read

Aya 116-119: Watu Wa Karne Zilizotangulia

Basi mbona hawakuwamo katika watu wa karne ya kabla yenu wenye akili wakakataza ufisadi katika nchi?

Baada ya Mwenyezi Mungu(s.w.t.) kutaja maangamizi yaliyowapitia kaumu ya Nuh, ya A’d, ya Thamud na wengineo kwa sababu ya jeuri na ufisadi wao, anasema hivi hawakupatikana watu na viongozi wema kuweza kuzuia dhulama na ufisadi.

Kwa sababu ya dhulma hiyo na ufisadi na wengine wakayanyamazia, basi walistahiki adhabu na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu wote;

Isipokuwa wachache tu, tuliowaokoa miongoni mwao.

Ambao ni mitume na wale walioamini pamoja nao. Yaani kikundi kidogo alichokiokoa Mwenyezi Mungu kilikuwa kikiamrisha mema na kukataza maovu, lakini hakuna amri kwa asiyetiiwa.

Na wakafuata wale waliodhulumu waliyostareheshewa na wakawa ni wakosefu.

Makusudio ya waliyostreheshewa ni mali zao. Wale wachache waliwakataza wengine ufisadi na dhulma, lakini kwa sababu ya mali zao hawakujali kabisa. Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا أَرْسَلْنَا فِي قَرْيَةٍ مِنْ نَذِيرٍ إِلَّا قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُمْ بِهِ كَافِرُونَ {34}

وَقَالُوا نَحْنُ أَكْثَرُ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ {35}

“Na hatukutumma mwonyaji yoyote kwenye mji, ila husema wenyeji wake waliostareheshwa: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo. Na wakasema sisi tuna mali nyingi zaidi na watoto, wala sisi hatutadhibiwa.” (34:34-35) .

Na hakuwa Mola wako wa kuiangamiza miji kwa dhulma na hali watu wake ni watenda mema.

Vinginevyo angelikuwa sawa kwake, mwema na muovu na mzuri na mbaya. Haiwi hivyo kwa Mwnyezi Mungu:

مَا يَفْعَلُ اللَّهُ بِعَذَابِكُمْ إِنْ شَكَرْتُمْ وَآمَنْتُمْ ۚ وَكَانَ اللَّهُ شَاكِرًا عَلِيمًا {147}

“Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye (kupokea) shukrani Mjuzi. Juz. 5 (4:147).

Na lau Mola wako angelitaka angeliwafanya watu wote kuwa umma mmoja.

Tangu iliposhuka Aya hii mpaka leo, watu wengi wanasema: Kwanini hakutaka Mwenyezi Mungu. Laiti Mwenyezi Mungu angelifanya hivyo miji ikawa na raha na kuepukana na balaa hili la kubaguana.

Jibu linafafanuka kwa namna ifuatayo:

1. Kabla ya kitu chochote inatakikana tuwe na yakini kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hataki waja wake wachukiane, wabughudhiane au wachinjane. Kwanini isiwe hivyo na hali yeye ndiye mwenye kusema:

وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا {46}

Wala msizozane, msije mkafunjika moyo.” (8:46).

Haina maana kuwa kwa vile hakuwalazimisha mshikamano na maafikiano, basi anawataka wazozane na wapigane. Kwa mfano ukisema: Sitaki wanangu wawe na rai moja katika siasa. Haina maana kwamba unataka wapigane na wauane.

2. Kulazimisha kwenye dini kuna njia mbili: Kwanza, ni kutumia nguvu. Pili, ni kuumba Mwenyezi Mungu imani katika moyo wa mtu, kama alivyomba ulimi katika mdomo.

Njia ya kwanza inapingana na misingi ya dini na ya mantiki pia. Kwa sababu nguvu haitengenezi imani; bali ni kinyume. Kwa vile njia ya imani ya haki ni dalili. Ndio maana Qur’ani ikazionyesha dalili hizi kwa mifumo mbalimbali. Na ikamuhimiza mtu kuzichunguza, kuziangalia vizuri na kuzizingatia. Ni hiyari yake sasa kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Ama amri ya kupigana ni kwa ajili yakuitetea sharia ya haki na uadilifu na kuchunga usalama na amani kwa jamii.

