read

Aya 27-31: Nuh Na Watu Wake

Wakasema wakuu wa wale waliokufuru katika kaumu yake, hatukuoni ilia ni mtu sawa na sisi.

Nuh alipowalingania watu wake kwenye tawhid walikataa mwito wake, kabla ya kuchunguza uhakika wake. Wakaleta sababu mbili: Ya kwanza, kwamba vipi watamfuata na hali yeye ni mmoja wao? Wao waliangalia msemaji, hawakuangalia yanayosemwa; wakapima haki na watu badala ya kuwapima watu na haki.

Unaweza kuuliza: Hili halihusiki na watu wa Nuh tu, tumewaona watu wengi wamewatukuza wageni kuliko wenyeji; na kuna usemi mashuhuri usemao: ‘msichana wa nyumbani ana sura mbaya,’ sasa kuna ubaya gani?

Jibu: ni kweli kwamba hayo hayahusiki na watu wa Nuh tu na wala Aya haipingi hilo; isipokuwa inawashutumu kwa jambo hilo na hii haiwabakishi watu wengine, wote wanashutumiwa.

Sababu ya pili waliyoisema wapinzaini ni:

Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni, wala hatuwaoni kuwa mnayo ziada juu yetu;

Yaani walimwambia Nuh na waumini kuwa vipi tuwafuate na nyinyi hamtuzidi na chochote kihali na kimali; sawa na walivyosema washirikina wa kiqurayash kumwambia Muhammad(s.a.w.):

لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ كَنْزٌ أَوْ {12}

“Mbona hakuteremshiwa hazina” (11:12).

Na wakasema tena:

لَوْلَا نُزِّلَ هَٰذَا الْقُرْآنُ عَلَىٰ رَجُلٍ مِنَ الْقَرْيَتَيْنِ عَظِيمٍ {31}

“Mbona hii Qur’ani haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili.” (43:31)

Bali tunawaona kuwa mu waongo, kwa vile nyinyi ni mafukara mlio maskini. Haya ndiyo matamshi ya wenye utajiri kung’ang’nia mali tu, lakini maneno ya kheri na matendo mema kwao ni maneno matupu yasiyokuwa na faida.

Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na amenipa rehema kutoka kwake.

Hili ni jawabu la kauli yao, kuwa vipi tukuamini na wewe ni kama sisi. Maana ya jawabu ni kuwa nifanye nini ikiwa Mwenyezi Mungu amenichagua kutekeleza ujumbe wake na amenihusu mimi na rehema yake? Tena akanipa ubainifu kutoka kwake wa risla hii.

Je, nikatae; nimwambie Mwenyezi Mungu sitaki kutumwa na wewe wala sitafikisha ujumbe wako kwa waja wako. Je, yote hayo niyakatae?

Kwa vile nyinyi hamna akili ndio ikafichikana kwenu risala na mmeshindwa kuifahamu.

Je, tuwalazimishe? Yaani tuwalazimishe na ujumbe wangu, na hali nyinyi mnaichukia?

Na enyi watu wangu! Siwaombi mali kwa hili la kuwaonya.

Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu mwenye kuzungumzia jina la Mwenyezi Mungu, akiwa ni mkweli katika maneno yake, basi hataki malipo kutoka kwa mwenginewe. Na wanaotafuta riziki kwa jina la dini ndio waombao watu mali na sadaka; na ndio wengi siku hizi.

Na mimi sitawafukuza wale walioamini, hakiaka wao watakutana na Mola wao.
Kwa nini niwafukuze? Kwani ufukara ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu anajua imani yao kwa vile wao wanamwelekea yeye.

Lakini mimi nawaona ni watu wajinga. Na watu ni maadui wa wasichokijua.

Na enyi watu wangu! Ni nani atakayenisaidia mbele za Mwenyezi Mungu nikiwafukuza?

Je, mnaweza nyinyi au wengine kunikinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Basi je, hamfikiri? Vipi atafikiri ambaye haogopi mwisho?

Wala siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi ninajua mambo ya ghaibu; wala sisemi kuwa ni Malaika.

Kauli hii ni ya Nuh (a.s.) ikiwa ni ufafanuzi na tafsiri ya kauli yake: “Hakika mimi kwenu ni muonyaji abainishaye” Si lazima muonyaji amiliki mali, ili fukara aonekane mwongo; wala si lazima ajue ghaibu, ili aonekane mwongo yule asiyejua ghaibu; wala pia si lazima awe Malaika ili asiyekuwa Malaika ambiwe wewe si lolote isipokuwa ni mtu.

Wala sisemi yale ambayo yanayadhuru macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nafsi zao.

Kuna mazoweya ya wenye mali kuona utajiri ndio kipimo cha haki na heri; bali hata wajinga na wapumbavu huona hivyo. Ama mbele ya Mwenyezi Mungu na watu wa Mwenyezi Mungu kipimo ni takua na amali njema na Nuh (a.s.) anapima kwa vipimo vya Mwenyezi Mungu. Vipi awaambie waumini kuwa hamtapata heri ya Mwenyezi Mungu; kama walivyoambiwa na mataghut? Ila ikiwa yeye naye ni taghuti kama wao.

Hapo bila shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu.

Kama wale waliomshirikisha Mwenyezi Mungu, wakavikataa vitabu vyake na mitume yake.

قَالُوا يَا نُوحُ قَدْ جَادَلْتَنَا فَأَكْثَرْتَ جِدَالَنَا فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِنْ كُنْتَ مِنَ الصَّادِقِينَ {32}

Wakasema: Ewe Nuh! Umejadiliana nasi na umezidisha kutujadili basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wakweli.

قَالَ إِنَّمَا يَأْتِيكُمْ بِهِ اللَّهُ إِنْ شَاءَ وَمَا أَنْتُمْ بِمُعْجِزِينَ {33}

Akasema: Mwenyezi Mungu atawaletea akipenda na wala nyinyi si wenye kumshinda.

وَلَا يَنْفَعُكُمْ نُصْحِي إِنْ أَرَدْتُ أَنْ أَنْصَحَ لَكُمْ إِنْ كَانَ اللَّهُ يُرِيدُ أَنْ يُغْوِيَكُمْ ۚ هُوَ رَبُّكُمْ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {34}

Wala nasaha yangu haitawafaa kitu nikitaka kuwapa nasaha ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kuwapoteza. Yeye ndiye Mola wenu; na kwake mtarejeshwa.

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ إِنِ افْتَرَيْتُهُ فَعَلَيَّ إِجْرَامِي وَأَنَا بَرِيءٌ مِمَّا تُجْرِمُونَ {35}

Au wanasema ameizua? Sema: ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na mimi sihusiki na makosa myatendayo.