho lililowahi kuona wala siko lilowahi kusikia au kuwaziwa na moyo wa mtu. Na wakosefu nao wataadhibiwa kwa namna isiyosemeka wala kuwazika.

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا {7}

Wanatimiza nadhiri, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea.

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا {8}

Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na mateka.

إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّهِ لَا نُرِيدُ مِنْكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا {9}

Hakika tunawalisha kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu tu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.

إِنَّا نَخَافُ مِنْ رَبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا {10}

Hakika tunaogopa kutoka kwa Mola wetu siku ya kukunja uso yenye giza kali.

فَوَقَاهُمُ اللَّهُ شَرَّ ذَٰلِكَ الْيَوْمِ وَلَقَّاهُمْ نَضْرَةً وَسُرُورًا {11}

Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha.

وَجَزَاهُمْ بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا {12}

Na atawalipa Bustani za hariri kwa vile walivyosubiri.

مُتَّكِئِينَ فِيهَا عَلَى الْأَرَائِكِ ۖ لَا يَرَوْنَ فِيهَا شَمْسًا وَلَا زَمْهَرِيرًا {13}

Humo wataegemea juu makochi, hawataona humo jua kali wala baridi kali.

وَدَانِيَةً عَلَيْهِمْ ظِلَالُهَا وَذُلِّلَتْ قُطُوفُهَا تَذْلِيلًا {14}

Na vivuli vyake vitanawiri juu yao, na mashada ya matunda yake yataning’inia chini chini.

وَيُطَافُ عَلَيْهِمْ بِآنِيَةٍ مِنْ فِضَّةٍ وَأَكْوَابٍ كَانَتْ قَوَارِيرَا {15}

Na watapitishiwa vyombo vya fedha na bilauri za kioo.

قَوَارِيرَ مِنْ فِضَّةٍ قَدَّرُوهَا تَقْدِيرًا {16}

Kioo kinachotokana na fedha, wamezikadiria kwa vipimo.

وَيُسْقَوْنَ فِيهَا كَأْسًا كَانَ مِزَاجُهَا زَنْجَبِيلًا {17}

Na humo watanyweshwa kikombe kilichochanganyika na tangawizi.

عَيْنًا فِيهَا تُسَمَّىٰ سَلْسَبِيلًا {18}

Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil.

وَيَطُوفُ عَلَيْهِمْ وِلْدَانٌ مُخَلَّدُونَ إِذَا رَأَيْتَهُمْ حَسِبْتَهُمْ لُؤْلُؤًا مَنْثُورًا {19}

Na watawazungukia wavulana wasiochakaa, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizotawanywa.

وَإِذَا رَأَيْتَ ثَمَّ رَأَيْتَ نَعِيمًا وَمُلْكًا كَبِيرًا {20}

Na utakapoyaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa.

عَالِيَهُمْ ثِيَابُ سُنْدُسٍ خُضْرٌ وَإِسْتَبْرَقٌ ۖ وَحُلُّوا أَسَاوِرَ مِنْ فِضَّةٍ وَسَقَاهُمْ رَبُّهُمْ شَرَابًا طَهُورًا {21}

Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao atawanywesha kinywaji safi.

إِنَّ هَٰذَا كَانَ لَكُمْ جَزَاءً وَكَانَ سَعْيُكُمْ مَشْكُورًا {22}

Hakika haya ni malipo yenu; na mahangaiko yenu yameshukuriwa.

Aya 7 – 22: Huwalisha Chakula Juu Ya Kukipenda Kwake

Maana

Baada ya kuashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baadhi ya yale aliyowaan­dalia watu wema kesho, hapa anasema wanastahiki hayo kutokana na sifa tatu:

1. Wanatimiza nadhiri.

Nadhiri kilugha ni ahadi, na kisharia ni kujilazimishaa mtu, aliyebaleghe na kuwa na akili timamu, kufanya jambo au kuliacha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; kutenda au kuacha kuwe kunamridhisha Mwenyezi Mungu; vinginevyo itakuwa sio nadhiri, kama wanavyosema wahakiki.

Tamko la nadhiri ni kusema mwenye kuweka nadhiri: Nimejilazimisha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, au nimeweka nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Haiwezi kuwa nadhiri ikiwa hakuna mojawapo ya majina ya Mwenyezi Mungu; kama vile Mwingi wa rehema, Muumba, Muhuyishaji, Mfishaji n.k. Lau atasema: nimeweka nadhiri kuwa nitafanya jambo kadhaa, basi itakuwa ni mchezo.