Na njia ya pili, ya kuumba imani moyoni, itamatoa mtu kwenye utu wake, awe sawa na matunda yaliyo mtini, hana matakwa wala fikra juu ya muumbaji na hatastahiki kusifiwa wala kulaumiwa au kuwa na thawabu au adhabu. Yametangulia maelezo katika kufasiri Juz. 7 (6:35).

Kwa ufupi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakutaka kwa namna yoyote ile kuwatumilia watu nguvu katika imani. Kwa sababu lau angelifanya hivyo angaliwaondolea sifa ya ubinadamu; wangelikuwa kama wanyama na wadudu, hawana majukumu yoyote wala hawahisabiwi chochote. Lakini Mwenyezi Mungu alitaka amtofautishe binadamu na viumbe vyote na afikie hali ambayo hakutakua na chochote juu yake isipokuwa Muumbaji tu.

Itakuwa Muhali kufikia cheo hiki bila ya juhudi na khiyari. Ndio maana Mwenyezi Mungu, amempa uwezo, utambuzi wa mambo, mhemuko na kumwonyesha njia mbili, kisha akamwachia uhuru wa hiyari, ili abebe mwenyewe lile atakalojichagulia.

Na hilo litamkamilishia ubinadamu wake kamili. Matokeo ya hayo sasa ni kutofautiana watu rai zao na itikadi zao. Angalia Juz. 2 (2:213) na Juz. 5 (4:78).

Na hawaachi kukhitalifiana.

Yaani watu waliopita walikhitalifiana na wataeendelea kukhitalifiana milele. Kwa vile hiyo ni natija ya kumfanya binadamu awe ni mwenye khiyari akielekea popote apendapo.

Ispokuwa wale ambao Mola wako amewarehemu.

Makusudio ya waliorehemiwa ni wale walioshikamana kiuhakika na kiikhlasi, hawavurugani. Ikitokea kutofautiana basi ni katika rai na mitazamo. “Kutofautiana rai hakuharibu mapenzi.” Na kuweko mitazamo tofauti kunaleta faida. Kwa sababu kauli yenye nguvu ni ile ambayo inakuwa na nguvu hata kama kuna kauli nyinginezo.

Na kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaumba.

Yaani Mwenyezi Mungu amewaumba kwa hiyo rehema na kwa kuhurumiana wao kwa wao. Itawapa rehema yake Mwenyezi Mungu mtukufu, ikiwa wataitafuta haki na kuitumia.

Abu Bakr almua’firiy Al-andalusi (Mhispania) anasema katika Kitabu Ahkamul Qur’ani: “Hakika Mwenyezi Mungu amewaumba watu ili watofautiane sio wahurumiane.”

Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu anataka shari, kufru na maasi. Ikiwa Mwenyezi Mungu anataka shari basi kuna tofauti gani na Iblis aliyesema “Nitawapoteza wote”? Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu Juz. 7 (6:100).

Na litatimia neno la Mola wako: kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa majini na watu kwa pamoja.

Yaani Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ataijaza Jahannam waasi wafuasi wa shetani miongoni mwa majini na watu. Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema:

قَالَ فَالْحَقُّ وَالْحَقَّ أَقُولُ {84}

لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنْكَ وَمِمَّنْ تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ {85}

“Akasema: Haki na haki ninaisema. Hakika nitaijaza Jahannam kwa wewe na kwa wale wote wenye kukufuata miongoni mwao.” (38:84-85).

وَكُلًّا نَقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنْبَاءِ الرُّسُلِ مَا نُثَبِّتُ بِهِ فُؤَادَكَ ۚ وَجَاءَكَ فِي هَٰذِهِ الْحَقُّ وَمَوْعِظَةٌ وَذِكْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ {120}

Na yote tunayokusimulia katika habari za mitume ni ya kuufanya thabiti moyo wako. Na katika hii imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa wenye kuamini.

وَقُلْ لِلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنَّا عَامِلُونَ {121}

Na waambie wale wasioamini: Fanyeni muwezavyo, nasi (pia) tunafanya.

وَانْتَظِرُوا إِنَّا مُنْتَظِرُونَ {122}

Na ngojeni, hakika sisi tunangoja.

وَلِلَّهِ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَإِلَيْهِ يُرْجَعُ الْأَمْرُ كُلُّهُ فَاعْبُدْهُ وَتَوَكَّلْ عَلَيْهِ ۚ وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ {123}

Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyofichikana katika ardhi na mbingu. Na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu yeye na umtegemee yeye Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.