read

Aya 30-35: Mke Wa Mheshimiwa Na Wanawake Wa Mjini

Lugha:

Kugubikwa ni kufunikwa kabisa, yaani moyo wake ulifunikwa.

Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa mheshimiwa anamtaka mtumishi wake pasipo kutamaniwa naye. Hakika amegubikwa na mapenzi. Sisi hakika tunamuona yuko katika upotevu uliodhahiri.

Ilienea habari mjini, hasa kwa wanawake kwamba mke wa mheshimiwa amesalitika kimapenzi na mtumishi wake na akamtaka, lakini akakataa. Hilo ni kosa lisilosamehewa.

Aliposikia vitimbi vyao.

Yaani maneno yao. Yameeitwa vitimbi kwa vile hawakukusudia njia ya haki, bali ni kule kuenea tu. Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa pengine walimlaumu kwa kumwambia wazi wazi mwanamume, na kwamba ilitakikana watumie mbinu. Kauli hii inaweza kufaa kwa Malaya sio kwa wanaojihesimu.

Aliwaita na akawawekea matakia, na akampa kila mmoja wao kisu.

Alitaka kuwafanyia vitimbi, kama wao walivyomfanyia. Kwa hiyo akawaandalia karamu ya kukata na shoka, akawekea mito laini na chakula chenye ladha na kila mmoja akampa kisu cha kukatia nyama. Kutumia visu wakati huo kunafahamisha kuwa walikuwa wameendelea. Katika Tafsir Attabariy anasema: Kazi ya kisu katika karamu ni ya kukatia kinacholiwa tu. Kwa hiyo kikitajwa kisu ndio kimetajwa kinacholiwa.

Akasema kumwambia Yusuf: Tokea mbele yao. Walipomuona wakaona ni kitu kikubwa na wakakata mikono yao kutokana na mshangao mkubwa.

Baadhi ya wafasiri wanasema maana ya kukata hapa ni kujijeruhi. Lakini dhahiri ya neno kukata ni kukata tu, na mfano wa matukio haya hufasiriwa vingine ikiwa iko haja ya kufanya hivyo kwa sababu ya mikanganyo na sio kwa nukuu iliyo wazi.

Na wakasema: Hasha lillahi Huyu si mtu, hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu.”

Alie katika umbo la binadamu, kutokana na haiba yake na uzuri, ambao ulimletea aina za balaa na mitihani.

Akasema yule bibi: Huyu ndiye mliyekua mkinilaumia.

Aliasema haya kwa uhuru ule wanaopigania wanawake wa sasa uhuru bila ya majukumu; hata katika kuvunja heshima na uharibifu. Sisi pia tunapigania uhuru wa wanaume na wanawake, lakini katika mipaka ya majukumu kikauli na kivitendo.

Hakika nilimtaka kinyume cha nafsi yake, lakini akakataa. Na akitofanya ninayomwamrisha basi hapana shaka atafungwa gerezani na atakuwa miongoni mwa madhalili.

Mwenye tafsir Al-Manar anasema: “Wallahi sistajabu kwa Yusuf kumkataa mwanamke aliyejileta mwenyewe; isipokuwa kustajabu kwangu ni mtazamo wake Yusuf kwa Mwenyezi Mungu haukuacha nafasi yoyote katika moyo wake wa kibinadamu wa kumwangalia mwanamke huyu aliyeshikwa na nyonda.” Nasi tunaongeza kwenye kauli hii kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amepiga mfano kwa Yusuf wa mumin mwenye ikhlasi ili ajulikane mumin aliye kombo kombo ambaye huipeleka dini vile atakavyo yeye.

Akasema: Ewe Mola wangu! Gereza linapendeza zaidi kwangu kuliko haya wanayoniitia.

Makusudio ya kupendeza hapa sio kuwa ni zuri, isipokuwa ni hiyari tu yaani afadhali. Amesema wanayoniitia, kwa tamko la wengi. Kwa sababu wanawake waliomuona pia walimtamani, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu katka Aya 50 ya sura hii: “Rejea kwa bwana wako na umuulize habari ya wale wanawake waliokata mikono yao. Hakika Mola wangu anajua vizurivitimbi vyao”. Yusuf alihiyari gereza pamoja na uchungu wake na kuacha ladha ili apate mwisho mtamu.

Unaweza kuuliza: Ikiwa mtu atahiyarishwa baina ya zina na kufungwa gerezani na hawezi kuepuka moja ya mawili hayo, je inaruhusiwa kuzini?

Hairuhusiwi. Kwa sababu hiyari hapo iko baina ya zina ambayo hiyo yenyewe ni haramu na kufungwa ambako ni haramu kwa dhalimu sio kwa mwenye kufungwa. Ila ikiwa kufungwa kutasababisha dhambi kubwa zaidi ya zina. Kwa hiyo mtu akihiyarishwa baina ya kuzini na kuua, basi atachagua kuzini. Lakini hiyo ni kwa asiyekuwa maasumu. Yeye an hukumu nyingine.

