read

Aya 18-24: Watahudhurishwa Mbele Ya Mola Wao

Maana

Ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uongo.

Ikiwa kumzulia uongo kiumbe ni kauli mbaya, itakuwaje kwa muumba? Kumzulia uongo Mwenyezi Mungu kuko aina nyingi; kama vile kumfanyia washirika, kuhalalisha na kuharamisha bila ya hoja kutoka Qur’ani au Hadith, wizi na unyang’anyi kwa kisingizio cha demokrasia n.k.

Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao.

Hao ni ishara ya wale wazushi, na kwamba wao kesho watasimama kuhisabiwa; kaulizao na vitendo vyao vitahudhurishwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Na watasema mashahidi, hawa ndio waliomzulia Mola wao uwongo. Sikilizeni! Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hahitajii mashahidi, kwa sababu yeye anajua na ni muweza wa kila kitu; anahukumu kwa ujuzi wake na uadilifu wake na kutekeleza kwa neno ‘kuwa.’

Ama ushuhuda wa Malaika na mitume na ushuhuda wa ndimi za waongo waliopotea na mikono yao na miguu yao, lengo lake ni kuzidisha majuto na kwamba wawe na yakini kuwa hawana hoja wala udhuru watakaoukimbilia; hakuna kuepuka laana ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Ambao wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wanataka ipotoke na wanaikataa Akhera.

Aya hii ni ubainifu na tafsiri ya madhalimu ambao Mwenyezi Mungu amewalaani; kwamba wao wanawazuia watu na tawhid na imani ya ufufuo. Vile vile wanawadanganya kwa shirki na kuikataa siku ya mwisho.

Hao hawataweza kuponyoka katika nchi.

Vipi waweze kufanya hivyo na hali lau Mwenyezi Mungu angelitaka asingeliacha yeyote kwenye ardhi

Na wala hawana walinzi badala ya Mwenyezi Mungu.

Hata masanamu waliyokuwa wakiyafanya mungu na kuyaabudu na pia watawa na wakuu wao waliowafanya waungu hawawezi kufaa kitu.

Watazidishiwa adhabu maradufu.
Hili ni jawabu la swali la kukadiriwa; kama kwamba muulizaji ameuliza wale waliozulia Mwenyezi Mungu uwongo wana hukumu gani? Basi Mwenyezi Mungu akajibu, watazidishiwa adhabu mara mbili.

Kuwa maradufu adhabu hapa ni fumbo la ukali wa adhabu. Wengine wamesema maana yake ni kuwa kila kosa lina adhabu yake: Watadhibiwa kwa uzushi na watadhibiwa kwa kuzuia njia na kupinga ufufuo.

Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.

Hii ni sababu ya kufanyiwa adhabu maradufu kwamba Mwenyezi Mungu akiwapa adhabu hii kwa vile walikuwa hawawezi kuisikiliza haki wala kuichunguza, kwa sababu ya kuzama kwao kwenye kufru na inadi.

Hao ndio ambao wamezitia hasara nafsi zao.

Mwenye hasara zaidi katia watu ni yule aliyejihasiri mwenyewe na adhabu isiyokwisha wala kupunguzwa.

Na yamepotea waliyokuwa wakiyazua.

Ambayo ni kumfanyia Mwenyezi Mungu washirika na watetezi, kuhalalisha na kuharamisha kwa uwongo na uzushi.

Bila shaka hao ndio wenye hasara zaidi katika Akhera.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema kuwa wao wamezitia hasara nafsi zao, amesisitiza kuwa hasara hii itatokea tu, haina kizuizi wala kuikimbia.

Hakika wale walioamini na wakafanya matendo mema na kun- yenyekea kwa Mola wao, hao ndio watu wa Peponi, wao watadumu humo.

Baada ya Mwenyezi Mungu(s.w.t.) kuwataja makafiri, amefuatilia kwa kuwataja wauminii na malipo yao; kama ilivyo desturi ya Qur’ani – kutaja vitu na vinyume vyake.

Neno kunyenyekea hapa limetumika kutokana na neno ‘khibt’ lenye maana ya kunyenyekea na utulivu. Tabrasi anasema: Asili ya neno khibt ni usawa wenye kuenea yaani ardhi iliyo sambamba.

Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu na kiziwi na anayeona na anayesikia.

Makundi mawili ni makafiri na waumini. Moja halinufaiki na hisia zake, ambapo kipofu hanufaiki na macho yake na kiziwi hanufaiki na masikio yake; na jingine linanufaika na hisia hizo mbili. Imama Ali (a.s.) anasema: “Mwenye kuzingatia huwa na busara na mwenye busara hufahamu na mwenye kufahamu huwa na elimu.” Ni hivyo hivyo mwenye kusikia.

Je, hawa wawili wanaweza kuwa sawa? Kwa sifa na hali. Je, hamfikiri? Hiyo tofauti?

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ إِنِّي لَكُمْ نَذِيرٌ مُبِينٌ {25}

Hakika tulimpeleka Nuh kwa watu wake. Hakika: mimi kwenu ni muonyaji abainishaye.

أَنْ لَا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّهَ ۖ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ أَلِيمٍ {26}

Ya kwamba msiabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi nawahofia na adhabu ya siku iumizayo.