read

Aya 23: Akamwambia Njoo

Na bibi mwenye nyumba aliyokuwemo (Yusuf) alimshawishi kinyume cha nafsi yake.

Neno alimshawishi linamaanisha kuwa alimfanyia vitimbi Yusuf ili atake vile anavyotaka yeye. Neno hili peke yake, linaonyesha kutojiheshimu. Lakini baadhi ya wafasiri wamechafua kurasa kuonyesha picha ya mke wa waziri kumvutia Yusuf kwa uzuri wake na ulimbwende wake. Na hayo hayana chimbuko lolote isipokuwa hadith za kiisrail. Amesema kweli mwenye Al-Manar: “Wapokezi wa kiisrail wamepokea riwaya zinazohusiana na Yusuf na mke wa waziri mambo ya ufedhuli ya uongo.

Mfano wa maneno hayo haujulikani kuwa unatoka kwa Mwenyezi Mungu, au kwa riwaya sahihi. Na hakuna yeyote anayedai hivyo”1

Mtu Na Mali Na Mambo Ya Kijinsiya Na Akafunga Milango.

Alijiuliza Mustafa Sadiq Arrafiy: kwanini ametumia neno waghallaqat, ambayo pia inakuwa kwenye mfumo wa kutilia mkazo jambo, na hakusema waaghlaqat? Na akajibu: “Hii inafahamisha kuwa yeye alipokata tamaa na kuona kuwa anataka kwenda zake, alikikuwa kama aliyepagawa akifikiria kufuli moja kama ni nyingi akakimbia kwenye mlango mmoja hadi mwingine, akiupigisha mkono wake, kama ambaye anajaribu kuziba milango sio kuufunga tu.”

Sisi hatuoni tofauti yoyote baina ya matamko hayo. Na hiyo inafahamisha tu uhodari wa Rafiy katika fasihi na uweza wake wa kutoa kitu kutoka kusiko na kitu.

Vyovyote iwavyo, ni kuwa Yusuf aliishi pamoja na mke wa waziri kwa muda mwingi akiwa ni barobaro mbichi, mwenye kuvutia. Kwa hiyo hakuna ajabu kwa mke wa waziri kuvutiwa naye wala si ajabu kwa Yusuf kuziepuka mbinu zake pamoja na kuwa matamanio mara nyingi yanashinda akali.

Kwani binadamu sio mtumwa wa matamanio yake ya kijinsia tu; kama asemavyo Freud; na wala si mtumwa wa mali na uchumi; kama asemavyo Marks. Ispokuwa anakuwa kwenye misukumo mingi, ikiwemo mambo ya kijinsia, mali, umashuhuri, utawala, dini, desturi kupenda nchi na mambo mazuri n.k. Kwa binadamu kuna misukumo miwili inayopingana:

Kheri inayomwongoza kwenye njia ya uongofu na shari inayompeleka kwenye njia ya maangamivu. Mara nyingine mvutano huu unaendelea kwa muda mfupi na mara nyingine kwa muda mrefu mpaka upande mmoja ushinde mwingine. Au hata unaweza kuendelea hadi mwisho, huku binadamu akiwa yuko huku na huku.

Mke wa waziri alipambana na mivutano miwili: Matamanio yake ya kinya- ma yaliyomfanya amtongoze Yusuf na kwa upande mwingine hadhi nakibri kinamkataza kujidhalilisha mbele ya aliyenunuliwa kwa thamani ndogo. Akabakia yuko katikati kiasi cha muda. Kisha akashindwa akanasa kwenye mtego wa matamanio ya kijinsia ambayo yanaonyeshwa na kauli yake: “Njoo.” Kauli hii si rahisi kuisema mwanamke ila yule aliyeshindwa kabisa, kiasi cha kuwa kama wazimu.

Ama Yusuf alikuwa na msukumo mmoja tu, unaomwongoza; na wala hakuna hata chembe ya msukumo mwingine katika moyo wake. Nao ni kumcha Mwenyezi Mungu na radhi yake. Hiyo peke yake ndiyo ladha yake na starehe yake, akasema:

Najikinga kwa Mwenyezi Mungu. Hakika yeye ni Bwana wangu ameyatengeneza vizuri makazi yangu. Hakika waliodhulumu hawatengenekewi.

