read

Aya 21 -22: Aliyemnunua

Na yule aliyemnunua kule Misri alimwambia mkewe: “Mtengenezee makazi ya heshima, huenda akatufaa au tukamfaya mtoto.”

Yusuf alinadiwa sokoni na akanunuliwa na Aziz (mheshimiwa). Hii ni lakabu ya waziri mkuu wa mfalme. Linalotufahamisha kuwa yeye ndiye aliyemnunua ni kauli yake Mwenyezi Mungu kwnye Aya 30 katika sura hii: “Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa muheshimiwa anamtaka mtumishi wake pasipo kutakiwa naye”

Waziri alitambua werevu na akili ya Yusuf, akamwambia mkewe amuweke makazi ya kiheshima. Kwa maana ya kuwa akishakuwa mkubwa, aje asimamie mambo yao au wamfanye ni mtoto wao.

Kwa sababu mheshimiwa alikuwa mgumba, hana mtoto; kama walivyosema wafasiri wengi. Na Aya inaashiria hilo pale iliposema: “Au tumfanye mtoto”

Na kama hivyo tulimkalisha Yusuf katika nchi ili tumfundishe kufasiri mambo.

Mwenyezi Mungu alimneemesha Yusuf kwa kumwokoa na vitimbi vya ndugu zake, kumtoa kisimani, kumjaalia kuwa katika nyumba ya mheshimiwa, kumweka kwenye moyo wa mwenye nyumba na kumfundisha hakika ya mambo, ikiwa ni pamoja na kutabiri ndoto.

Neema zote hizi zilimwinua Yusuf mbele za watu na kumfanya awe ni tegemeo la watu wote na mwenye kuheshimiwa. Vile vile kuwekwa kuwa ndiye mweka hazina wa nchi ya Misr na kuambiwa na mfalme: “Hakika wewe leo kwetu ni mwenye heshima mwenye kuaminika”

Na mwenyezi Mungu ndiye mshindi katika jambo lake.

Ndugu zake Yusuf walimtakia shari na Mwenyezi Mungu alimtakia kheri.

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَنْ يَقُولَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ {82}

“Hakika amri yake anapotaka chochote hukiambia ‘Kuwa,’ basi kinakuwa” (36:82).

Lakini watu wengi hawajui.

Kuwa amri ni ya Mwenyezi Mungu peke yake na kwamba mwenye kujifanya jeuri na kughurika na nguvu zake na uwezo wake, Mwenyezi Mungu atampatiliza kwa mashiko ya mwenye nguvu mwenye uweza.

Na alipofikilia kukomaa kwake, tulimpa hukumu na elimu.

Kukomaa hapa ni kukomaa kimwili na kiakili. Ahglab, hali hii huaanzia kwenye umri wa miaka thelathini na kuendelea hadi arobaini. Katika muda huu yanatimia maandalizi ya utume na kuanza wahyi. Makusudio ya hukumu hapa ni hekima; yaani kila kitu kukiweka mahali pake na kupatia.

Maana ni kuwa, baada ya Yusuf kukomaa, Mwenyezi Mungu alimpa elimu na kumwezesha kuitumia.
Imesemekana kuwa makusudio ya elimu hapa ni utume. Hilo haliko mbali. Kwa sababu Yusuf ni katika mitume.

Na hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

Yusuf alitenda wema kwa uvumilivu wake na twaa yake kwa Mwenyezi Mungu, naye akamlipa mema kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa yeyote mwenye kutenda jambo.

وَرَاوَدَتْهُ الَّتِي هُوَ فِي بَيْتِهَا عَنْ نَفْسِهِ وَغَلَّقَتِ الْأَبْوَابَ وَقَالَتْ هَيْتَ لَكَ ۚ قَالَ مَعَاذَ اللَّهِ ۖ إِنَّهُ رَبِّي أَحْسَنَ مَثْوَايَ ۖ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ {23}

Na bibi mwenye nyumba aliyokuwemo (Yusuf) alimshawishi kinyume cha nafsi yake. Na akafunga milango akasema: Njoo. Akasema: Najikinga kwa Mwenyezi Mungu. Hakika yeye ni Bwana wangu ameyatengeneza vizuri makazi yangu. Hakika waliodhulumu hawatengenekewi.