Ahadi katika istilahi ya wanafiqh wengi, ni kusema yule mwenye kuweka ahadi: Ninamuahidi Mwenyezi Mungu, au nimejilazimisha kumwahidi Mwenyezi Mungu jambo fulani. Yamini ni kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu (kiapo). Yametangulia maelezo kuhusu Viapo katika Juz. 7 (5:59). Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anapenda na anamlipa thawabu kila mwenye kusadikisha na kufanya vizuri katika kitendo au kauli; ni sawa iwe ni kauli, ahadi, nad­hiri, kiapo, ushahidi au habari yoyote.

2. Na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea.

Wanamtii Mwenyezi Mungu katika kila kitu kuhofia siku ambayo shari yake inaenea kwa kila mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na akamhali­fu katika hukumu miongoni mwa hukumu zake.

3. Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yati­ma, na mateka.

Wanajitolea kila kizuri tena wakiwa wanakihitajia sana; mfano wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu:

 وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ {9}

“Na wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji.” Juz. 28 (59:9).

Mateka hapa, imesemekana ni mateka aliyetekwa na waislamu katika vita na maadui wa Mwenyezi Mungu na wa Uislamu. Imepokewa riwaya kuwa maswahaba walikuwa wakimpeleka mtu waliyemteka, basi mtume humk­abidhi kwa mmoja wa waislamu na kumwambia kaa naye vizuri. Akimchukua nyumbani kwake na kumtunza kuliko yeye mwenyewe na familia yake.

Hakika tunawalisha kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu tu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani. Hakika tunaogopa kutoka kwa Mola wetu siku ya kukunja uso yenye giza kali.

Hatutaki malipo kutoka kwenu wala kwa mwingine; isipokuwa tunawal­isha na kujitolea kwa msukumo wa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kuhofia siku ya kuchunguzwa matendo na yenye vituko vingi. Waliyasema haya kwa lugha ya maneno na ya matendo au amewasemea Mwenyezi Mungu kwa kujua imani na ikhlasi iliyo nyoyoni mwao.

Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawaku­tanisha na raha na furaha.

Walihofia siku ya mkusanyiko wakapata kinga ya shari yake kwa kumtii Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhlasi, wakabadilishiwa hofu yao kuwa amani, nyuso zao zikaangaza nuru ya furaha.

Na atawalipa Bustani za hariri kwa vile walivyosubiri.

Walivumilia njaa ili wamshibishe mwingine, malipo yao yamekuwa Bustani iliyo na kila kinachotamaniwa na nafsi na kuburudika na macho. Katika tafsiri nyingi imeelezwa kuwa Aya hizi zilimshukia Imam Ali bin Abi Twalib; miongoni mwazo ni ibara ya Ar -Razi, ninamnuku: “Ametaja Al-Wahidi, katika watu wetu ‧ yaani Sunni ‧ na mwenye Al­kashaf katika Mu’tazila, kwamba Hasan na Husein (a.s.) walikuwa wag­onjwa, Mtume (s.a.w.) na watu wengine wakaenda kuwaamkia, wakasema: “Ewe Abul-Hasan, unaonaje lau utaweka nadhiri kwa ajili ya wanao. Basi akaweka nadhiri Ali, Fatima na Mtumishi wao Fidha, kufunga siku tatu ikiwa watapona.

Basi wakapona. Ali akakopa pishi tatu za shairi. Fatima akasaga pishi moja na kutengeneza mikate mitano kulingana na idadi yao. Wakaiweka ili wafuturu, akaja muombaji, akasema: As-salamu alaykum, enyi watu wa nyumba ya Muhammad! Maskini jamani, nilisheni atawal­isha Mwenyezi Mungu Peponi. Basi wakampa bila ya kuonja kitu isipokuwa maji, wakaamkia saumu.

Ilipofika jioni na kuleta chakula aliwasimamia yatima wakampa. Akaja mateka usiku wa tatu, wakafanya hivyo hivyo. Ilipofika asubuhi Mtume wa Mwenyezi Mungu akawaona wanatetemeka kama vifaranga, akasema: “Ni huzuni kubwa iliyoje kuwaona katika hali hii! Jibril akashuka na kusema: “Chukua ewe Muhammad! Mwenyezi Mungu anakupongeza kwa watu wa nyumba yako, soma Sura hii.”

Humo wataegemea juu makochi, hawataona humo jua kali wala bari­di kali.

Humo ni humo Peponi. Jua kali ni kinaya cha joto. Maana yako wazi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (18:31).

Na vivuli vyake vitanawiri juu yao, na mashada ya matunda yake yataning’inia chini chini.

Neno kunawiri tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu daniU ambalo lina maana ya kuwa karibu, kama walivyofasiri hivyo wafasiri wengi. Lakini pia lina maana hiyo tuliyoitumia. Tumetumia maana hiyo kwa vile inaen­dana na kivuli, pia inaendana na herufi alayhim, (jua yao); kama inge­likuwa na maana ya karibu ingelitumika herufi ilayihim. Kuwa chini matunda maana yake ni kuweza kuchumwa bila ya kizuizi chochote. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo (69:23)

Na watapitishiwa vyombo vya fedha na bilauri za kioo; kioo kina­chotokana na fedha, wamezikadiria kwa vipimo.

Ni watu wa Peponi hao, na ndio watakaokadiria. Maana ni kuwa rangi na ukubwa wa vikumbe utakua vile wanavyotaka watu wa Peponi, vile watakavyokadiria kwenye nafsi zao na kuleta picha kwenye akili zao. Wafasiri wameleta swali kuhusu Aya hii, kwamba chombo cha kioo kinawezaje kuwa cha fedha, je, ni sawa kusema kioo kinatokana na fedha na maji yanatokana na udongo? Wamejibu kuwa madini ya bilauri yametokana na fedha, lakini ni nyem­bamba zinaonesha kama kioo.1
Na humo watanyweshwa kikombe kilichochanganyika na tangawizi.

Wafasiri wanasema kuwa waarabu walikuwa wakipenda kuweka tangaw­izi kwenye vinywaji, ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akakisifia kinywaji cha Peponi kwayo.

Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil ambayo ni tamu mno, kinywaji chake kinashuka vizuri, Na watawazungukia kuwatumikia wavulana wasiochakaa, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizotawanywa.

Wao ni kama lulu kwa uzuri wao na kunyinyirika kwao. Waliotawanywa ni ishara ya wingi wao na kuweko huku na huko.

Na utakapoyaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa.

Ukiingia Peponi utaona ambayo hayajaonekana wala kusikiwa na kuwazi­wa.

Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao atawanywesha kinywaji safi kabisa.

Watavaa Hariri nyembamba na nzito, vile vile mikononi mwao mtakuwa na bangili na watakunywa kinywaji safi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (18:31). Hakika haya ni malipo yenu; na mahangaiko yenu yameshukuriwa. Baada ya takrima yote hiyo wataaambiwa huu ndio mshahara wenu wa matendo yenu mliyoyafanyia juhudi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:19).

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ تَنْزِيلًا {23}

Hakika Sisi tumekuteremshia Qur’an kidogo kidogo.

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تُطِعْ مِنْهُمْ آثِمًا أَوْ كَفُورًا {24}

Basi subiri hukumu ya Mola wako wala usimtii miongoni mwao mwenye dhambi au
mwenye kufuru.

وَاذْكُرِ اسْمَ رَبِّكَ بُكْرَةً وَأَصِيلًا {25}

Na lidhukuru jina la Mola wako asubuhi na jioni.

وَمِنَ اللَّيْلِ فَاسْجُدْ لَهُ وَسَبِّحْهُ لَيْلًا طَوِيلًا {26}

Na usiku msujudie Yeye, na umsabihi usiku mrefu.

إِنَّ هَٰؤُلَاءِ يُحِبُّونَ الْعَاجِلَةَ وَيَذَرُونَ وَرَاءَهُمْ يَوْمًا ثَقِيلًا {27}

Kwa hakika watu hawa wanapenda ya sasa, na wana­iacha nyuma yao siku nzito.

نَحْنُ خَلَقْنَاهُمْ وَشَدَدْنَا أَسْرَهُمْ ۖ وَإِذَا شِئْنَا بَدَّلْنَا أَمْثَالَهُمْ تَبْدِيلًا {28}

Sisi tumewaumba, na tukavi­imarisha viungo vyao. Na tuk­itaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao.

إِنَّ هَٰذِهِ تَذْكِرَةٌ ۖ فَمَنْ شَاءَ اتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِ سَبِيلًا {29}

Hakika haya ni mawaidha; basi anayetaka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake.

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَنْ يَشَاءَ اللَّهُ ۚ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا {30}

Wala hamuwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hiki­ma.

يُدْخِلُ مَنْ يَشَاءُ فِي رَحْمَتِهِ ۚ وَالظَّالِمِينَ أَعَدَّ لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا {31}

Humuingiza amtakaye katika rehema yake. Na wenye kud­hulumu amewawekea adhabu
iliyo chungu.

Aya 23 – 31: Wanapenda Ya Sasa

Maana

Hakika Sisi tumekuteremshia - ewe Muhammad (s.a.w.) -Qur’an kido­go kidogo.