Na kama hutaniondolea vitimbi vyao nitawaelekea na nitakuwa miongoni mwa wajinga.

Vilipozidi vitisho na vivutio, Yusuf alihofia kudhoofika msimamo wake, kwa hiyo akamwelekea Mwenyezi Mungu akiomba kujinasua, huku akisema: Ewe Mola wangu! Yamenishukia nisiyoyaweza isipokuwa kwa msaada wako; na wewe ni muweza wa kuyaondoa. Na kama hutayaondoa nguvu zangu zitadhoofika na uwezo wangu utakuwa mchache.

Basi Mola wake akamwitikia na akamuondoshea vitimbi vyao; kama alivyomwondoshea vya ndugu zake hapo mwanzo. Mja yeyote hamfanyii ikhlasi Mwenyezi Mungu ila humjaalia matokeo na faraja.

وَكَانَ حَقًّا عَلَيْنَا نَصْرُ الْمُؤْمِنِينَ {47}

“Na ililkuwa ni haki juu yetu kuwanusuru wauminii.” (30:47).

Hakika yeye ni Msikizi, Mjuzi.

Anasikia dua ya mwenye kumnyenyekea na anajua ikhlasi ya mwenye kumfanyia ikhlas.

Kisha ikawadhihirikia baada ya kuona ishara ya kuwa wamfunge kwa muda.

Dhamir ya ikawadhihirikia inamrudia mheshimiwa na mkewe na wengineo waliokuwa na maoni kama yao. Imesemekana kuwa inamrudia yeye peke yake na tamko la wengi likafaa kwa vile halikutajwa jina lake.

Makusudio ya ishara ni dalili zinazonyesha usafi wa Yusuf na kutokuwa na hatia. Hatia yake ni usafi wake na kujichunga. Kama angelikuwa mhalifu kama wao wasingempa cheo kikubwa.

Yusuf alikataa matakwa yao kwa hiyo wakamwadhibu kama mwenye hatia. Hivi ndivyo ilivyo katika historia yoyote.

Mtu mzuri anapata tabu katika mazingira ya dhulma, lakini Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaomcha na wakavumilia misukosuko katika njia yake si katika njia yao. Na muovu anampa muda kisha mambo humgeukia.

Na Mwenyezi Mungu humpa nguvu kwa nusra yake mwenye kuamini na akawa na subira; sawa na yaliyomtokea Yusuf pamoja na ndugu zake na mke wa mheshimiwa, pale mwisho ndugu zake walipomwambia:

“Wallahi Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi na hakika sisi tulikuwa wenye makosa” Aya: 90. Na mke wa mheshimiwa aliposema: “Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliyemtaka kinyume cha nafsi yake na hakika yeye ni katika wakweli” Aya: 51

وَدَخَلَ مَعَهُ السِّجْنَ فَتَيَانِ ۖ قَالَ أَحَدُهُمَا إِنِّي أَرَانِي أَعْصِرُ خَمْرًا ۖ وَقَالَ الْآخَرُ إِنِّي أَرَانِي أَحْمِلُ فَوْقَ رَأْسِي خُبْزًا تَأْكُلُ الطَّيْرُ مِنْهُ ۖ نَبِّئْنَا بِتَأْوِيلِهِ ۖ إِنَّا نَرَاكَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ {36}

Na wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi nimeota nakamua mvinyo. Mwingine akasema: Hakika mimi nimeota nimebeba mkate juu ya kichwa changu na ndege wanaula hebu tuambie tafsiri yake. Kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.

قَالَ لَا يَأْتِيكُمَا طَعَامٌ تُرْزَقَانِهِ إِلَّا نَبَّأْتُكُمَا بِتَأْوِيلِهِ قَبْلَ أَنْ يَأْتِيَكُمَا ۚ ذَٰلِكُمَا مِمَّا عَلَّمَنِي رَبِّي ۚ إِنِّي تَرَكْتُ مِلَّةَ قَوْمٍ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَهُمْ بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ {37}

Akasema: Hakitawafikia chakula mtakachopewa ila nitawaambia hakika yake kabla hakijawafikia. Haya ni katika aliyonifundisha Mola wangu. Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasiomwamini Mwenyezi Mungu na wao wanaikanusha siku ya mwisho.

وَاتَّبَعْتُ مِلَّةَ آبَائِي إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ ۚ مَا كَانَ لَنَا أَنْ نُشْرِكَ بِاللَّهِ مِنْ شَيْءٍ ۚ ذَٰلِكَ مِنْ فَضْلِ اللَّهِ عَلَيْنَا وَعَلَى النَّاسِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ {38}

Na nikafuata mila ya baba zangu Ibrahim na Is-haq na Ya’qub. Haitufalii sisi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote. Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu na juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru.