read

Aya 41-42: Utabiri Wa Ndoto Za Wafungwa Wawili

Baada ya Yusuf kutekeleza wajib wa mwito wa kulingania kwa Mwenyezi Mungu, aliwafasiria ndoto zao. Yule muhusika wa vinywaji alimwambia utatoka jela na utarudia kazi yako.

Na yule wa vyakula akamwambia utasulubiwa na ndege watakula kichwa chako. Yusuf alikuwa na uhakika na utabiri wake, kwa vile ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ndio maana akawaambia kuwa mambo yamekwisha.

Yusuf akamwambia yule wa vinywaji ambaye ataokoka, kuwa amwambie mfalme kuwa yeye amefungwa bila ya hatia yoyote na hata bila ya kuhukumiwa au kuulizwa. Lakini akasahau kumkumbuka Yusuf kutokana na kazi nyingi. Kwa hiyo akamaliza miaka gerezani. Kuna riwaya inayosema alikaa miaka saba, nyingine inasema minane. Mungu ndiye ajuaye zaidi.

وَقَالَ الْمَلِكُ إِنِّي أَرَىٰ سَبْعَ بَقَرَاتٍ سِمَانٍ يَأْكُلُهُنَّ سَبْعٌ عِجَافٌ وَسَبْعَ سُنْبُلَاتٍ خُضْرٍ وَأُخَرَ يَابِسَاتٍ ۖ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَفْتُونِي فِي رُؤْيَايَ إِنْ كُنْتُمْ لِلرُّؤْيَا تَعْبُرُونَ {43}

Na akasema mfalme: Hakika mimi nimeota ng’ombe saba walionona wanaliwa na ng’ombe saba waliokonda; na mashuke saba mabichi na mengine makavu. Enyi wakubwa niambieni maana ya ndoto yangu ikiwa nyinyi mnaweza kutabiri ndoto.

قَالُوا أَضْغَاثُ أَحْلَامٍ ۖ وَمَا نَحْنُ بِتَأْوِيلِ الْأَحْلَامِ بِعَالِمِينَ {44}

Wakasema: Ni ndoto zilizoparaganyika wala sisi sio wenye kujua tafsir ya ndoto hizi.

وَقَالَ الَّذِي نَجَا مِنْهُمَا وَادَّكَرَ بَعْدَ أُمَّةٍ أَنَا أُنَبِّئُكُمْ بِتَأْوِيلِهِ فَأَرْسِلُونِ {45}

Na akasema yule aliyeokoka katika wale wawili, akakumbuka baada ya muda: Mimi nitawaambia tafsiri yake, basi nitumeni.

يُوسُفُ أَيُّهَا الصِّدِّيقُ أَفْتِنَا فِي سَبْعِ بَقَرَاتٍ سِمَانٍ يَأْكُلُهُنَّ سَبْعٌ عِجَافٌ وَسَبْعِ سُنْبُلَاتٍ خُضْرٍ وَأُخَرَ يَابِسَاتٍ لَعَلِّي أَرْجِعُ إِلَى النَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَعْلَمُونَ {46}

Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng’ombe saba wanene kuliwa na ng’ombe saba waliokonda na mashuke saba mabichi na mengine yaliyokauka Ili nirejee kwa watu wapate kujua.

قَالَ تَزْرَعُونَ سَبْعَ سِنِينَ دَأَبًا فَمَا حَصَدْتُمْ فَذَرُوهُ فِي سُنْبُلِهِ إِلَّا قَلِيلًا مِمَّا تَأْكُلُونَ {47}

Akasema: Mtalima miaka saba mfululizo. Mtakachovuna kiwacheni katika mashuke yake, isipokuwa kidogo mtakachokula.

ثُمَّ يَأْتِي مِنْ بَعْدِ ذَٰلِكَ سَبْعٌ شِدَادٌ يَأْكُلْنَ مَا قَدَّمْتُمْ لَهُنَّ إِلَّا قَلِيلًا مِمَّا تُحْصِنُونَ {48}

Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayokula kile mlichokitanguliza, isipokuwa kidogo mtakachokihifadhi.

ثُمَّ يَأْتِي مِنْ بَعْدِ ذَٰلِكَ عَامٌ فِيهِ يُغَاثُ النَّاسُ وَفِيهِ يَعْصِرُونَ {49}

Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao watu watapata mvua na watakamua.