read

Aya 36-39: Akaletewa Wahyi Nuhu

Maana

Akaletewa wahyi Nuh kuwa hataamini katika watu wako isipokuwa yule aliyekwi shaamini. Basi usisikitike kwa waliyokuwa wakiyatenda.

Mwenyezi Mungu alimpa habari Nuh kwamba kazi yake imekwisha, baada ya kutekeleza ujumbe kwa njia sahihi na kumpa hoja kila mpinzani; na kwamba hakuna yeyote atakayemwitikia baada ya sasa.

Mwenyezi Mungu alimpoza Nuh, kwani alikuwa anaungulika na kuwa na kuwa na huzuni, kwa sababu ya watu wake kuendelea na ushirikina.

Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa wahyi wetu wala usinizungumzie kuhusu wale waliodhulumu, hakika wao watazamishwa.

Mbele ya macho yetu ni fumbo la kuhifadhi kwake na kuchunga kwake Mwenyezi Mungu. Na makusudio ya wahyi wetu ni amri na maelekezo yake. Baada ya Mwenyezi Mungu kumwamrisha kuunda jahazi, alimkataza kutawasali naye kuhusu wale waliojidhulumu, kwa sababu neno la adhabu limekwisha wathibitikia wote.

Na akawa anaunda jahazi na kila wakimpita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli kwa vile anaitengeza kwenye nchi kavu mbali na maji. Walimkejeli na kumcheka kwa vile walikuwa na yakini kuwa hakuna chochote zaidi ya wanavyoona. Hivi ndivyo alivyo mjinga anategemea mambo ya nje tu wala hafikirii vizuri au kuzingatia.

Inasemekana kuwa watu wa Nuh walikuwa hawajui jahazi wala manufaa yake; ndio wakamkejeli na kustaajabu. Lakini ni maarufu kuwa Wafoeniki ndio watu wa mwanzo mwanzo kuunda majahazi.

Abu Hayyan Al-andalusiy, katika tafsir yake, Albahrul muhit, akimnukuu Ibn Abbas, anasema kuwa Nuh alikata mbao za kutengenezea Safina, kutoka katika msitu wa milima ya Lebanon. Hili linafahamisha kwamba, misitu ya mili- ma ya Lebanon, ilikuwa maarufu tangu zamani na kwamba Wafoniki walikuwa wakikata mbao za majahazi yao kwenye msitu huo.

Waumini Na Wenye Kejeli

Akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli, hakika nasi tutawakejeli, kama mnavyotukejeli. Nanyi mtakuja jua ni nani itakayemfikia adhabu ya kumfedhehesha na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu.

Hawakujua hakika ya jahazi (Safina) na lengo lake, hawakujua siku zimeficha majanga gani. Hilo likawapelekea dharau na kejeli. Lakini Nuh alikuwa na hakika na alifanyalo, kwamba yeye anafanya kwa uangalizi, kuwa ataokoka yeye na walio pamoja naye na kwamba mwisho wa wenye kejeli ni gharka tu.

Vijana wetu wa leo wanafanana sana na wale waliokufuru katika watu wa Nuh. Wale walikejeli Safina ya Nuh na hawa wanawakejli waumini, wakisema: Mpaka sasa, karne ya ishirini, bado watu wanaswali na kufunga tu; sawa na walivyosema wale makafiri: Jahazi kwenye nchi kavu kusiko na bahari wala maji? Hawakujua siri na hakika ya Safina, wakamkejeli Nuh. Na vijana wa leo hawajui siri ya saum na swala, ndio wanawadharau wafungaji na waswaliina. Je, vijana wanaokejeli dini, watasalimika kupatwa na yaliyowapata watu wa Nuh na Safina yake?

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ قُلْنَا احْمِلْ فِيهَا مِنْ كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَنْ سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ وَمَنْ آمَنَ ۚ وَمَا آمَنَ مَعَهُ إِلَّا قَلِيلٌ {40}

Hata ilipokuja amri yetu na ikafurika tanuri, tulisema: Pakia humo wawili wawili, dume na jike kutoka kila aina. Na watu wako wa nyumbani isipokuwa yule ambaye limempitia neno na walioamini. Na hawakuamini pamoja naye isipokuwa wachache tu.

وَقَالَ ارْكَبُوا فِيهَا بِسْمِ اللَّهِ مَجْرَاهَا وَمُرْسَاهَا ۚ إِنَّ رَبِّي لَغَفُورٌ رَحِيمٌ {41}

Na pandeni humo kwa Jina la Mwenyezi Mungu (Bismillah) kuwa ndio kwenda kwake na kuthibiti kwake. Hakika Mola wangu ni mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.

وَهِيَ تَجْرِي بِهِمْ فِي مَوْجٍ كَالْجِبَالِ وَنَادَىٰ نُوحٌ ابْنَهُ وَكَانَ فِي مَعْزِلٍ يَا بُنَيَّ ارْكَبْ مَعَنَا وَلَا تَكُنْ مَعَ الْكَافِرِينَ {42}

Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuh akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi wala usiwe pamoja na makafiri.

قَالَ سَآوِي إِلَىٰ جَبَلٍ يَعْصِمُنِي مِنَ الْمَاءِ ۚ قَالَ لَا عَاصِمَ الْيَوْمَ مِنْ أَمْرِ اللَّهِ إِلَّا مَنْ رَحِمَ ۚ وَحَالَ بَيْنَهُمَا الْمَوْجُ فَكَانَ مِنَ الْمُغْرَقِينَ {43}

Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. Akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu. Na wimbi likaingia kati yao akawa miongoni mwa waliogharikishwa.

وَقِيلَ يَا أَرْضُ ابْلَعِي مَاءَكِ وَيَا سَمَاءُ أَقْلِعِي وَغِيضَ الْمَاءُ وَقُضِيَ الْأَمْرُ وَاسْتَوَتْ عَلَى الْجُودِيِّ ۖ وَقِيلَ بُعْدًا لِلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ {44}

Na ikasemwa: Ewe ardhi! meza maji yako na ewe mbingu! Jizuie. Na maji yakadidimia chini na amri ikapitishwa, na Jahazi ikasimama juu ya Judi. Na ikasemwa: wapotelee mbali watu madhalimu!