read

Aya 4-6: Nyota Kumi Na Mbili

Maana

Yusuf alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja na jua na mwezi nimeota zikinisujudia.

Yusuf ni mtoto wa Ya’qub mtoto wa Is-haq mtoto wa Ibrahim Khalil (a.s.). Ya’qub ndiye Israil. Maana ya Israil, wakati huo, ilikuwa ni Abdullah (Mtumishi wa Mwenyezi Mungu), lakini wakati huu ni mtumishi wa ukoloni na jeshi lake.

Siku moja Yusuf aliota ndoto aliyomsimulia baba yake Ya’qub. Nayo ni kwamba yeye aliona usingizini nyota kumi na moja na jua na mwezi zikimsujudia. Hapo baba yake akajua kuwa ndoto hii ni ya kweli, akapata bishara ya mustakbali wa mwanawe.

Kuna tafsiri zisemazo kuwa umri wa Yusuf wakati huo ulikuwa ni miaka saba; wala hatujui rejea sahii za kipimo hiki. Lakini ukweli ni kuwa yeye, wakati huo, alikuwa ni kijana mwenye haiba na mwenye sura nzuri, akipigiwa mfano kwa uzuri wake; kama itakavyobainika katika masimulizi ya kisa.

Nyota kumi na moja ni ndugu zake na jua na mwezi ni baba na mama yake. Hayo yanafahamika kutokana na kauli yake itakayokuja mbele kwenye Aya 100: “Hii ndiyo tafsir ya ile ndoto yangu” Ufafanuzi unafuatia.

Akasema ewe mwanagu! Usiwasimulie ndugu zako ndoto yako wasije wakakufanyia vitimbi. Hakika Shetani ni adui aliye dhahiri kwa mtu.

Baba yake alihofia ndugu zake wakisikia aliyomsimulia na wakafahamu alivyofahamu yeye wasije wakadhihirisha chuki yao kwake na wasighilibiwe na Shetani kwa kumfanyia vitimbi vya kumwangamiza. Kwa vile alijua wivu wao kwake kutokana na kumpenda sana na kutukuza kwake. Kwa hiyo akamnasihi asiwasimule ndoto yake. Tutaizungumzia ndoto mahali pake, inshaallah.

Na kadhalika Mola wako atakuteua na atakufundisha tafsiri ya mambo.

Kukuteua ni kukuchagua wewe si mwingine na kukujaza aina za karama. Imesemekana makusudio ya kutafsiri mambo ni kutafsiri ndoto, kwa vile Yusuf alikuwa na kiwango cha juu cha kutafsiri ndoto, lakini dhahiri ya neno inaenea zaidi ya hivyo. Linalonasibiana na utume wa Yusuf ni kuwa tafsri ya mambo ni fumbo la kujua hakika ya mambo na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atamfundisha ambayo hakuwa akiyajua.

Na atatimiza neema yake juu yako na juu ya ukoo wa Ya’qub; kama alivyowatimizia hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq.

Nema za Mwenyezi Mungu hazihisabiki na ukamilifu wake ni unabii na utume. Na amewaneemesha nao Ibrahim babu wa Ya’qub na Is-haq babu wa Yusuf na Ya’qub mwenyewe. Pia na atamneemesha nao Yusuf baada ya ndoto hii na wengineo katika wajukuu wa Ya’qub.

Hakika Mola wako ni Mjuzi Mwenye hekima.

Anamjua anayemchagua na kumteua kwa ujumbe na ana hekima katika uteuzi huo na katika mambo yote.

لَقَدْ كَانَ فِي يُوسُفَ وَإِخْوَتِهِ آيَاتٌ لِلسَّائِلِينَ {7}

Kwa hakika katika Yusuf na ndugu zake kuna ishara kwa wanaouliza.

إِذْ قَالُوا لَيُوسُفُ وَأَخُوهُ أَحَبُّ إِلَىٰ أَبِينَا مِنَّا وَنَحْنُ عُصْبَةٌ إِنَّ أَبَانَا لَفِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {8}

Waliposema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi na hali sisi ni kikundi imara. Hakika baba yetu yumo katika upotevu dhahiri.

اقْتُلُوا يُوسُفَ أَوِ اطْرَحُوهُ أَرْضًا يَخْلُ لَكُمْ وَجْهُ أَبِيكُمْ وَتَكُونُوا مِنْ بَعْدِهِ قَوْمًا صَالِحِينَ {9}

Muuweni Yusuf au mtupeni nchi ya mbali, uso wa baba yenu utawaelekea nyinyi. Na baada ya haya mtakuwa ni watu wema.

قَالَ قَائِلٌ مِنْهُمْ لَا تَقْتُلُوا يُوسُفَ وَأَلْقُوهُ فِي غَيَابَتِ الْجُبِّ يَلْتَقِطْهُ بَعْضُ السَّيَّارَةِ إِنْ كُنْتُمْ فَاعِلِينَ {10}

Akasema msemaji kati yao: Msimuue Yusuf, lakini mtumbukizeni ndani ya kisima, watamuokota baadhi ya wasafiri, ikiwa nyinyi ni wenye kufanya.

قَالُوا يَا أَبَانَا مَا لَكَ لَا تَأْمَنَّا عَلَىٰ يُوسُفَ وَإِنَّا لَهُ لَنَاصِحُونَ {11}

Wakasema: Ewe baba yetu! Mbona hutuamini kwa Yusuf na hakika sisi ni wenye kumnasihi.

أَرْسِلْهُ مَعَنَا غَدًا يَرْتَعْ وَيَلْعَبْ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ {12}

Mpeleke kesho pamoja nasi afaidi na acheze, na bila shaka sisi tutamhifadhi.

قَالَ إِنِّي لَيَحْزُنُنِي أَنْ تَذْهَبُوا بِهِ وَأَخَافُ أَنْ يَأْكُلَهُ الذِّئْبُ وَأَنْتُمْ عَنْهُ غَافِلُونَ {13}

Akasema: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na ninahofia asije mbwa mwitu akamla nanyi mmeghafilika naye.

قَالُوا لَئِنْ أَكَلَهُ الذِّئْبُ وَنَحْنُ عُصْبَةٌ إِنَّا إِذًا لَخَاسِرُونَ {14}

Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na sisi ni kundi imara, basi hakika sisi tutakuwa kwenye hasara.”

فَلَمَّا ذَهَبُوا بِهِ وَأَجْمَعُوا أَنْ يَجْعَلُوهُ فِي غَيَابَتِ الْجُبِّ ۚ وَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ لَتُنَبِّئَنَّهُمْ بِأَمْرِهِمْ هَٰذَا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ {15}

Basi walipokwenda naye na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima. Na tukampa wahyi bila shaka utakuja waambia jambo lao hili na hali hawatambui.