read

Aya 36-38: Gerezani Pamoja Na Vijana Wawili

Na wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi nimeota nakamua mvinyo. Mwingine akasema: Hakika mimi nimeota nimebeba mkate juu ya kichwa changu na ndege wanaila.

Yusuf mtwaharifu aliingia gerezani na mke mchafu wa mheshimiwa akabaki kwenye jumba akiwa huru, anaamrisha na kukataza. Lakini Yusuf aliingia gerezani huku moyo umemtua akiwa na raha ya dhamiri, kuokoka na maasi na kufuzu kupata radhi ya Mwenyezi Mungu. Na mke wa mheshimiwa alikuwa katika gereza la adhabu iumizayo, adhabu ya dhamiri, fedheha na kukosa raha ya moyo.

Miongoni mwa walioingia gerezani pamoja na Yusuf ni vijana wawili kati- ka wafanyakazi wa mfalme: Anayehusika na vinywaji na mtunza vyakula kutokana na tuhumma walizobandikiwa. Yule wa vinywaji akasema nimeota ninakamua mvinyo. Na wa vyakula akasema ameota kichwani kwake kuna mkate unaoliwa na ndege na kwenda nao. Wakasema:

Hebu tuambie tafsir yake. Kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wema. katika sera yako.

Akasema: Hakitawafikia chakula mtakachopewa ila nitawaambia hakika yake kabla hakijawafikia.

Kuna karibu kauli sita zilizosemwa kuhusu tafsri ya Aya hii. Iliyokaribu zaidi ni ile isemayo kuwa Yusuf aliwaambia mimi na nyinyi tumezuiliwa hapa, hakuna hata mmoja anayejua kinachoendelea nje, lakini pamoja na hayo nitawaambia chakula mtakacholetewa, ni cha aina gani na lengo la kuletwa kwake.
Unaweza kuuliza: Yeye aliulizwa kuhusu ndoto naye anajibu mambo ya vyakula, kuna uhusiano gani? Ndio ni kweli kuwa hii si ibara ya ndoto, lakini ni utangulizi. Yusuf alitaka kuitumia nafasi hii ili kuwathibitishia wafungwa wenzake kwamba yeye ni Nabii aliyetumwa na Mwenyezi Mungu.

Akatoa dalili ya utume wake kwa kutolea habari mambo yaliyofichikana; sawa na alivyotoa dalili Nabii Issa (a.s.).

وَأُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ وَأُحْيِي الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِ اللَّهِ ۖ وَأُنَبِّئُكُمْ بِمَا تَأْكُلُونَ وَمَا تَدَّخِرُونَ فِي بُيُوتِكُمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ {49}

“Na niwaambie mnavyo vila na mtakavyoweka akiba. Hakika katika haya ipo ishara kwenu mkiwa ni wenye kuamini.” Juz.3 (3:49)

Kimsingi hasa, lengo la kwanza la Yusuf ni kuwaeleza wafungwa itikadi ya tawhid (umoja wa Mungu) na kuikubali siku ya mwisho; kama ilivyo kawaida ya mitume. Hilo linadhirika katika kauli yake:

Haya ni katika aliyonifundisha Mola wangu.

Yaani haya ya kuwaambia mambo yaliyofichikana sio ukuhani wala uchawi au utabiri; isipokuwa ni wahyi wa Mwenyezi Mungu alioniletea; kama alivyowa pelekea mitume katika mababa zangu.

Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasiomwamini Mwenyezi Mungu na wao wanaikanusha siku ya mwisho.

Hii ni kupinga itikadi yao kwa upole, ili mafundisho yake yaingie nyoyoni mwao. Imeelezwa katika historia kwamba Wamisri wakati huo walikuwa wakiaabudu miungu, likiwemo jua na walikuwa wakiita ra na ndama wao (ibis).

Na nikafuata mila ya baba zangu Ibrahim na Is-haq na Yaqub. Haitufalii sisi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote.

Majina ya wote hao yalikuwa maarufu kwa wote; hasa Ibrahim kipenzi (a.s.), ndio maana Yusuf akajinasibisha kwao kinasabu na dini.

Razi anasema: Yusuf alipodai utume na kuonyesha muujiza, wa kujua ghaibu, aliunganisha na kuwa yeye ni katika watu wa nyumba ya utume na kwamba mababa zake na mababu zake walikuwa mitume. Kwani mtu anapodai kuwa na kazi ya baba yake, basi haiwi uzito kuaminiwa nayo.

Vile vie daraja ya Ibrahim, ish-aq, na Ya’qub ilikuwa maarufu mbele za watu. ikibainika kuwa yeye ni katika watoto wao, basi wanamuadhimisha. Na kuathirika zaidi na maneno yake katika nyoyo zao.

Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu na juu ya watu.

Yaani kuhusika kwetu na utume ni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutuona kua tunafaa. Vile vile ni fadhila kwa watu kwa vile wao wameongoka kwa sababu yetu sisi.

Lakini watu wengi hawashukuru.

Bali wanaendelea kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kumkana. Na kila wanavyozidi utajiri ndivyo wanavyozidi ukafiri na utaghuti.

يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَأَرْبَابٌ مُتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ {39}

Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, waungu wengi wanaofarikiana ni bora au Mwenyezi Mungu mmoja mwenye nguvu?

مَا تَعْبُدُونَ مِنْ دُونِهِ إِلَّا أَسْمَاءً سَمَّيْتُمُوهَا أَنْتُمْ وَآبَاؤُكُمْ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ بِهَا مِنْ سُلْطَانٍ ۚ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّهِ ۚ أَمَرَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {40}

Hamuabudu badala yake ila majina matupu mliyoyapanga wenyewe na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote. Hapana hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu tu. Ameamrisha msimwabudu yoyote isipokuwa yeye tu. Hiyo ndiyo dini iliyonyooka, lakini watu wengi hawajui.