read

Aya 52 – 55: Watapewa Ujira Mara Mbili

Maana

Wale ambao tuliwapa Kitabu kabla yake wanaiamini.

Yaani waliopewa Kitabu kabla ya Qur’an wanaiamini hii Qur’an. Zimethibiti Hadith Mutawatir kwamba wanaswara (wakiristo) wengi na baadhi ya mayahudi walimwamini Muhammad (s.a.w.), kwa sababu Tawrat na Injili zimenukuu wasifu wake, kabla hazijapotolewa:

الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِنْدَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنْجِيلِ{157}

“Ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injili” Juz. 9 (7:157)

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:121) na Juz. 4 (3:199).

Na wanaposomewa, husema: Tunaiamini. Hakika hiyo ni haki inayotoka kwa Mola wetu. Hakika sisi kabla yake tulikuwa waislamu (wanyenyekevu).

Maulama wa watu wa Kitabu walisoma sifa za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na Qur’an Tukufu katika Tawrat na injil. Walizisoma hizo kabla ya kutumilizwa Muhammad (s.a.w.). Alipotumilizwa aliwasomea Qur’an wakaitambua na wakamtambua Muhammad kwa sifa zake, kama zilivyo katika vitabu viwili; sawa na walivyowajua watoto wao:

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ ۖ {146}

Wale tuliowapa Kitabu wanamjua kama wanavyowajua watoto wao.” Juz.1 (2:146).

Basi baadhi wakaamini na wengine wakaficha haki na hali wanajua, kwa kupupia vyeo na chumo.

Basi hao watapewa ujira wao mara mbili.

Wa kwanza ni kwa sababu ya ikhlasi yao katika dini yao ambayo imewaamrisha kumfuata Muhammad na Qur’an, na wa pili ni kwa walivyovumilia adha ya makafiri wapumbavu, kwa sababu kusilimu kwao kulikuwa ni hoja kubwa kwa yule anayeng’ang’ania ukafiri kwa inadi.

Subira Ni Hekima Na Ushujaa

Na wanaondoa ubaya kwa wema.

Waislamu wa mwanzo walipambana na maudhi na mateso, kiasi ambacho Muhammad (s.a.w.) alikuwa akizomewa na wapumbavu barabarani: “Huyoo mwenda wazimu... Huyoo mwongo... Huyoo mchawi!”

Wakawa na subira wakavumilia bila ya kulalamika. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameiita subira yao wema na maudhi ya washirikina akayaita ubaya.

Katika ibara hii kuna ishara kuwa silaha pekee ya mnyonge ni subira na kwamba hasira na kusimamisha mishipa ni wenda wazimu na kupigana bila ya silaha ni kujitia kitanzi.

Kwa hiyo subira ya mnyonge ni akili na hekima na ni ushujaa na werevu; kwa sharti ya kuhangaika na kufanya juhudi ya kuondoa huo unyonge na visababishi vyake. Lakini atakayebweteka na kufanya uvivu atakuwa amejitweza mwenyewe na kuridhia udhalili na unyonge.

Kwa maneno mengine ni kuwa unyonge ni kama ugonjwa, ni lazima utafutiwe dawa ya kuuondoa, sio kuvumilia kubaki na ugonjwa isipokuwa baada ya kushindwa kabisa na kukata tamaa.

Na wakatoa katika tuliyowaruzuku.

Wanaondoa shari ya uovu kwa kuvumilia. Pia wanafanya wema kwa kutoa kile wanachoruzukiwa na Mwenyezi Mungu kwa fadhila zake. Imam Ali (a.s.) anasema: Muadhibu ndugu yako kwa kumfanyia wema na urudishe uovu wake kwa kumneemesha.

Na wanaposikia upuuzi hujitenga nao.

Makafiri walianzisha matusi na shutuma kwa wale waliosilimu na kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wakavumilia na kujitia hamnazo, na husema: Sisi tuna vitendo vyete na nyinyi mna vitendo vyenu. Nyinyi mmeridhia batili mliyo nayo na sisi tumeridhia haki tuliyo nayo.

Salamun alaykum!

Wafasiri wamesema: Salamu hii ni ya kuwavumilia majahili sio ya maamkuzi; sawa na kumwambia unayetaka uepukane naye: “Niondokee kwa amani.

Hatuwataki wajinga.

Hatuchanganyiki nao wala hatuwi na hulka zao.

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ يَهْدِي مَنْ يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ {56}

Kwa hakika wewe humuongoi umtakaye, lakini Mwenyezi Mungu humuongoa amtakaye naye ndiye anayewajua zaidi waongokao.

وَقَالُوا إِنْ نَتَّبِعِ الْهُدَىٰ مَعَكَ نُتَخَطَّفْ مِنْ أَرْضِنَا ۚ أَوَلَمْ نُمَكِّنْ لَهُمْ حَرَمًا آمِنًا يُجْبَىٰ إِلَيْهِ ثَمَرَاتُ كُلِّ شَيْءٍ رِزْقًا مِنْ لَدُنَّا وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ {57}

Na wakasema: Tukifuata muongozo huu pamoja nawe, tutanyakuliwa kutoka nchi yetu. Je, kwani hatukuwaweka imara mahali patakatifu pa amani, panapoletwa matunda ya kila aina kuwa ni riziki itokayo kwetu? Lakini wengi wao hawajui.

وَكَمْ أَهْلَكْنَا مِنْ قَرْيَةٍ بَطِرَتْ مَعِيشَتَهَا ۖ فَتِلْكَ مَسَاكِنُهُمْ لَمْ تُسْكَنْ مِنْ بَعْدِهِمْ إِلَّا قَلِيلًا ۖ وَكُنَّا نَحْنُ الْوَارِثِينَ {58}

Na ni miji mingapi iliyojifaharisha maisha yake tumeiangamiza! Na hayo maskani yao hayakukaliwa tena baada yao ila kwa uchache tu. Na sisi ndio tumekuwa warithi.

وَمَا كَانَ رَبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَىٰ حَتَّىٰ يَبْعَثَ فِي أُمِّهَا رَسُولًا يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا ۚ وَمَا كُنَّا مُهْلِكِي الْقُرَىٰ إِلَّا وَأَهْلُهَا ظَالِمُونَ {59}

Na Mola wako haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika mji wao mkuu awasomee Aya zetu. Wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake wawe madhalimu.

وَمَا أُوتِيتُمْ مِنْ شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَزِينَتُهَا ۚ وَمَا عِنْدَ اللَّهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {60}

Na chochote mlichopewa ni matumizi ya maisha ya dunia na pambo lake. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio bora na yatakayobaki zaidi. Basi je, hamfahamu?

أَفَمَنْ وَعَدْنَاهُ وَعْدًا حَسَنًا فَهُوَ لَاقِيهِ كَمَنْ مَتَّعْنَاهُ مَتَاعَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ثُمَّ هُوَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنَ الْمُحْضَرِينَ {61}

Je yule tuliyemuahidi ahadi nzuri tena naye akaipata, ni kama tuliyemstarehesha kwa starehe za maisha ya duniani na kisha siku ya Kiyama akawa miongoni mwa wanaohudhurishwa?