read

Aya 103 – 109: Siku Itakayoshuhudiwa

Maana

Hakika katika hayo kuna ishara kwa yule anayeogopa adhabu ya Akhera. Hiyo ndiyo siku itakayokusanyiwa watu na hiyo ndiyo siku itakayoshuhudiwa.

Hayo ni ishara ya kuadhibu kwake Mwenyezi Mungu vijiji. Yaani katika kuadhibu huku kuna mazingatio kwa mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na ni waadhi kwa anayeogopa adhabu ya siku watakayoishuhudia viumbe wote, pale atakapowakusanya kwa ajili ya hisabu na malipo.

Unaweza kuuliza kuwa tufani au tetemeko na mfano wake mara nyingi huzuka kwa sababu za kimaumbile na maumbile hayawezi kumpambanua mwema na muovu. Je, haiwezekani kuwa yaliyowatokea kaumu za mitume ni aina hii?

Jibu, Mtume alikuwa akiwaonya watu wake kwa kuzuka adhabu na kuieleza aina ya adhabu yenyewe na wakati wa kutokea kwake.

Nayo hutokea kama ilivyoelezwa. Kwa hiyo haiwezekani kuipa tafsiri ya ugunduzi wa kielimu, kwani wakati huo hakukuwa na nyenzo zozote za kielimu, wala hatuwezi kuitafsiri kua ni kawaida ya maumbile, kwa sababu Mtume alikuwa akielezea kwa kujiamini; akisema huu ndio uhakika na mtaona.
Kama ambavyo pia haiwezekani tafsiri ya sadfa kutokana na kukaririka. Ikiwa tafsiri zote hizi haziwezekani, basi inabaki tafsiri ya wahyi na matakwa ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Na hatuiakhirishi ila kwa muda unaohisabiwa.

Kila kitu mbele ya Mwenyezi Mungu kina muda wake, hautangulii wala kuchelewa. Miongoni mwavyo ni kuisha dunia na kuja Akhera.

Siku itakapofika, nafsi yoyote haitasema ila kwa kwa idhini yake.

Itapewa idhini ya kujitetea kama ilivyo katika mahakama za kidunia.

Katika wao kuna waovu na wengine ni wema.

Uovu wa mtu au wema wake kesho utakuwa kwa matendo yake tu hapa duniani.

Ile kauli ya “Muovu ni muovu tangu tumboni mwa mama yake na mwema ni mwema tangu tumboni mwa mama yake,” inatiliwa mashaka. Kwa sababu dhahiri yake inapingana na uadilifu wake Mwenyezi Mungu na rehema yake; mbali ya kuwa ni hadith Ahaad ambayo ni hoja katika hukumu za kisharia tu; kama halali, haramu, twahara na najisi; sio katika misingi ya itikadi na yanayoambatana nayo.

Kisha akawaelezea wale watakaokuwa waovu kwa kusema:

Ama wale waovu watakuwa motoni watachachatika na kukoroma.

Kimsingi ni kuwa Mwenyezi Mungu humwadhibu mfisadi. Kwa hiyo basi uovu anauchumma mwenyewe mtu; sio kwa kadha na kadari.

kuchachatika na kukoroma ni kuelezea uchungu wa watu wa motoni.

Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa apendavyo Mola wako.

Wafasiri wamerefusha maneneno sana kuhusu makusudio ya ‘apendavyo Mwenyezi Mungu,’ hapa. Wakataja njia zilizofanya Aya iwe yenye kutatiza na yenyewe siyo ya kutatiza, bali iko wazi.

Kwa ufupi ni kuwa mwenye kuingia Jahannam kwa dhambi yoyote ile, hataweza kutoka humo yeye mwenyewe, si kwa kuombewa wala kwa fidia. Kwa namna hiyo ndiyo inasemwa ni mwenye kudumu. Lakini Mungu akitaka atoke humo atatoka na ataondokewa na wasifa wa kudumu motoni. Kwa sababu matakwa ya Mwenyzi Mungu, hayazuiwi na kitu chochote.

Hakika Mola wako hufanya atakavyo.

Na kila kitu mwisho wake unarejea kwenye matakwa yake wala matakwa yake hayarejei isipokuwa kwake. Kwa hiyo sababu ya kudumu itafanyakazi madamu muumbaji anataka hivyo na asipotaka basi haiwi.

