read

Aya 15-17: Wanaotaka Mapambo Ya Dunia

Wanotaka maisha ya dunia na pambo lake, tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.

Atakayepanda atavuna, mwenye kufanya biashara vizuri, atapata faida, mwenye kusoma kwa bidii, atafaulu, mwenye kujenga viwanda, kuchimba visima vya mafuta na madini bila shaka hazina yake itajaa mali na kila mwenye kulifanyia bidii jambo lolote, atapata matunda yake, awe mumin au kafiri.

Riziki huja ikiwa ni natija ya kazi; haipunguzwi na ulafi wala kuzidishwa na imani. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.” Hata hivyo ufisadi nao una athari zake; kama tulivyoieleza katika Juz. 6 (5:64).

Neema za maisha ya Akhera zinashikiliwa na kazi ya hapa duniani; sawa na mapambo katika maisha haya. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu na hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema:

أَمْ حَسِبْتُمْ أَنْ تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنْكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ {142}

“Je, mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu haja wajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira?” Juz.4 (3:142).

Amesema tena Mwenyezi Mnungu:

وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُمْ مَشْكُورًا {19}

“Na anayeitaka Akhera na akaihangaikia inavyotakikana, naye ni mumin, basi hao mahangaiko yao yatakuwa ni yenye kushukuriwa” (17:19)

Mwenye kuhangaikia riziki yake nzuri ya halali, basi atakuwa amehangaikia dunia na Akhera.

Hao ndio ambao katika Akhera hawatakuwa na kitu isipokuwa moto.

Hao ni ishara ya wale waliozama katika dunia wakawa hawajishughulishi na lolote isipokuwa dunia tu. Hawatakuwa na malipo yoyote isipokuwa adhabu.

Na yataharibika waliyokuwa wakiyafanya humo na yatapotea bure waliyokuwa wakiyatenda.

Humo ni duniani. Maana ni kuwa matendo yao si kitu mbele ya Mwenyezi Mungu; hata kama watu watanufaika nayo, maadamu lengo halikuwa la heri ya kiutu. Kwa ufupi, mwenye kutafuta heri yoyote itamfikisha pale anapopataka; mwenye akili hujichagulia njia ya uokovu bila ya kudanganyika na chochote.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumtaja yule anayejishighulisha na dunia tu, amemtaja anayetenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kumlin- gania yeye tu, akiwa na dalili itokayo kwa Mola wake. Ufafanuzi ni kama ufuatao:

Basi je, aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake.

Makusudio ya aliye na dalili wazi ni Muhammad (s.a.w.) na dalili wazi ni Qur’ani.

Na anaifuata na shahidi atokaye kwake.

Tabari, Razi, Abu Hayan Alaandalusi na wengineo katika wafasiri, wamesema kuwa kuna kutofautiana kuhusu shahidi huyu anayemshuhudia Muhammad na utume wake. Wengine wamesema ni Jibril, wengine ni ulimi wa Muhammad na wengine wakasema ni Ali bin Abutwalib.

Waliosema kuwa ni Ali wametoa dalili kwa Hadith aliyoipokea Bukhari katika Sahih yake, inayosema: “Alisema Mtume (s.a.w.) kumwambia Ali: Wewe ni katika mimi na mimi ni katika wewe.” Na Umar akasema: Mtume (s.a.w.) alikufa akiwa yuko radhi naye (Ali).

Na kabla yake kulikuwa na Kitabu cha Musa kilichokuwa kiongozi na rehema (atakuwa muongo?).

Tawrat ilimbashiria Muhammad na utume wake kabla ya kushuhudiwa na Qur’ani. Tawrat ni Kitab cha Mwenyezi Mungu alichomteremshia Musa na ni kiongozi kinachofuatwa katika mambo ya kidini na rehema kwa anayekitumia kabla ya kupotolewa.

Hao wanamwamini yeye.

Yaani yeye Muhammad (s.a.w.) na hao ni wale wanaofuata dalili za haki na ubainifu wake; kama vile Qur’ani na Kitabu cha Musa jinsi kilivyoteremshwa. Na hao, wanaoashiriwa, hawakutajwa katika Qur’ani, isipokuwa wametajwa kwa sifa zao.

