read

Aya 43-49: Ng’ombe Saba Walionona

Ndoto Na Nadharia Ya Freud

Ndoto ni dhahiri ya kinafsi. Wataalamu mbali mbali wamefanya utafiti na wakasema maneno mengi, lakini hawakuleta jambo la kutegemewa kuhusu ndoto kwa namna zake zote.

Ni kweli kwamba wamepatia katika kuelezea chanzo chake na wakagundua baadhi ya maradhi ya mishipa ya fahamu. Lakini kuna ndoto nyingine hazizungumzi lugha ya anayeiota wala nafsi au maisha yake. Wataalamu wameshindwa kuzielezea.

Freud amejaribu kukadiria tafsiri ya mamabo ya kijinsia kwenye ndoto zote; bali kwenye vitu vyote katika maisha haya au kwenye vitu vingi. Kwa hiyo ndoto zote kwake ni alama ya mambo ya kijinsia.

Mtoto mdogo wa kiume kumpenda zaidi mama yake na kumwonea wivu baba yake, kunatokana na fikra ya kinjisiya. Na vilevile msichana kumpenda zaidi baba yake na kumwonea wivu mama yake. Bali hata urafiki wa aina yoyote. Hata fikra ya dini pia, anasema, matokeo yake ni mambo ya kijinsiya; ndio maana dini ikahofia kulala pamoja maharimu.

Wataalamu wengi wameipinga fikra hii na wakasema kuwa binadamu anaendeshwa na matamanio mengi, sio mambo ya kijinsia tu. Gastro kutoka Poland, ametunga Kitabu cha kumjibu Freud katika juzuu mbili na akakiita Dream and sex na kikatarjumiwa ( kwa kiarabu) na Fauzi Shushtary.

Miongoni mwa yaliyomo katika Kitabu hicho ni kwamba maulama wamezichambua ndoto kwa maelfu kutoka kwa watu mbalimbali, wakakuta karibu asilimia hamsini za ndoto hizo haziwezekani kuzifasiri kwa nadharia ya Freud. Na nadharia hii inaacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu.
Nadharia ya Freud haifuatwi isipokuwa na yeye mwenyewe. Yeye ni mwenye mawazo ya kuona kila kilicho mduara basi ni cha kike na kila kilicho mstatili basi ni kiume. Lakini ubinadamu uko mbali na nadharia hii. Nadharia hii ni finyu, haina ukweli. Binadamu sio mtumwa wa ngono tu; isipokuwa ni mtumwa wa starehe nyingi, ngono ikiwa moja yao. Nyingine ni mapenzi, urafiki, urembo, maarifa, utawala, nguvu na uhuru. Vizuri ni kuungana starehe zote hizi katika maisha ya pamoja yenye upeo mpana.

Tuanavyo ni kuwa ndoto ziko aina nyingi; kama ifuatavyo:-

Kuna zile zinazoakisi desturi na fikra ya mtu; kama mwanafalsafa kuota kuwa anajadiliana na Plato au Aristotle. Au Mwislamu kuswali msikitini, mkristo na msalaba wake kanisani, mkulima akilima shambani, mjenzi akijenga n.k. Aina hii ya ndoto iko wazi haihitaji ufafanuzi wala watu hawatofautiani kwayo. Kwa sababu iko pamoja na tafsiri yake.

Kuna zisizokuwa na uhusiano kabisa na maisha ya muotaji na fikra zake; kama mfalme kuota n’gombe saba na mashuke, ambapo yeye si mkulima wala mfugaji. Ndoto imekuja kuonya juu ya ukame baada ya rutuba.

Kuna ndoto nyingine ziko sawa na yale yaliyotokea mtu akiwa macho. Ndoto hii ni nadra kutokea.

Aina hizi mbili za mwisho za ndoto bado elimu haijagundua tafsir yake, pengine hivi karibuni inawezekana kujulikana. Wengine wamefasiri kuwa ni sadfa. Bila ya shaka sadfa ni kimbilio la kushindwa. Mwengine akatafsiri kuwa ni hisia za binadamu ambazo hazijulikani hakika yake. Huku ndiko kushindwa kabisa.

Mnamo mwaka 1956 nilimuota ndugu yangu, marehemu Sheikh Abdulkarim, aliyefariki miaka ishirini iliyopita. Akanipa habari ya mambo yatakayotokea na wakati wake. Ikawa kama alivyonieleza. Baadae nikaota ndoto nyingine mbaya kama ile ya mwanzo, ikatokea kama nilivyoota. Basi nikafanya utani na rafiki yangu na kumwambia kuwa ndoto mbaya huwa za kweli kinyume na ndoto za shari.

Nilipokuwa nafasiri sura Yusuf nilisoma ibara kwenye Tafsir ya Razi ikisema: “Jua kwamba wenye hekima wanasema kuwa ndoto mbaya zinajitokeza haraka” basi nikashangaa sana na kukumbuka mshairi aliyesema: Ubaya niutao uko karibu uzuri niutao uko janibu

Kwa ufupi ni kwamba hakuna udhibiti hasa wa kutegemea katika kufasiri ndoto kwa ukamilifu. Kwa sababu zinapingana. Kuna zinazotokea kwa wasiwasi wa nafsi na matatizo yake. Chimbuko la ndoto hii linajulikana, nyingine zinanukuu yale yaliyotokea kabla ya kulala. Aina hii hatuijui chimbuko lake. Nyingine ni ishara ya yatakayotokea baadae; kama vile nyota zilizomsujudia Yusuf, mkate uliochukuliwa na mfungwa na ng’ombe na mashuke aliyoyaota mfalme wa Misri. Hii pia haijulikani siri yake wala chimbuko lake.

Yule anayedai kuwa aina hizi mbili za ndoto ni bishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu au ni hisia za binadamu, basi atakuwa amedai kuwa na elimu ya ghaibu, asiyekubali kuwa hajui hata yale aliyoyafunika Mwenyezi Mungu kwa waja wake.

Na akasema mfalme: Hakika mimi nimeota ng’ombe saba walionona wanaliwa na ng’ombe saba waliokonda na mashuke saba mabichi na mengine makavu.

Siku moja Mfalme alota ndoto ya kushangaza kuwa ng’ombe walionona wanaliwa na waliokonda. Mfano wa ndoto kama hii haukuwahi kutokea. Vilevile mashuke saba mabichi na mengine saba makavu katika shamba moja. Akawaita wasaidizi wake na wakuu wa serkali yake na kuwaambia:

Enyi wakubwa niambieni maana ya ndoto yangu ikiwa nyinyi mnaweza kutabiri ndoto.”

Lakini walishindwa kutafsir na Wakasema:

Ni ndoto zilizoparaganyika wala sisi sio wenye kujua tafsir ya ndoto hizi.

Maana yako wazi, lakini Razi hapa ana maneno yenye faida, ambayo kwa ufupi ni kwamba Mwenyezi Mungu mtukufu alijaalia ndoto ya mfalme ni sababu ya kuokoka Yusuf (a.s.). Mwenyezi Mungu akitaka jambo huliandalia sababu zake. Mfalme ameshuhudia dhaifu akimtawala mwenye nguvu, jambo ambalo ni kinyume na maumbile.

Akaona kuwa inatoa onyo la shari, lakini ikawa hajui hakika yake. Kwa hiyo akawa na hamu sana ya kujua hakika yake. Akawakusanya watabiri na kuwauliza tafsir ya alivyoota, lakini Mwenyezi Mungu akawapofusha na hakika yake, ili iwe ni sababu ya kutoka Yusuf gerezani.

Kisha Razi akaendelea kusema: “Watabri hawakukataa kuwa na ujuzi wa kutabiri ndoto; isipokuwa waligawanya ndoto kwenye mafungu mawili: Zile zilizopangika ambazo zinakuwa nyepesi kuzijua na zile ambazo zimeparaganyika ambazo hazina tafsir isipokuwa dhana na kuwazia tu, na wakasema kuwa ndoto ya Mfalme ni katika ile isiyokuwa na tafsir au wa hawaijui; pengine yule aliyebobea kwenye ilimu ya ndoto anaweza kutafsiri”.

Na akasema yule aliyeokoka katika wale wawili, akakumbuka baada ya muda: Mimi nitawaambia tafsiri yake, basi nitumeni.

Itakumbukwa kwamba Yusuf aliingia gerezani na vijana wawili na akawatafsiria ndoto zao amabazo zilitokea kweli kama alivyowatafsiria. Mmoja aliuawa na mwingine akaokoka.

Aya hii inamuashiria yule aliyeokoka ambaye aliambiwa na Yusuf, ni kumbuke mbele ya bwana wako, lakini shetani alimsahauliza. Basi alipoona kudangana kwa mfalme kuhusu ndoto yake na hamu ya kutafsiriwa na kushindwa watabiri kuiagua, alimkumbuka Yusuf na akampa habari Mfalme za Yusuf, kuhusu wema wake na ujuzi wake wa kutafsiri ndoto, akamwambia kama ukinituma nitakuletea habari za uhakika.

Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng’ombe saba walionona kuliwa na ng’ombe saba waliokonda na mashuke saba mabichi na mengine yaliyokauka.

Mfalme almwamrisha mtumishi wake wa vinywaji kwenda kwa huyo mtu mwema aliyemzungumizia na amwelezee hiyo ndoto kisha amletee habari atakazozisikia kwake. Yule mtumishi alikwenda kwa Yusuf, na kama kawaida akaomba msamaha kwa kusahau maagizo ya Yusuf. Baada ya kumsifu kwa ukweli alimsimulia ndoto ya Mfalme, na kumtaka amtafsirie huku akisema:

Ili nirejee kwa watu wapate kujua.

Yaani mfalme na wasaidizi wake wapate kujua hadhi yako na fadhila yako, ili waweze kukutoa gerezani.

Akasema mtalima miaka saba mfululizo. Mtakachovuna kiwacheni katika mashuke yake, isipokuwa kidogo mtakachokula.

Yusuf alimwambia kuwa watalima miaka saba mfululizo na kutakuwa na rutuba katika miaka hiyo. Hiyo inaishiriwa na ng’ombe saba walionona na mashuke ya kijani; kila ng’ombe na kila shuke likiashiria mwaka mmoja.

Kisha akawapa nasaha Yusuf kuwa kila watakachokivuna wakiweke akiba kikiwa kwenye mashuke yake, kwa sababu ngano ikiwa kwenye mashuke yake inahifadhika na wadudu waharibifu na inabaki kuwa kavu. Ama kile mnachotaka kukila basi mnaweza kukipukuchua huku mkichunga israf na kutosheka na kinachotosheleza haja tu.

Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayokula kile mlichokitanguliza, isipokuwa kidogo mtakachokihifadhi.

Miaka imefanywa ndiyo inayokula, lakini makusudio yake ni watu, mara nyingi Waarabu wanatumia aina hii ya maneno. Maana ni kuwa miaka ya mavuno itafuatiwa na miaka ya ukame, hakitamea chochote ardhini. Hapo mtakula kile mlichokiweka akiba, na hakutabakia isipokuwa kiasi kidogo tu cha mbegu.

Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao watu watapata mvua na watakamua.

Yaani baada ya miaka saba ya shida utafuatia mwaka amabao utakuwa na mvua, mimea itamea na miti itanawiri, na watu watakamua matunda wapate vinywaji na mafuta.

Kwa hakika mwaka huu haukuashiriwa kwenye ndoto ya Mfalme, isipokuwa ni katika ghaibu za mwenyezi Mungu ambazo hawazijui isipokuwa wale aliowaridhia katika mitume.

وَقَالَ الْمَلِكُ ائْتُونِي بِهِ ۖ فَلَمَّا جَاءَهُ الرَّسُولُ قَالَ ارْجِعْ إِلَىٰ رَبِّكَ فَاسْأَلْهُ مَا بَالُ النِّسْوَةِ اللَّاتِي قَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ ۚ إِنَّ رَبِّي بِكَيْدِهِنَّ عَلِيمٌ {50}

Na mfalme akasema: Nileteeni. Basi mjumbe alipomjia Yusuf alisema: Rejea kwa bwana wako na umuulize habari ya wale wanawake waliokata mikono yao. Hakika Mola wangu anajua vizuri vitimbi vyao.

قَالَ مَا خَطْبُكُنَّ إِذْ رَاوَدْتُنَّ يُوسُفَ عَنْ نَفْسِهِ ۚ قُلْنَ حَاشَ لِلَّهِ مَا عَلِمْنَا عَلَيْهِ مِنْ سُوءٍ ۚ قَالَتِ امْرَأَتُ الْعَزِيزِ الْآنَ حَصْحَصَ الْحَقُّ أَنَا رَاوَدْتُهُ عَنْ نَفْسِهِ وَإِنَّهُ لَمِنَ الصَّادِقِينَ {51}

Akasema: Mlikuwa mna nini nyinyi mlipomshawishi Yusuf kinyume cha nafsi yake? Wakasema: Hasha lillah! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mke wa mheshimiwa akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliyemtaka kinyume cha nafsi yake na hakika yeye ni katika wakweli.

ذَٰلِكَ لِيَعْلَمَ أَنِّي لَمْ أَخُنْهُ بِالْغَيْبِ وَأَنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي كَيْدَ الْخَائِنِينَ {52}

Hayo ni apate kujua kuwa mimi sikumfanyia khiyana alipokuwa hayuko. Na kwamba Mwenyezi Mungu haviongoi vitimbi vya wahaini.