read

Aya 110- 115: Neno Lililokwishatangulia.

Na hakika tulimpa Musa Kitabu, zikazuka khitilafu ndani yake.

Makusudio ya Kitabu hapa ni Tawrat. Kaumu ya Musa ilikhitalifiana kuhusiana na Tawrat, wengine waliiamini na wengine wakaikataa. Ndio ilivyo kwa umma wowote, wa zamani na wa sasa, hauafikiani kuhusu mtume wake au kiongozi wake aliyemwaminifu.

Bali wana wa israil waliwaua mitume wao. Hata wale waliomwamini Musa waliigeuza Tawrat baada yake, wakazusha mambo ya upotevu. Kwa hiyo siajabu kwako ewe Muhammad wakikuamini baadhi na wengine wakikukana.

Na lau kama si neno lililokwisha tangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka ingelihukumiwa baina yao.

Makusudio ya neno ni kupitisha kuakhirisha adhabu. Baina yao ni wale waliokhitalifiana katika Tawrat. Hekima yake ilitaka wasipate adhabu hapa duniani.

Na hakika wao wamo katika shaka inayowahangaisha.

Bado maneno yako kwa Musa(a.s.), kaumu na Kitabu chake. Amekuwa mbali yule anayesema kuwa hapa maneno yametoka kwa wana wa Israil hadi kwa Muhammad (saww) na Maquraishi.

Kwa ujumla ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameakhirisha adhabu ya waliokadhibisha Tawrat katika kaumu ya Musa, na waliokadhibisha Qur’ani katika kaumu ya Muhammad.

Na hakika Mola wako atawatimizia malipo ya vitendo vyao. Hakika Yeye ana khabari za wanayoyatenda.

Yaani kila muongo na mkweli atapata malipo ya matendo yake kesho yakiwa kamili. Ikiwa ni kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi ni shari.

Msimamo

Basi simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa wewe na yule anayeelekea (kwa Mwenyezi Mungu) pamoja nawe wala msipetuke mipaka. Hakika yeye anayaona mnayoyafanya.

Maana ya kusimama sawa sawa (msimamo) inatofautiana kulingana na inavyonasibiana. Kwa hiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ {56}

“Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka” (11:56),

ni kuwa Yeye anaongoza kwenye njia hiyo na kuamuru ifuatwe na kwenye msingi wake analipa thawabu na adhabu na kwamba vitendo vyake vyote vinaenda na hekima na maslahi.

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا{115}

Je, mlidhani kwamba tuliwaumba bure bure…?” (23:115)

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ۚ ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ {27}

“Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake bure; hiyo ni dhana ya wale waliokufuru.” (38:27).

Na kama ukisifu kusimama sawa kwenye kitu na ukasema kitu hiki kiko sawasawa maana yake umekiweka mahali panapolingana nacho. Ama mtu aliye sawasawa (msimamo) maelezo yake mazuri ni yale aliyoyasema Mwenyezi Mungu:

الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ ۚ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّهُ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ {18}

“Ambao husikiliza kauli wakafuata zilizo nzuri zaidi. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza na hao ndio wenye akili” (39:18).

Kauli nzuri zaidi kwa Mungu na mwenye kumwamini ni hii Qur’ani:

اللَّهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ الْحَدِيثِ كِتَابًا مُتَشَابِهًا {23}

“Mwenyezi Mungu ameteremsha hadith nzuri kabisa, Kitabu chenye maneno yenye kufanana.” (39:23).

Na kauli nzuri zaidi kwa Mungu na kwa watu wote ni ile inayozipa raha nyoyo za walimwengu sio wezi na wamwaga damu.

Kuna Hadith ya Mtume (s.a.w.) inayosema: “Sura ya Hud imenizeesha” Inasemekana kuwa alikusudia Aya hii ya Sura ya Hud. Kwa sababu umma wake umeamrishwa kusimama sawa (msimamo) naye hana mategemeo kama watauitikia.

Na sisi tunaona sio mbali kuwa makusudio ya umma ni viongozi wake kwa sababu hao ndio asili ya ugonjwa na chimbuko la balaa. Tumezungumza msimamo katika maelezo ya Bismillah kwenye Juzuu ya kwanza. Itikadi ya Uislamu, sharia yake na maadili yake inakuwa katika neno moja ‘Unyoofu’ (msimamo).

Majukumu Ya Mshikamano Dhidi Ya Dhulma

Wala msiwategemee madhalimu, usije ukawagusa moto. Na hamna walinzi asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala hamtasaidiwa.

Dhulma haihusiki na wanaowafanyia uadui watu na uhuru wao tu, Imeelezwa katika Hadith na Nahju-lbalagha “Dhulma ni tatu: Dhulma isiyosamehewa, dhulma isiyoachwa na dhulma inayosamehewa.

Dhlma isiyosamehewa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu (ushirikina), Dhulma inayosamehewa ni kujidhulumu mja yeye mwenyewe kwa kufanya madhambi madogo; na dhulma isiyoachwa ni ya kudhulumiana waja wenyewe kwa wenyewe.”

Makusudio ya kutegemea madhalimu ni pamoja na kuwanyamazia kwa sababu ni wajibu kukataza maovu. Kuna Hadith isemayo: “Watu wakiona maovu na wasiyakanye, basi wanakurubia nao kuchanganywa kwenye adhabu. Imam Ja’far As-swadiq (a.s.) anasema: “Muumin kumsaidia mumin mwengine ni faradhi ya wajib.” Katika Kitabu Wasail katika mlango Aljihadi anil-masum Imeelezwa: “Mwislamu anapigana kwa ajili ya Uislam au kuhofia miji ya waislamu.”

Kwa kutegemea Hadith hizo na nyenginezo, mafaqih wamegawanya jihadi kwenye aina mbili:
1. Jihadi ya kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuueneza Uislam.

2. Kuulinda Uislamu na miji ya Waislamu, bali ni kuitetea haki yoyote ni sawa iwe yake au ya mtu mwengine.

Mwenye Al-Jawahir amesema: “Akishambulia adui, anayehofiwa, himaya ya waislamu au kafiri akitaka kuteka miji ya waislamu, kuwachukua mateka na kupora mali zao, ikitokea hivyo, basi ni wajibu kuutetea kwa kila mtu: muungwana, mtumwa, mwanamume, mwanamke, mwenye afya, mgonjwa, kipofu, kilema na wengineo wakihitajika. Na wajibu wenyewe haungoje kuwepo Imam au idhini yake. Vile vile wajibu huo hahusiki na walioshambuliwa na kulengwa tu, bali ni wajibu kwa kila atakayejua hata kama siye aliyelengwa, ikiwa hajui kuwa walioshambuliwa wanamuweza adui yao. Na wajibu unasisitizwa kwa aliyekaribu na aliye karibu zaidi.”

Kisha akaendelea kusema mwenye A-Jjawahir “Kujitetea mtu ni wajib hata kama hadhanii usalama wake, kwa sababu tayari yuko hatarini kwa namna yoyote. Ama kupigania heshima yake na mali yake ni wajibu ikiwa anaona hakuna hatari ya nafsi yake, kwa kuhofia isiende nafsi, mali na heshima pamoja. Vile vile kutetea maisha ya mtu mwingine, mali yake au heshima yake.”

Mafaqihi wametoa fat-wa ya wajibu wa kumwokoa mwenye kuangamia na kuzima moto ikiwa unaangamiza mali ya mtu mwingine. Na kwamba ni wajibu kwa mwenye kuswali kukata swala yake ili kuzuia hatari ya nafsi yoyote muhimu au mali ambayo ana wajib kwake kuihifadhi; iwe ni yake au ya mtu mwingine. Na atakayemuona mtoto jangwani ni wajib kumwokota na kumuhifadhi ikiwa hawezi kujilinda.

Imepokewa riwaya kwamba watuhumiwa watatu, waliomuua mtu, waliletwa kwa Imam Ali (a.s.). Mmoja alimshika yule aliyeuliwa, wapili akaua na watatu akaangalia bila ya kufanya lolote. Yule aliyeua akamhukumu kuuliwa na aliyeshika, afungwe maisha na aliyeangalia, ang’olewe macho. Mafakihi wameitumia riwaya hii.

Mwenye kufuatilia utafiti wa vitabu vingi vya Fiqh ataona aina hii ya maelezo; nayo ni dalili mkataa kwamba mtu kumsaidia na kumwokoa mtu mwingine ni wajibu wa kisharia ikiwa ni umuhimu kufanya hivyo.

Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana.

Ncha ya kwanza ya mchana ni wakati wa swala ya asubuhi, ncha ya pili ni adhuhuri na alasiri, na usiku uliokaribu na mchana ni maghribi na isha. Aya nyingine inasema:

أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ ۖ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا {78}

“Simamisha swala jua linapopinduka mpaka giza la usiku na Qur’ani ya alfajiri. Hakika Qur’ani ya alfajiri ni yenye kushuhudiwa.” (17:78).

Kupinduka jua ni wakati wa swala ya adhuhuri na alasiri na giza la usiku ni wakati wa swala ya maghrib na isha na Qur’ani ya alfajiri ni swala ya asubuhi ambayo watu wanaishuhudia. Ufafanuzi uko katika vitabu vya Fiqh, ikiwemo Juzuu ya kwanza ya Fiqhul-Imam Jaffer As-swadiq.

Hakika mema huondoa maovu.

Mwenye Majmaulbayan, akiwanukuu wafasiri wengi, anasema kuwa makusudio ya mema hapa ni swala tano na kwamba hizo zinafuta madhambi yaliyo baina yao. Wengine wakasema ni kule kusema tu: “Subhanallah walhamdulillah walailahaillaha illallah wallahu akbar”

Tafsiri zote zinakataliwa na akili. Kwani hakuna mahusiano yoyote baina yake si ya kihukumu wala sharia au akili. Vile vile si kikanuni wala kidesturi. Hukumu yoyote ya wajibu au haramu haiifungi hukumu nyingine. Ama hadith inayosema: “Kila anaposwali hufutiwa madhambi yaliyo baina ya swala mbili ni fumbo la kwamba swala ina mema mengi.

Ikiwa mwenye kuswali ana maovu huwekwa kwenye kiganja na yale mengine kwenye kiganja, hapo mazuri huondoa mabaya. Kwa sharti yasiwe makubwa wala yasiwe ni haki miongoni mwa haki za watu. Maelezo ya maudhui haya yamekwishatangulia katika Juz. 2 (2:217).

Hiyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.

Hiyo ni ishara ya amri ya kusimama sawa sawa (msimamo), kusimamisha swala na kukatazwa kuwategemea madhalimu. Makusudio ya wenye kukumbuka ni wenye kuwaidhika.

Na subiri, kwani hakika Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanaofanya wema.

Hapo kuna ishara kwamba mwenye kufuata njia ya sawa sawa atapambana na wapotevu wenye kupotoka na kwamba subra (uvumilivu) katika jihadi yao ndio twaa bora na wema mkuu.

فَلَوْلَا كَانَ مِنَ الْقُرُونِ مِنْ قَبْلِكُمْ أُولُو بَقِيَّةٍ يَنْهَوْنَ عَنِ الْفَسَادِ فِي الْأَرْضِ إِلَّا قَلِيلًا مِمَّنْ أَنْجَيْنَا مِنْهُمْ ۗ وَاتَّبَعَ الَّذِينَ ظَلَمُوا مَا أُتْرِفُوا فِيهِ وَكَانُوا مُجْرِمِينَ {116}

Basi mbona hawakuwamo katika watu wa karne ya kabla yenu wenye akili wakakataza ufisadi katika nchi? Na wakafuata wale waliodhulumu waliyostareheshewa na wakawa ni wakosefu.

وَمَا كَانَ رَبُّكَ لِيُهْلِكَ الْقُرَىٰ بِظُلْمٍ وَأَهْلُهَا مُصْلِحُونَ {117}

Na hakuwa Mola wako wa kuiangamiza miji kwa dhulma na hali watu wake ni watenda mema.

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَجَعَلَ النَّاسَ أُمَّةً وَاحِدَةً ۖ وَلَا يَزَالُونَ مُخْتَلِفِينَ {118}

Na lau Mola wako angelitaka angeliwafanya watu wote kuwa umma mmoja. Na hawaachi kukhitalifiana.

إِلَّا مَنْ رَحِمَ رَبُّكَ ۚ وَلِذَٰلِكَ خَلَقَهُمْ ۗ وَتَمَّتْ كَلِمَةُ رَبِّكَ لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ {119}

Ispokuwa wale ambao Mola wako amewarehemu. Na kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako: kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa majini na watu kwa pamoja.