Yaani najilinda kumwasi Mwenyezi Mungu. Vipi nimuasi na hali yeye amenipa hisani na fadhila nyingi; pale aliponitoa kisimani na akaufanya moyo wa waziri unipende na kuniweka kwenye daraja ya mwanawe. Na vipi nijidhulumu kwa kumwasi Mwenyezi Mungu na hali Mungu hawaongozi madhalimu? Hivi ndivyo ifanyavyo imani ya kweli. Inamlinda mtu na yaliyoharamu na kumpa ushindi katika kupambana na shetani na chama chake.

Wafasiri wengi wamesema kuwa dhamiri ya yeye ni bwana wangu inamrudia waziri kwa maana ya kuwa yeye ni mlezi wangu vipi nitamfanyia hiyana? Lakini mfumo wa maneno unaerejesha dhamiri kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kuwa karibu na neno: “Najilinda kwa Mwenyezi Mungu,” kuongezea kuwa msukumo wa kujizuia Yusuf ni kumwofia Mwenyezi Mungu, sio waziri.

Kama tutakadiria kuwa dhamir inarudia kwa waziri, basi makusudio yatakuwa ni kumtahayariza kuwa anavyotakikana ni kuwa na heshima na mumewe ambaye amemfanya awe na daraja ya juu.

وَلَقَدْ هَمَّتْ بِهِ ۖ وَهَمَّ بِهَا لَوْلَا أَنْ رَأَىٰ بُرْهَانَ رَبِّهِ ۚ كَذَٰلِكَ لِنَصْرِفَ عَنْهُ السُّوءَ وَالْفَحْشَاءَ ۚ إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُخْلَصِينَ {24}

Na hakika (mke) alimtamani naye alimtamani kama asingeona dalili ya Mola wake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa ili tumwepushie uovu na uchafu. Hakika yeye ni katika waja wetu waliotakaswa.

وَاسْتَبَقَا الْبَابَ وَقَدَّتْ قَمِيصَهُ مِنْ دُبُرٍ وَأَلْفَيَا سَيِّدَهَا لَدَى الْبَابِ ۚ قَالَتْ مَا جَزَاءُ مَنْ أَرَادَ بِأَهْلِكَ سُوءًا إِلَّا أَنْ يُسْجَنَ أَوْ عَذَابٌ أَلِيمٌ {25}

Na wote wawili wakakimbilia mlangoni na mwanamke akairarua kanzu yake kwa nyuma. Wakamkuta bwana wake mlangoni. Akasema: Hapana malipo ya mwenye kukusudia uovu kwa mkeo isipokuwa kufungwa gerezani au kupewa adhabu iumizayo.

قَالَ هِيَ رَاوَدَتْنِي عَنْ نَفْسِي ۚ وَشَهِدَ شَاهِدٌ مِنْ أَهْلِهَا إِنْ كَانَ قَمِيصُهُ قُدَّ مِنْ قُبُلٍ فَصَدَقَتْ وَهُوَ مِنَ الْكَاذِبِينَ {26}

Akasema (Yusuf): Yeye ndiye aliyenitaka bila ya mimi kumtaka. Na shahidi, aliyekuwa katika jamaa za mke, akatoa ushahidi, ikiwa kanzu yake imechanwa mbele, basi mke ni mkweli na yeye (Yusuf) ni katika waongo.

وَإِنْ كَانَ قَمِيصُهُ قُدَّ مِنْ دُبُرٍ فَكَذَبَتْ وَهُوَ مِنَ الصَّادِقِينَ {27}

Na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma basi mke ni muongo na yeye Yusuf ni katika wakweli.

فَلَمَّا رَأَىٰ قَمِيصَهُ قُدَّ مِنْ دُبُرٍ قَالَ إِنَّهُ مِنْ كَيْدِكُنَّ ۖ إِنَّ كَيْدَكُنَّ عَظِيمٌ {28}

Basi mume alipoona kanzu imechanywa nyuma, alisema: Hii ni katika vitimbi vyenu (wanawake). Hakika vitimbi vyenu ni vikuu.

يُوسُفُ أَعْرِضْ عَنْ هَٰذَا ۚ وَاسْتَغْفِرِي لِذَنْبِكِ ۖ إِنَّكِ كُنْتِ مِنَ الْخَاطِئِينَ {29}

Yusuf! Achana nayo haya. Na wewe mwanamke omba msamaha kwa dhambi zako, hakika wewe ni miongoni mwa wakosaji.
  • 1. Sheikh Al-maraghi amenukuu ibara hii kwa herufi, lakini hakuashiria chimbuko lake au kuweka alama za nukuu. Amefanya hivi mara nyingi katika kauli za mwenye Al-Manar akimnukuu kwa kudhania kuwa yeye ndiye aliyesema na kumbe sheikh ana rai yake.