Na atakayemkataa katika makundi, basi moto ndio miadi yake.

Makusudio ya makundi ni yaliyompiga vita Mtume (s.a.w.). Mwenye Tafsir Al-manar na sheikh Al-maraghi, wamesema: “Amesema Muqatil: Hao ni ni ukoo wa Ummayya, ukoo wa Mughira bin Abdallah Al-makhzumi na jamii ya Twalha bin Abdallah na mfano wao katika Mayahudi na manaswara”

Basi usiwe na shaka naye, hakika yeye ni haki itokayo kwa Mola wako.

Dhamir katika usiwe na shaka naye na hakika yeye, inaweza kuwa ni ya Muhammad au ya Qur’ani na msemo wa usiwe, unaelekezwa kwa kila aliyesikia ujumbe wa Muhammad. Maana ni kuwa haitakikani kwa mwenye akili kutia shaka kuwa Muhammad ni mtume na kwamba Qur’ani ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, baada ya kuweko na dalili zilizowazi juu ya hilo.

Ikiwa mtu anaweza kutia shaka kuwa Tawrat na Injil zimetoa bishara ya utume wa Muhammad, je anaweza kutia shaka kwamba Muhammad amewapatia watu njia za maisha na kwamba yeye ameleta ambayo hakuwahi kuwaletea nabii au kiongozi yeyote.

Lakini watu wengi hawaamini haki, kwa sababu hiyo ni adui wa dhulma yao na ufisadi wao katika nchi au kwa kuwa wao hawatilii umuhimu dini ya haki au batil madamu maisha yao hayategemei dini. Sisi tutaachana nao hawa na yale waliyojichagulia; na wao wawaache wengine na yale waliyojichagulia na wasiingilie dini wasiyoijua isipokuwa jina tu.

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّهِ كَذِبًا ۚ أُولَٰئِكَ يُعْرَضُونَ عَلَىٰ رَبِّهِمْ وَيَقُولُ الْأَشْهَادُ هَٰؤُلَاءِ الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَىٰ رَبِّهِمْ ۚ أَلَا لَعْنَةُ اللَّهِ عَلَى الظَّالِمِينَ {18}

Ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uongo. Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao. Na watasema mashahidi: Hawa ndio waliomzulia Mola wao uwongo. Sikilizeni! Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.

الَّذِينَ يَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ وَيَبْغُونَهَا عِوَجًا وَهُمْ بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ {19}

Ambao wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wanataka ipotoke na wanaikataa Akhera.

أُولَٰئِكَ لَمْ يَكُونُوا مُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَمَا كَانَ لَهُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ ۘ يُضَاعَفُ لَهُمُ الْعَذَابُ ۚ مَا كَانُوا يَسْتَطِيعُونَ السَّمْعَ وَمَا كَانُوا يُبْصِرُونَ {20}

Hao hawataweza kuponyoka katika nchi na wala hawana walinzi badala ya Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa adhabu maradufu. Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.

أُولَٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنْفُسَهُمْ وَضَلَّ عَنْهُمْ مَا كَانُوا يَفْتَرُونَ {21}

Hao ndio ambao wamezitia hasara nafsi zao. Na yamepotea waliyokuwa wakiyazua.

لَا جَرَمَ أَنَّهُمْ فِي الْآخِرَةِ هُمُ الْأَخْسَرُونَ {22}

Bila shaka hao ndio wenye hasara zaidi katika Akhera.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَأَخْبَتُوا إِلَىٰ رَبِّهِمْ أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {23}

Hakika wale walioamini na wakafanya matendo mema na kunyenyekea kwa Mola wao, hao ndio watu wa Peponi, wao watadumu humo.

مَثَلُ الْفَرِيقَيْنِ كَالْأَعْمَىٰ وَالْأَصَمِّ وَالْبَصِيرِ وَالسَّمِيعِ ۚ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ {24}

Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu na kiziwi na anayeona na anayesikia. Je, hawa wawili wanaweza kuwa sawa? Je, hamfikiri?