read

Aya 12 – 14: Mbona Hakuteremshiwa Hazina

Maana

Basi pengine utaacha baadhi ya yale uliyopewa wahyi.

Mtume Muhammad (s.a.w.) alikuwa akiwasomea washirikina Aya za Qur’anii kwa kuwalingania kwenye imani ya umoja na ufufuo. Mara nyingine wakimkejeli na mara nyingine wakitaka aina ya miujiza kwa kukaidi sio kutaka kuongoka. Hali hiyo ilikuwa ikimuuma Mtume Muhammad (s.a.w.) na kumhuzunisha, ndipo Mola Mtukufu akamwambia, ili kumwondokea huzuni hiyo.

Endelea na mwito wako wala usijali wayasemayo na wayatakayo. Utawafanya nini hao! Je, uwaache wahyi na ufute kwenye Qur’anii yale yasiyowapendeza? Hapana! Wewe huwezi kufanya hivyo. Kwa hiyo basi kwa nini unahuzunika na kujitia jaka moyo?

Haya ndiyo maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu. ‘Basi pengine uache baadhi ya yale tuliyokupa wahyi.’ Kwa sababu Mtume ni maasum hawezi na haiwezekani kuacha kitu katika wahyi. Aya inafuatana na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu.

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ لَا يَحْزُنْكَ الَّذِينَ يُسَارِعُونَ فِي الْكُفْرِ{41}

“Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wanaofanya haraka kukufuru.” Juz.6 (5:41).

Na kifua chako kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema, mbona hakuteremshiwa hazina au wakaja naye Malaika?

Miongoni mwa mambo waliyoyataka washirikina, kwa Mtume Muhamamad (s.a.w.), ni kunyesha mvua ya dhahabu au amjie Malaika ashuhudie utume wake.

Hivi ndivyo wanavyofikiria wenye mali na utajiri tangu zamani na sasa. Wanaamini kwamba cheo ni lazima kiwe kwa wenye mali. Ama mafukara, wao ni wakufuata tu.

Majigambo yao haya yalimsababishia Mtume (s.a.w.) huzuni, ndipo Mola akamwambia:
Hakika wewe ni muonyaji tu.

Lako ni kufikisha wahyi tu. Usifazahike na upumbavu wa wapumbavu na ujinga wa wajinga.

Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu.

Kauli kwake ni yenye kuhifadhiwa na siri inafichika na kila nafsi ni rahani wa ilichokichumma. Aya hii inaambatana na tuliyo yataja Juz. 8 (6:111) kifungu cha ‘aina ya watu’

Au wanasema ameizuia? Sema, basi leteni Sura kumi zilizozuliwa mfano wa hii na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.1 (2:23).

Na wasipowaitikia, basi jueni ya kwamba imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana Mola isipokuwa Yeye, basi je, nyinyi ni waislamu?

Wasipowaitikia ni wale wanaoikadhibisha Qur’ani na wasioitikiwa ni Mtume Muhammad (s.a.w.) na kila mwenye kuulingania Uislam na ‘jueni’ anaambiwa kila mwenye kuikadhibisha Qur’ani wakati wowote na mahali popote alipo.

Maana ni kuwa wajue wanaokadhibisha ambao wameshindwa kuipinga Qur’ani, kwamba hiyo imeteremshwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.) kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye hapana Mola isipokuwa yeye.

Hakuna lililobaki isipokuwa musilimu, kwani upinzani umewashinda. Inatosha kusema kuwa Qur’ani ni muujiza kule kuwa imebakia na thamani yake na utukufu wake pamoja na kuwa umepita muda mrefu.

Na itabakia hivyo ikimvutia kila mwenye kuisoma na mawenye kuisikiliza, mpaka siku ya mwisho. Na hilo ni kwa vile hakika yake ni ya kiutu inayokubaklika kwa kila mwenye akili, vyovyote alivyo.

مَنْ كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لَا يُبْخَسُونَ {15}

Wanaotaka maisha ya dunia na pambo lake, tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.

أُولَٰئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ إِلَّا النَّارُ ۖ وَحَبِطَ مَا صَنَعُوا فِيهَا وَبَاطِلٌ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {16}

Hao ndio ambao katika Akhera hawatakuwa na kitu ispokuwa moto. Na yataharibika waliyokuwa wakiyafanya humo na yatapotea bure waliyokuwa wakiyatenda.

أَفَمَنْ كَانَ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِنْ رَبِّهِ وَيَتْلُوهُ شَاهِدٌ مِنْهُ وَمِنْ قَبْلِهِ كِتَابُ مُوسَىٰ إِمَامًا وَرَحْمَةً ۚ أُولَٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۚ وَمَنْ يَكْفُرْ بِهِ مِنَ الْأَحْزَابِ فَالنَّارُ مَوْعِدُهُ ۚ فَلَا تَكُ فِي مِرْيَةٍ مِنْهُ ۚ إِنَّهُ الْحَقُّ مِنْ رَبِّكَ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ {17}

Basi je, aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake na anaifuata na shahidi atokaye kwake na kabla yake kulikuwa na Kitabu cha Musa kilichokuwa kiongozi na rehema (atakuwa muongo?) Hao wanamwamini yeye. Na atakayemkataa katika makundi, basi moto ndio miadi yake. Basi usiwe na shaka naye, hakika yeye ni haki itokayo kwa Mola wako. Lakini watu wengi hawaamini.