read

Aya 100-102: Habari Za Miji

Hizo ni habari za miji tunazokusimulia, mingine bado ipo na mingine imefyekwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja sehemu ya visa katika umma zilizopita pamoja na mitume yao, alimwambia mtume mtukufu (saww) kwamba baadhi ya umma hizo athari zake bado zipo na nyingine athari zake hazipo.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa ambazo athari zake zimebakia ni miji ya Aa’d na Thamud, na zile ambazo hazikubakia athari zake ni miji ya Nuh. Ama sisi tunawachia wataalamu wa mambo ya kale.

Kwa hali yoyote iwayo, ni kuwa ubainifu wa kisa hiki kwa ulimi wa Muhammad (saww) ni dalili mkataa ya utume wake na kwamba ni wahyi wa kutoka kwa Mwenyezi Mungu sio njozi wala nukuu ya yaliyosemekana.

Nasi hatukuwadhulumu, lakini wao wamejidhulumu wenyewe kwa kumkadhibisha kwao mtume wa Mwenyezi Mungu na kung’ang’ania kwao shirki na ufisadi. Maana haya yamekaririka katika Katika Qur’ani kwa karibu Aya ishirini.

Na miungu yao waliyokuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, haikuwafaa kitu ilipofika amri ya Mola wako, na haikuwazidishia isipokuwa maangamizi.

Miungu yao ni masanamu yao. Maana yanaupishwa na kauli yake:

وَيَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ مَا لَا يَنْفَعُهُمْ وَلَا يَضُرُّهُمْ ۗ {55}

“Na wanaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu yasiyowafaa wala kuwadhuru” (25:55)

Na ni kama hivyo kushika kwa Mola wako anapoishika miji inapokuwa imedhulumu.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Atawaangamiza makafiri, madhlimu kama mfano wa tufani, tetemeko na ukelele wa adhabu.

Hakika kushika kwake ni kuchungu, kukali, lakini ni baada ya onyo na hoja kupitia mitume wakionya ana kwa ana.

Tumesema ana kwa ana, kwa sababu hivi sasa ukafiri na ufisadi ni mwingi kuliko hapo zamani, na maonyo yapo, ya kiakili, vitabu vya mbinguni na hadith za Mtume, lakini pamoja na hayo, hakuna matufani wala mitetemeko au mawe ya udongo mkavu.

Hatujui siri ya hilo, isipokuwa kudhani kuwa matakwa ya Mwenyezi Mungu yamehukumia maangamivu ya wale wanaowapinga mitume wao ana kwa ana; na sio wale wanaoasi wahyi na akili. Lakini dhana haitoshelezi kitu haki. Na Mwenyezi ndiye Mjuzi zaidi.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِمَنْ خَافَ عَذَابَ الْآخِرَةِ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمٌ مَجْمُوعٌ لَهُ النَّاسُ وَذَٰلِكَ يَوْمٌ مَشْهُودٌ {103}

Hakika katika hayo kuna Ishara kwa yule anayeogopa adhabu ya Akhera. Hiyo ndiyo siku itakayokusanyiwa watu na hiyo ndiyo siku itakayoshuhudiwa.

وَمَا نُؤَخِّرُهُ إِلَّا لِأَجَلٍ مَعْدُودٍ {104}

Na hatuiakhirishi ila kwa muda unaohisabiwa.

يَوْمَ يَأْتِ لَا تَكَلَّمُ نَفْسٌ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ فَمِنْهُمْ شَقِيٌّ وَسَعِيدٌ {105}

Siku itakapofika, nafsi yoyote haitasema ila kwa kwa idhini yake. Katika wao kuna waovu na wengine ni wema.

فَأَمَّا الَّذِينَ شَقُوا فَفِي النَّارِ لَهُمْ فِيهَا زَفِيرٌ وَشَهِيقٌ {106}

Ama wale waovu watakuwa motoni watachachatika na kukorama.

خَالِدِينَ فِيهَا مَا دَامَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ إِلَّا مَا شَاءَ رَبُّكَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ فَعَّالٌ لِمَا يُرِيدُ {107}

Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa apendavyo Mola wako. Hakika Mola wako hufanya atakavyo.

وَأَمَّا الَّذِينَ سُعِدُوا فَفِي الْجَنَّةِ خَالِدِينَ فِيهَا مَا دَامَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ إِلَّا مَا شَاءَ رَبُّكَ ۖ عَطَاءً غَيْرَ مَجْذُوذٍ {108}

Ama wale wema watakuwa Peponi watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa apendavyo Mola wako. Ni kipawa kisicho na ukomo.

فَلَا تَكُ فِي مِرْيَةٍ مِمَّا يَعْبُدُ هَٰؤُلَاءِ ۚ مَا يَعْبُدُونَ إِلَّا كَمَا يَعْبُدُ آبَاؤُهُمْ مِنْ قَبْلُ ۚ وَإِنَّا لَمُوَفُّوهُمْ نَصِيبَهُمْ غَيْرَ مَنْقُوصٍ {109}

Basi usiwe na shaka na wanayo yaabudu hao. Hawaabudu ila kama walivyoabudu baba zao zamani. Na hakika sisi tutawatimizia fungu lao bila ya kupunguzwa.