read

Aya 25-26: Ujumbe Wa Nuh

Maana

Aya mbili hizi zinaelezea kwa ufupi kwamba watu wa Nuh walikuwa wakiabudu masanamu. Inasemekana wao ndio wa kwanza kufanya shirki na kumfanyia Mwenyezi Mungu washirika.

Ndipo Mwenyezi Mungu akawapelekea mtume awape bishara na maonyo.

Basi Nabii Nuh (a.s.) akatekeleza risala yake kwa maneno haya mafupi: Mwabuduni Mwenyezi Mungu peke yake wala msimshirikishe na kitu.

Akadhihirisha hurumma yake kwao kwa kuwahofia kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu, kama wataendelea na shirk. Huu ndio msingi wa kwanza wa risala ya mitume wote.

فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ قَوْمِهِ مَا نَرَاكَ إِلَّا بَشَرًا مِثْلَنَا وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلَّا الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِيَ الرَّأْيِ وَمَا نَرَىٰ لَكُمْ عَلَيْنَا مِنْ فَضْلٍ بَلْ نَظُنُّكُمْ كَاذِبِينَ {27}

Wakasema wakuu wa wale waliokufuru katika kaumu yake: Hatukuoni ila ni mtu sawa na sisi. Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni, wala hatuwaoni kuwa mnayo ziada juu yetu; bali tunawaona kuwa mu waongo.

قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِنْ كُنْتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِنْ رَبِّي وَآتَانِي رَحْمَةً مِنْ عِنْدِهِ فَعُمِّيَتْ عَلَيْكُمْ أَنُلْزِمُكُمُوهَا وَأَنْتُمْ لَهَا كَارِهُونَ {28}

Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na amenipa rehema kutoka kwake, ikafichikana kwenu, Je, tuwalazimishe na hali nyinyi mnaichukia?

وَيَا قَوْمِ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مَالًا ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّهِ ۚ وَمَا أَنَا بِطَارِدِ الَّذِينَ آمَنُوا ۚ إِنَّهُمْ مُلَاقُو رَبِّهِمْ وَلَٰكِنِّي أَرَاكُمْ قَوْمًا تَجْهَلُونَ {29}

Na enyi watu wangu! Siwaombi mali kwa hili. Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu. Na mimi sitawafukuza wale walioamini, hakika wao watakutana na Mola wao. Lakini mimi nawaona nyinyi ni watu wajinga.

وَيَا قَوْمِ مَنْ يَنْصُرُنِي مِنَ اللَّهِ إِنْ طَرَدْتُهُمْ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ {30}

Na enyi watu wangu! Ni nani atakayenisaidia mbele za Mwenyezi Mungu nikiwafukuza? Basi je, hamfikiri?

وَلَا أَقُولُ لَكُمْ عِنْدِي خَزَائِنُ اللَّهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ إِنِّي مَلَكٌ وَلَا أَقُولُ لِلَّذِينَ تَزْدَرِي أَعْيُنُكُمْ لَنْ يُؤْتِيَهُمُ اللَّهُ خَيْرًا ۖ اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا فِي أَنْفُسِهِمْ ۖ إِنِّي إِذًا لَمِنَ الظَّالِمِينَ {31}

Wala siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi ninajua mambo ya ghaibu; wala sisemi kuwa mimi ni Malaika. Wala sisemi yale ambayo yanayadhuru macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nafsi zao. Hapo bila shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu.