read

Aya 40-44: Mafuriko

Lugha

Neno tannur (tanuri) katika lugha ya kiarabu lina maana nyingi; miongoni mwazo ni ardhi, na ndiyo iliyokusudiwa hapa.

Maana

Hata ilipokuja amri yetu na ikafurika tanuri.

Maana ni kuwa, ilipokuja amri ya Mwenyezi Mungu na maji yakawa yanabubujika kutoka ardhini

Tulisema: Pakia humo wawili wawili, dume na jike kutoka kila aina.

Neno kila linategemea kile kinachoelzewa. Kwa mfano katika kaule yake Mwenyezi Mungu: Nichake kila kitu, inamaanisha kuwa vitu vyote ni vyake. Na kauli yake kuhusu Bilqis:

وَأُوتِيَتْ مِنْ كُلِّ شَيْءٍ{23}

Na amepewa kila kitu, (27:23),

Inahusu vitu vya wakati wake au mji wake. Kwa hiyo basi maana ya kila aina katika Aya hii tuliyonayo ni kiasi kile atakachoweza kukichukua Nuh (a.s.). Katika Safina (jahazi ) miongoni mwa viumbe na wala sio aina yote ya viumbe.
Vinginevyo ingelibidi urefu na upana wa Safina uwe mamia ya maili.

Na watu wako wa nyumbani isipokuwa yule ambaye limempitia neno.

Yaani pakia ndani ya Safina watu wa nyumbani isipokuwa wale ambao tumekukataza kuwachukua.

Wafasiri wanasema kuwa watoto wa Nuh aliowachukuwa ni: Ham, Sam na Yafith. Ama yule ambaye aliandikiwa kuangamia katika watu wake wa nyumbani ni mmoja wa watoto wake ambaye Mwenyezi Mungu amemwashiria kwa kusema: Akawa katika waliozama ambaye inasemekana jina lake ni Kanani.

Mke wa Nuh pia alikuwa ni miongoni mwa waliozama, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:

ضَرَبَ اللَّهُ مَثَلًا لِلَّذِينَ كَفَرُوا امْرَأَتَ نُوحٍ وَامْرَأَتَ لُوطٍ ۖ {10}

“Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa waliokufuru kwa mke wa Nuh na mke wa Lut” (66:10).

Na walioamini; na hawakuamini pamoja naye isipokuwa wachache tu.

Yaani chukua kikundi kidogo cha watu walioamini pamoja nawe.

Na pandeni humo kwa Jina la Mwenyezi Mungu (Bismillah) kuwa ndio kwenda kwake na kuthibiti kwake

Nuh alifuata amri ya Mwenyezi Mungu, akwaita wauminii katika watu wake wa nyumbani na swahaba zake wapande Safina; na yeye pamoja na waliokuwa naye wasome Bismillah katika kwenda na kutua.

Nimeona baadhi ya tafsir za kisufi wakisema kuwa makusudio ya Safina hapa ni sharia na makusudio ya mawimbi ni hawa za nafsi na matamanio yake. Nikawa najiulza: wametoa wapi masheikh hawa tafsir ya kukiita Kitabu cha Mwenyezi Mungu na ujumbe wake kuwa ni Safina?

Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima.

Katika hali hii, inayofanana na kukata roho, Nuh alimwangalia mwanawe kwa masikitiko akimpa mwito wa kumwamini Mungu na kuokoka, kabla ya kuvuta pumzi za mwisho.

Na Nuh akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi wala usiwe pamoja na makafiri.

Maskini! Hurumma za mzazi, mwanawe akiguswa na shida yoyote naye inamgusa moyoni mwake na rohoni mwake. Nuh alikuwa na uhakika kuwa mwanawe ataangamia ikiwa atang’ang’ania kumshirikisha Mwenyezi Mungu, hivyo akamtaka amwamini Mwenyezi Mungu na apande Safina pamoja nao, lakini hakuna kuokoka kwa mwenye inadi. Upuuzaji wa ujana ukampofusha kujua mwisho mbaya, akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji.

Ujinga na ghururi ulimpa picha kuwa tatizo ni maji tu na kwamba ataweza kulitatua tatizo hilo kwa kupanda mlimani; hakujua kwamba hayo ni matakwa ya Mwenyezi Mungu na hasira zake kwa washirikina.

Akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu

Nuh akamjibu kuwa tatizo sio maji; isipokuwa ni matakwa ya Mwenyezi Mungu ambayo hayana kimbilio. Atakayeokoka ni yule aliyerehemiwa na Mwenyezi Mungu na atakyeangamia ni yule aliyekasirikiwa na Mwenyezi Mungu.

Na wimbi likaingia kati yao akawa miongoni mwa waliogharikishwa.
Wimbi lilikuja katikati ya mazungumzo ya mzazi na mwanawe. Yaliyomfika Nuh(a.s.) na mwanawe yanawafika wazazi wengi na watoto wao wanaojifanya wajuaji; kisha mwisho wao unakuwa kama wa mtoto wa Nuh.

Na ikasemwa: Ewe ardhi! meza maji yako na ewe mbingu! Jizuie. Na maji yakadidimia chini na amri ikapitishwa, na Jahazi ikasimama juu ya Judi.

Mwenyezi Mungu aliamrisha ardhi imeze maji na akaamrisha mbingu isimamiishe kumimina na mambo yakaishia kwa kuokoka waumini na kuangamia washirikina. Safina nayo ikatua Judiy mlima uloko Muosal, Lebanon; kama inavyosemekana.

Na ikasemwa: wapotelee mbali watu madhalimu!

Ambao wameikad- hibisha haki. Neno ‘potolea mbali’ ni dua ya kuwekwa mbali na rehema. Kama kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَسُحْقًا لِأَصْحَابِ السَّعِيرِ {11}

Kuangamia ni kwa watu wa motoni” (67:11).

وَنَادَىٰ نُوحٌ رَبَّهُ فَقَالَ رَبِّ إِنَّ ابْنِي مِنْ أَهْلِي وَإِنَّ وَعْدَكَ الْحَقُّ وَأَنْتَ أَحْكَمُ الْحَاكِمِينَ {45}

Na Nuh alimwomba Mola wake akasema: Ewe Mola wangu! Hakika mwanangu ni katika watu wangu, na hakika ahadi yako ni haki na wewe ni hakimu bora wa mahakimu wote.

قَالَ يَا نُوحُ إِنَّهُ لَيْسَ مِنْ أَهْلِكَ ۖ إِنَّهُ عَمَلٌ غَيْرُ صَالِحٍ ۖ فَلَا تَسْأَلْنِ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۖ إِنِّي أَعِظُكَ أَنْ تَكُونَ مِنَ الْجَاهِلِينَ {46}

Akasema: Ewe Nuh! Huyo si katika watu wako. Hakika yeye ni mwendo usio mwema. Basi usiniombe usilo na ujuzi nalo mimi ninakuwaidhi usije ukawa miongoni mwa wasiojua.

قَالَ رَبِّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ أَنْ أَسْأَلَكَ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ ۖ وَإِلَّا تَغْفِرْ لِي وَتَرْحَمْنِي أَكُنْ مِنَ الْخَاسِرِينَ {47}

Akasema: Ewe Mola wangu! Hakika mimi ninajikinga kwako kukuomba nisilo na ujuzi nalo. Na kama hutanisamehe na kunirehemu nitakuwa katika waliohasirika.

قِيلَ يَا نُوحُ اهْبِطْ بِسَلَامٍ مِنَّا وَبَرَكَاتٍ عَلَيْكَ وَعَلَىٰ أُمَمٍ مِمَّنْ مَعَكَ ۚ وَأُمَمٌ سَنُمَتِّعُهُمْ ثُمَّ يَمَسُّهُمْ مِنَّا عَذَابٌ أَلِيمٌ {48}

Ikasemwa: Ewe Nuh! Shuka kwa salama itokayo kwetu na baraka juu yako na juu ya umma zilizo pamoja nawe; na zitakuwepo umma tutakazozistarehesha kisha zishikwe na adhabu chungu itokayo kwetu.

تِلْكَ مِنْ أَنْبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهَا إِلَيْكَ ۖ مَا كُنْتَ تَعْلَمُهَا أَنْتَ وَلَا قَوْمُكَ مِنْ قَبْلِ هَٰذَا ۖ فَاصْبِرْ ۖ إِنَّ الْعَاقِبَةَ لِلْمُتَّقِينَ {49}

Hizo ni habari za ghaibu tunazokupa wahyi. Hukuwa ukizijua wewe wala watu wako kabla ya hii. Basi subiri! Hakika mwisho ni wa wacha Mungu.