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَنْ يَقُولَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ {82}

“Hakika amri yake anapotaka chochote ni kukiambia: Kuwa, kikawa” (36:82)

Kama alivyowaelezea walio mashakani kuwa watadumu motoni, vile vile amewaeelezea wenye furaha kuwa ni wenye kudumu Peponi.

Ama wale wema watakuwa Peponi watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa apendavyo Mola wako. Ni kipawa kisicho na ukomo.

Yaani hakikatiki. Unaweza kuuliza kwamba mwenye kuingia pepeoni hatoki, sasa kuna haja gani ya kukuwekea matakwa ya Mwnyezi Mungu?
Imesemekana kuwa Mwenyezi Mungu atawatoa kutoka pepo moja hadi nyingine mfano wake au nzuri zaidi. Tuonavyo sisi ni kuwa hilo ni kiasi cha kuashiria uweza wa Mwenyezi Mungu na ukuu wake, na kwamba sababu zinafanya kazi ikiwa hazikugongana na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo moto utaunguza ikiwa mwenyezi Mungu hakuuambia kuwa baridi na salama.

Basi usiwe na shaka na wanayoyaabudu hao.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (saww). Na hao ni ishara ya watu wake waliomkadhibisha. Muhammad hakuwa wala hatakuwa na shaka kwamba wao wako kwenye ubatilifu katika ibada yao, lakini lengo ni kuwatahayariza na kuwahadharisha.

Hawaabudu ila kama walivyoabudu baba zao zamani.

Hii ni sababu ya yakini ya kutokuwepo shaka katika kubatilika wanayoaabudu hawa. Kwa sababu ni mfano wa walivyoabudu wa kwanza ambao walipatwa na adhabu kwa sababu ya shirki yao na kuabudu kwao masanamu.

Na hakika sisi tutawatimizia fungu lao bila ya kupunguzwa.

Sawa na tulivyotimiza fungu la adhabu waliyostahaiki mababa zao bila ya kupunguza kitu. Unaweza kuuliza: Huku sikukatisha tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu amesema:

يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِنْ رَحْمَةِ اللَّهِ ۚ {53}

“Enyi waja wangu waliojidhulumu msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu” (39:53).

Jibu: Hakika makusudio ya kauli yake, Msikate tamaa ni kuhimiza katika toba na kwamba mwenye kutubia Mwenyezi Mungu humtakabalia toba yake.

Na makusudio ya bila kupunguzwa ni kwamaba mwenye kung’ang’ania shirki na wala asitubie, Mungu atamlipa anavyostahiki.

Sisi hatuna shaka kwamba Mwenyezi Mungu anasamehe na kumhurumia anayewahurumia watu, na anayefanya kwa maslahi ya watu. Ama wale wanaoingilia uhuru na ahaki zao, hawatapunguziwa adhabu wala hawatasaidiwa.

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَاخْتُلِفَ فِيهِ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِنْ رَبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۚ وَإِنَّهُمْ لَفِي شَكٍّ مِنْهُ مُرِيبٍ {110}

Na hakika tulimpa Musa Kitabu, zikazuka khitilafu ndani yake. Na lau kama si neno lililokwisha tangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka ingelihukumiwa baina yao. Na hakika wao wamo katika shaka inayowahangaisha.

وَإِنَّ كُلًّا لَمَّا لَيُوَفِّيَنَّهُمْ رَبُّكَ أَعْمَالَهُمْ ۚ إِنَّهُ بِمَا يَعْمَلُونَ خَبِيرٌ {111}

Na hakika Mola wako atawatimizia malipo ya vitendo vyao. Hakika yeye ana khabari za wanayoyatenda.

فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَنْ تَابَ مَعَكَ وَلَا تَطْغَوْا ۚ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {112}

Basi simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa wewe na yule anayeelekea (kwa Mwenyezi Mungu) pamoja nawe wala msipetuke mipaka. Hakika yeye anayaona mnayoyafanya.

وَلَا تَرْكَنُوا إِلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا فَتَمَسَّكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ ثُمَّ لَا تُنْصَرُونَ {113}

Wala msiwategemee madhalimu, usije ukawagusa moto. Na hamna walinzi asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala hamtasaidiwa.

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ {114}

Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Hiyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.

وَاصْبِرْ فَإِنَّ اللَّهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ {115}

Na subiri, kwani hakika Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanaofanya wema.