read

Aya 39-40: Enyi Wafungwa Wenzangu

Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, waungu wengi wanaofarikiana ni bora au Mwenyezi Mungu mmoja mwenye nguvu?

Wafungwa wawili ni wale vijana wawili walioingia gerezani pamoja na Yusuf. Alijadiliana kuhusu wanaowaaabudu, ameleta majadala na hoja katika njia ya swali, kwa sababu hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuiponda itikadi mbovu. Tumezungumzia kuhusu dalili ya Tawhid katika Juz.5 (4: 48)

Kisha Yusuf akapiga hatua ya pili katika kuelezea Tawhid na kuitupilia mbali shirk kwa kusema:

Hamuabudu badala yake ila majina matupu mliyoyapanga wenyewe na baba zenu. Mwenyezi hakuyateremshia dalili yoyote.

Nyinyi mnaabudu majina tu yasiyokuwa na maana yoyote, yaani hawako hao mnaowataja. Na kila kisichokuwapo hakina athari yoyote na ni muhali kuwasimishia dalili. Kwa hiyo mnaowaabudu ni wa kuwazia tu. Hivi ndivyo anavyofanya Mjuzi mwenye hekima. Hutumia mifumo mbalimbali kumkinaisha mjinga. Anaonyesha na kusema mpaka afikie kwenye lengo.

Hapana Hukumu Ispokuwa Ya Mwenyezi Mungu

Hapana hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu tu. Ameamrisha msimwabudu yoyote isipokuwa yeye tu.

Maana ya msimwabudu ila yeye tu, iko wazi. Ama maana ya kuwa hukumu ni ya Mwenyezi Mungu, inahitaji tafsir. Kwa ufupi ni kuwa hukumu ya Mwenyezi Mungu iko mafungu mawili:

Kwanza, ni kupitisha kwake na makadirio yake ( kadha na kadar). Hii haiepukiki kwa binadamu.

Pili, ni halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake inayoitwa hukumu ya sharia. Inajulikana kwamba Mwenyezi Mungu hawasiliani na waja wake moja kwa moja katika maisha haya; isipokuwa anaweka sharia na kuzifikisha kupitia kwa mitume yake.

Haya ndiyo makusudio ya kuwa hukumu ni ya Mwenyezi Mungu. Kwamba yeye ndio chimbuko la sharia sio mtu mmoja wala vikundi; hakuna mwenye kuhalalisha au kuharamisha isipokuwa yeye tu.Yeyote mwenye kuhukumu hukumu yake haiwezi kuwa ya haki na uadilifu isipokuwa kama itaafikiana na aliyoyaleta Mwenyezi Mungu:

وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ {45}

“Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu.”
Juz.6 (5: 45).

Aya nyingine inasema hao ndio mafasiki na nyingine inasema hao ndio makafiri.

Kwa hiyo hukumu yoyote isiyofuata matakwa na radhi za Mwenyezi Mungu, basi ni ukafiri, dhula na ufasiki.

Tafsir hii tumeitoa kutokana na kauli ya Imam Ali (a.s.) aliposikia kauli ya makhawarij waliposema: Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu, alisema: “Ni neno la haki liliokusudiwa batili, ndio! Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu, lakini hawa wanasema hakuna mamlaka ila ya Mwenyezi Mungu. Na ilivyo hasa hakuna budi aweko mwenye mamlaka aliye mwema, au muovu ambaye mamlaka yake yanatumiwa na mumin na anafurahika nayo kafiri.”

Yaani haki ya kuweka sharia ni ya Mwenyezi Mungu peke yake na nijuu ya watu kufuata aliyoyawekea sharia, na anayewachukua kwenye hilo ni mwenye mamlaka. Na makhawarij wamechanganya baina ya chimbuko la sharia na yule anayeifuata na anayeipotosha. Hawakutofautisha baina ya hawa wawili.

Hiyo ndiyo dini iliyonyooka, lakini watu wengi hawajui.

Hiyo ni ishara ya kudhibiti sharia na ibada kwa Mwenyezi Mungu tu. Maana ni kuwa dini yenye kunyooka ambayo haiko kombo kombo ni lile inayomuhusu Mwenyezi Mungu peke yake katika kuweka sharia na ibada. Binadamu yeyote haimfai kuwafanya watu wamwabudu au awawekee sharia ya hukumu, halali na haramu. Wote, hata mitume, ni waja wa Mwenyezi Mungu, wanafanya kulingana na amri yake na makatazo yake.

Maana ya yote haya ni kuwa watu wote ni ndugu waliosawa. Muumba wao amewapa haki ya ubinadamu ya milele, isiyokubali mabadilko wala marekebisho. Haki hizi zimedhihirisha maisha, uhuru na wema. Mwenye kuizuwiya haki basi huyo ni adui mkubwa wa Mwenyezi Mungu, dini yake na sharia yake.

يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَمَّا أَحَدُكُمَا فَيَسْقِي رَبَّهُ خَمْرًا ۖ وَأَمَّا الْآخَرُ فَيُصْلَبُ فَتَأْكُلُ الطَّيْرُ مِنْ رَأْسِهِ ۚ قُضِيَ الْأَمْرُ الَّذِي فِيهِ تَسْتَفْتِيَانِ {41}

Enyi wafungwa wenzangu wawili! Ama mmoja wenu atamnywesha bwana wake mvinyo. Na ama mwingine atasulubiwa na ndege watamla kichwa chake. Imekwisha katwa hukumu ya hilo jambo mlilokuwa mkiuliza.

وَقَالَ لِلَّذِي ظَنَّ أَنَّهُ نَاجٍ مِنْهُمَا اذْكُرْنِي عِنْدَ رَبِّكَ فَأَنْسَاهُ الشَّيْطَانُ ذِكْرَ رَبِّهِ فَلَبِثَ فِي السِّجْنِ بِضْعَ سِنِينَ {42}

Na akamwambia yule aliyemdhania kuwa ataokoka katika wawili hao: Unikumbuke mbele ya bwana wako. Lakini shetani akamsahaulisha kumtaja kwa bwana wake. Basi (Yusuf) akakaa gerezani miaka kadhaa.