read

Aya 71 – 75: Hekima Ya Usiku Na Mchana

Maana

Sema: Mwaonaje, kama Mwenyezi Mungu angeliufanya usiku uwakalie moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, mungu gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu atakayewaletea mwangaza basi je, hamsikii.

Binadamu hufanya kazi na kupumzika kwa usingizi. Kazi inahitajia mwangaza na usingizi kwenye giza unakuwa mzito na unaleta siha ya mwili.

Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akaumba mchana kwa ajili ya kufanya kazi na usiku kwa ajili ya kupumzika. Lau usiku ungeliendelea bila ya asubuhi au mchana ukaendelea bila ya usiku basi maisha yangelikuwa balaa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipotaja usiku amesema: ‘Hamsikii?’ na mchana akasema: ‘Hamuoni?’ kwa sababu usiku unanasibiana na kusikia na mchana kwa kuona.

Huko nyuma tumesema kuwa kufuatana usiku na mchana kunategemezwa moja kwa moja kwenye sababu zake za kimaumbile na kunategemezwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kupitia hizo sababu, kwa vile yeye ndiye muumba wa ulimwengu na vilivyomo, na ndiye aliyeupangilia vizuri kwa hekima yake.

Na katika rehema zake amewafanyia usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake na ili mpate kushukuru.

Yaani amewafanyia usiku mpumzike na amewafanyia mchana mtafute. Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:67), Juz. 15 (17:12) na Juz. 19 (25:47).

Na siku atakapowaita na akasema: Wako wapi mliokuwa mkidai kuwa ni washirika wangu.

Imetangulia punde tu katika Sura hii tuliyo nayo Aya 62. hatujui wajihi wa kukaririka huku isipokuwa kuthibitisha na kusisitiza.

Na tutatoa shahidi katika kila umma na tuseme: Leteni hoja zenu!

Kesho Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kila umma atauletea nabii wao atoe ushahidi juu yao kuwa alifikisha ujumbe na aeleze upinzani alioupata na kukadhibishwa baada ya kuwawasilishia hoja na kukata nyudhuru zote. Hapo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atasema Mtume amenieleza yake, haya nanyi elezeni yenu na kile kilichowafanya muwakadhibishe; sawa na hakimu anavyofanya–kwanza anamsikiliza mwenye madai kisha mshatikiwa anajibu.

Hapo wataziba mdomo wabatilifu na adhabu itawastahili. Umetangulia mfano wake katika Juz. 2 (2:143), Juz. 14 (16:89).

Hapo watajua kwamba hakika haki ni ya Mwenyezi Mungu.

Yaani watajua kuwa hoja ya Mungu itawasimamia juu yao na wao hawatakuwa na hoja kwa Mwenyezi Mungu.

Na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyazua, kuwa Mwenyezi Mungu ana mshirika na uwongo walioueneza juu ya watu wema.

إِنَّ قَارُونَ كَانَ مِنْ قَوْمِ مُوسَىٰ فَبَغَىٰ عَلَيْهِمْ ۖ وَآتَيْنَاهُ مِنَ الْكُنُوزِ مَا إِنَّ مَفَاتِحَهُ لَتَنُوءُ بِالْعُصْبَةِ أُولِي الْقُوَّةِ إِذْ قَالَ لَهُ قَوْمُهُ لَا تَفْرَحْ ۖ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْفَرِحِينَ {76}

Hakika Qaruni alikuwa katika kaumu ya Musa, lakini aliwafanyia dhulma. Na tulimpa hazina ambazo funguo zake ziliwaelemea kundi la watu wenye nguvu. walipomwambia watu wake: Usijigambe, hakika Mwenyezi Mungu hapendi wanaojigamba.

وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّهُ الدَّارَ الْآخِرَةَ ۖ وَلَا تَنْسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا ۖ وَأَحْسِنْ كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ ۖ وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الْأَرْضِ ۖ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ {77}

Na utafute kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi ya akhera; wala usisahau fungu lako la dunia. Na fanya wema kama alivyokufanyia wema Mwenyezi Mungu, wala usitafute ufisadi katika ardhi; hakika Mwenyezi Mungu hapendi wafisadi.

قَالَ إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَىٰ عِلْمٍ عِنْدِي ۚ أَوَلَمْ يَعْلَمْ أَنَّ اللَّهَ قَدْ أَهْلَكَ مِنْ قَبْلِهِ مِنَ الْقُرُونِ مَنْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُ قُوَّةً وَأَكْثَرُ جَمْعًا ۚ وَلَا يُسْأَلُ عَنْ ذُنُوبِهِمُ الْمُجْرِمُونَ {78}

Akasema: Kwa hakika nimepewa haya kwa sababu ya elimu niliyo nayo. Je, hakujua kwamba Mwenyezi Mungu amekwishaangamiza karne zilizokuwa kabla yake waliokuwa na nguvu zaidi kuliko yeye na wenye makundi makubwa zaidi. Na wakosefu hawataulizwa dhambi zao.

فَخَرَجَ عَلَىٰ قَوْمِهِ فِي زِينَتِهِ ۖ قَالَ الَّذِينَ يُرِيدُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا يَا لَيْتَ لَنَا مِثْلَ مَا أُوتِيَ قَارُونُ إِنَّهُ لَذُو حَظٍّ عَظِيمٍ {79}

Basi akawatokea watu wake katika pambo lake. Wakasema wale waliokuwa wanataka maisha ya duniani: Laiti tungelikuwa nayo kama aliyopewa Qaruni! Hakika yeye ni mwenye bahati kubwa.

وَقَالَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ وَيْلَكُمْ ثَوَابُ اللَّهِ خَيْرٌ لِمَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا وَلَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الصَّابِرُونَ {80}

Na wakasema wale ambao wamepewa elimu: Ole wenu! Thawabu za Mwenyezi Mungu ni bora kwa mwenye kuamini na akatenda. Na wala hawatapewa isipokuwa wenye subira.

فَخَسَفْنَا بِهِ وَبِدَارِهِ الْأَرْضَ فَمَا كَانَ لَهُ مِنْ فِئَةٍ يَنْصُرُونَهُ مِنْ دُونِ اللَّهِ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُنْتَصِرِينَ {81}

Basi tukamdidimiza yeye na nyumba yake ardhini; wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia kinyume na Mwenyezi Mungu wala hakuwa miongoni mwa wanaojisaidia.

وَأَصْبَحَ الَّذِينَ تَمَنَّوْا مَكَانَهُ بِالْأَمْسِ يَقُولُونَ وَيْكَأَنَّ اللَّهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَنْ يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ ۖ لَوْلَا أَنْ مَنَّ اللَّهُ عَلَيْنَا لَخَسَفَ بِنَا ۖ وَيْكَأَنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ {82}

Na wakawa wanasema wale waliotamani mahala pake jana: Kumbe Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, katika waja wake, na humdhikisha amtakaye. Asingetufanyia hisani Mwenyezi Mungu angelitudidimiza. Kumbe makafiri hawafanikiwi.