Ni haki isiyokuwa na shaka na tumekuahidi kukunusuru, kwa sharti la kuvumila maudhi kutoka kwa wenye inadi na upinzani.

Basi subiri hukumu ya Mola wako.

Hukumu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kupita mambo kwa desturi yake ya maumbile na kupatikana kwa wakati wake maalum. Njia ya uon­gofu kwa mwenye kuipendelea ni nasaha na uongofu, na njia ya nusra ni kuwa na subira katika jihadi.

Wala usimtii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru,

katika yale wanayokuzuwia nayo na wanayokuvutia nayo. Washirikina walimwekea mtume mali, wanawake na uongozi ili aache mwito wake wa kumlingania Mwenyezi Mungu, akawa anakataa. Hilo linaashiriwa na kukatazwa kumtii mwenye dhambi na mwenye kufuru. Makusudio ya mwenye kufuru ni kila mpinzani.

Kundi la wafasiri wamesema kuwa makusudio ya mwenye dhambi hapa ni Utba bin Rabia, kwa sababu alikuwa amezama kwenye starehe, mwenye kufuru ni Abu Jahl au Walid bin Mughira. Vyovyote iwavyo sababu ya kushuka, lakini haihusishi tamko.

Na lidhukuru jina la Mola wako asubuhi na jioni.

Yaani kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu katika mambo yako yote na wakati wako wote wala usiogope lawama. Umetangulia mfano wake kati­ka Juz. 23 (33:42).

Na usiku msujudie Yeye, na umsabihi usiku mrefu.

Fanya tahajudi usiku muda kiasi. Amri hii ni ya Sunna sio ya wajib kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَكَ {79}

“Na katika usiku amka kwayo, ni ziada kwa ajili yako.” Juz. 15 (17:79).

Kwa hakika watu hawa wanapenda ya sasa, na wanaiacha nyuma yao siku nzito.

Hawa ni ishara ya washirikina na kila mwenye kuipenda dunia, ikamtawala na kuichukia akhera na kuifanyia uadui. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameita siku nzito kwa vile itakuwa ngumu kwa makafiri.

Sisi tumewaumba, na tukaviimarisha viungo vyao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye aliyewaleta kutoka kutokuwepo, akawatia sura na kuzifanya nzuri sura zao, vipi wanamkana na kuasi amri zake na makatazo yake?

Na tukitaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao.

Huu ni ukemeo kwa wale wanokadhibisha kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuwangamiza na kuwaleta watu wengine bora kuliko wao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 26 (47:38) .

Hakika haya ni mawaidha.

Haya ni haya yaliyo katika Sura hii tuliyo nayo, ndani yake mkiwa na maonyo na mapendekezo, yakiwa ni mawaidha kwa mwenye moyo au akatega sikio naye ni shahidi.

Basi anayetaka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake; wala hamuwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebainisha njia mbili ya kheri na shari. Akakataza hii na akaamrisha ile, akamwacha mtu ajichagulie mwenyewe, lakini mwenye inadi hawezi kufanya heri ila akifanyishwa kwa nguvu na Mwenyezi Mungu, na hili haliwezi kuwa kwa sababu litakwenda kinyume na uadilifu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu, hikima yake na desturi yake kwa viumbe wake. Tazama Juzuu hii tuliyo nayo (74:56), tumefafanua zaidi huko.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hikima.

Mwenye kujua hali za waja wake, ana hikima kwa sababu hatoi amri ila kwa lenye heri na masilahi, wala hakatazi ila lenye shari na ufisadi.

Humuingiza amtakaye katika rehema yake.

Makusudio ya rehema hapa ni Pepo na matakwa yake ni kuwa hamwingizi Peponi yoyote yule ila kwa juhudi na kuifanyia kazi; hivyo ndivyo anavy­otaka.

Aya zinazofahamisha hivyo ziko nyingi na wazi; miongoni mwazo ni: “Je, mwadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira? Juz. 4 (3:142). Vipi atataka Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumwingiza Peponi asiyestahiki na hali alimtoa humo Adam alipoasi.

Na wenye kudhulumu amewawekea adhabu iliyo chungu.

Wenye takua watapata rehema ya Mwenyezi Mungu na wakosefu watapa­ta ghadhabu na adhabu yake.

  • 1. Mimi ningeifasiri kwa namna ambayo haitaleta swali: “Na bilauri za kauri,” kwa kufasiri qawarirU kwa maana ya madini ya kauri, ambayo ni udongo mweupe mwepesi unaong’aa na unaotengenezewa vyombo; kwa kudhani kuwa waswahili wamelichukua neno kauri kutoka neno hilo la kiarabu qarura. ‧Mtarjumi.