read

Aya 32-35: Ewe Nuh Umezidisha Majadiliano Nasi

Wakasema: Ewe Nuh! Umejadiliana nasi na umezidishi kutujadili basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wakweli.

Nuh (a.s.) alipowaziba mdomo watu wake kwa hoja na dalili, walipata dhiki na wakawa hawana pa kutokea, basi wakaona njia pekee, iliyobaki, ya upinzani ni kuomba adhabu.

Walipoiomba, Akasema: Mwenyezi Mungu atawaletea akipenda na wala nyinyi si wenye kumshinda.

Washirikina wa Makka walimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu, kama walivyosema watu wa Nuh. Tazama Juz.9 (8:32).

Wala nasaha yangu haitawafaa kitu nikitaka kuwapa nasaha .

Mwenyezi Mungu alitaka kuwanasihi bali alikithirisha kuwanasihi, lakini kuna faida gani ikiwa nyoyo zimesusuwaa na wala hazipondokei kwenye uongofu, ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kuwapoteza.

Mwenyezi Mungu haumbi upotevu kwa mtu. Lau ingelikuwa hivyo basi angekuwa ameuondoa utu wake. Lakini desturi ya Mwenyezi Mungu, katika maumbile yake, imepitisha kuwa mwenye kufuata, njia ya upotevu, kwa matakwa yake, atakuwa katika wapotevu tu. Sawa na na aliyejinyonga kwa hiyari yake.

Ni kwa maana hii ndio ikafaa kunasibishwa upotevu kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Yametangulia maelezo katika Juz.11 (10:78) kifungu cha ‘uongofu na upotevu’

Yeye ndiye Mola wenu; na kwake mtarejeshwa

Wala hakuna kuhepa kukutana naye, hisabu yake na malipo yake.

Au wanasema ameizua? Sema: ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na mimi sihusiki na makosa myatendayo.

Dhahiri ya mfumo wa maneno inafahamisha kuwa dhamiri katika ‘wanasema’ inawarudia watu wa Nuh na uliozuliwa ni wahyi; kwa maana ya kuwa: Sema ewe Nuh kuwaambia watu wako: Ikiwa mimi ni mwongo wa ninayoyasema, kama mnavyodai, basi mimi peke yangu ndiye nitakayebeba majukumu na dhambi ni zangu na adhabu. Na ikiwa ninasema kweli, basi nyinyi ndio wenye majukumu, na adhabu ya kukadhibisha itawashukia peke yenu.

Insemekana kuwa Aya ii ni jumla ya maneno iliyoingia kati, katika kisa cha Nuh; na kwamba ilishuka kwa washirikina wa kiquraish, kwa sababu walimtilia shaka Muhammad (s.a.w.) katika kuwaelezea kisa hiki. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha awaambie: Sio lawama lenu uzushi wangu, ni langu mimi peke yangu. Maana haya yenyewe yanafaa, lakini yako mbali na dhahiri ya maneno.

وَأُوحِيَ إِلَىٰ نُوحٍ أَنَّهُ لَنْ يُؤْمِنَ مِنْ قَوْمِكَ إِلَّا مَنْ قَدْ آمَنَ فَلَا تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ {36}

Akaletewa wahyi Nuh kuwa hataamini katika watu wako isipokuwa yule aliyekwishaamini. Basi usisikitike kwa waliyokuwa wakiyatenda.

وَاصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا ۚ إِنَّهُمْ مُغْرَقُونَ {37}

Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa wahyi wetu wala usinizungumzie kuhusu wale waliodhulumu, hakika wao watagharikishwa.

وَيَصْنَعُ الْفُلْكَ وَكُلَّمَا مَرَّ عَلَيْهِ مَلَأٌ مِنْ قَوْمِهِ سَخِرُوا مِنْهُ ۚ قَالَ إِنْ تَسْخَرُوا مِنَّا فَإِنَّا نَسْخَرُ مِنْكُمْ كَمَا تَسْخَرُونَ {38}

Na akawa anaunda jahazi na kila wakimpita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli, hakika nasi tutawakejeli, kama mnavyotukejeli.

فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ مَنْ يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَيَحِلُّ عَلَيْهِ عَذَابٌ مُقِيمٌ {39}

Mtakuja jua ni nani itakayemfikia adhabu ya kumfedhehesha na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu.