read

Aya 120-123: Tunayokusimulia

Na yote tunayokusimulia katika habari za mitume ni ya kuufanya thabiti moyo wako. Na katika hii imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa wenye kuamini.

Hii ni ishara ya sura, ukumbusho ni mazingatio na makusudio ya kuufanya thabiti moyo wa Mtume (s.a.w.) ni subra na uvumilivu wa maudhi katika njia ya ujumbe wake na kuufikisha. Maana ni kuwa habari za mitume na watu wao tulizokusimulia ni haki hazina shaka na kwamba lengo lake ni kukupunguzia adha inayokupata.

Kwani anayeona masaibu ya mwingine, yake huyaona madogo. Vile vile katika visa hivi kuna mawaidha na mazingatio kwa mwenye kuwaidhika na kuzingatia.

Kwa hakika wanahistoria wa zamani walikuwa wakitilia umuhimu matukio ya siasa na dola na wapya wakatilia umuhimu uchumi, sayansi, sanaa, fasihi na mengineyo katika harakati za binadamu.

Lakini Qur’ani inaleta matukio kuwa ni mazingatio na mawaidha yatakayomwongoza binadamu kwenye njia iliyo sawa. Kauli yake Mwenyezi MunguMtukufu: “N mawaidha na ukumbusho” inaeleza hivyo. Aya nyingine inasema:

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِمَنْ يَخْشَىٰ {26}

“Hakika katika hayo mna mazingatio kwa anayemcha (Mwenyezi Mungu)” (79:26).

Na waambie wale wasioamini: Fanyeni muwezavyo, nasi (pia) tunafanya.

Umepita mfano wake katika Juz. 8 (6:135).

Na ngojeni, hakika sisi tunangoja.

Vile vile mfano wake umepita katika (6: 158).

Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyofichikana katika ardhi na mbingu.

Kila siri kwake iko wazi na kila lililofichikana linaonekana. Katika mfano wa hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye; anajua kilichomo nchi kavu na kilichomo baharini; na halianguki jani ila analijua wala punje katika giza la ardhi; wala kibichi au kikavu, ila kimo katika Kitabu kinachobainisha.” Juz.7 (6:59).

Na mambo yote yatarejezwa kwake.

Wala hakuna kitu kinachokimbia ufalme wake.

Basi muabudu yeye na umtegemee yeye.

Yaani ikiwa Mwenyezi Mungu yuko hivi, basi yeye ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa na kutegemewa si mwengine. Amri ya kurukui na kusu- judi ni nyepesi, lakini kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuachana na wengine, asiyekuwa Yeye ni jambo zito, isipokuwa kwa wanaomcha Mwenyezi Mungu.

Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.

Atawalipa wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyafanya na atawalipa mema wale waliofanya mema. Imesemwa kwenye Nahjul balagha: “Usighafilike kwani wewe hujasahauliwa… Ee! Kuangamia kwa mwenye kughafilika kuwa umri wake ni hoja juu yake.” Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuhifadhi na yale yanayoleta majuto na majonzi.