read

Aya 50-51: Mfalme Akasema Nileteeni

Na mfalme akasema: Nileteeni.

Baada ya Yusuf kufasiri ndoto ya Mfalme, yule mjumbe alirudi kwa bwana wake na ule utabiri na nasaha. Na mfalme akagundua kuwa kwenye kauli ya Yusuf kuna elimu ikhlas na ukweli; akapenda awe karibu naye ili anufaike na elimu yake na ikhlasi yake, akasema aletewe huyo aliyefasiri. Qur’ani imetosheka na kauli hii ya mfalme na kumwacha msomaji aongeze mwenyewe.

Basi mjumbe alipomjia Yusuf na kumwita aende kwa Mfalme, alisema Yusuf: Rejea kwa bwana wako na umuulize habari ya wale wanawake waliokata mikono yao. Hakika Mola wangu anajua vizuri vitimbi vyao.

Yusuf alikataa kutoka gerezani na wala hakuwa na haraka ya kukimbilia mwito wa Mfalme, kama wafanyavyo wengi wanaojiita watu wa dini. Hakumharakia kwa kupima mambo yafuatayo:-

WKwamba mumin wa kweli hauoni ukubwa; isipokuwa ukubwa wa Mungu; wala hajali lolote katika njia ya kuidhihirisha haki na kuitangaza. Na kwa ajili hii, alikataa, siddiq (mkweli) kutoka gerezani hivi hivi tu, kwa msamaha wa raisi. Aliendelea kushikilia msimamo wa kuitangaza haki kabla ya chochote. Akahiyari kuvumilia kifungo maisha yote au atoke gerezani akiwa hana tuhumma yoyote.

W Yusuf alipendelea upite uchunguzi akiwa yeye hayupo. Hilo litamasafisha zaidi na tuhumma na kufahamisha zaidi hadhi yake na upole wake.
W Yusuf alikuwa na imani kwamba uchunguzi utakuwa kwa masilahi yake; na kutofanya haraka kutoka gerezani kutapelekea watu kuwa na imani naye na kuitikia mwito wa ujumbe wake.

Kuongezea kuwa hilo litakata njia ya atakayewasilisha tuhumma kwa Mfalme pale atakapokuwa karibu naye na kwa mwenginewe, atakapomwita kwenye haki.

Mjumbe alirudi kwa mfalme na kumpa habari kuwa Yusuf amekataa kutoka gerezani mpaka kufanywe uchunguzi wa kufungwa kwake.

Basi Mfalme akalichukulia umuhimu hilo na akawahudhurisha wanawake, akasema:

Mlikuwa mna nini nyinyi mlipomshawishi Yusuf kinyume cha nafsi yake? Wakasema: Hasha lillah! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mke wa mheshimiwa akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliyemtaka kinyume cha nafsi yake na hakika yeye ni katika wakweli.

Huku ndiko kukiri hasa, kunakoondoa tuhumma na shakashaka zote, kwa sababu kunatoka kwa mtesi mwenyewe. Hana uovu… Yeye ni mkweli… Namna hii haki hudhihiri, hata muda ukiwa mrefu. Wanasalimu amri waovu wakiwa hawana la kufanya, hawana kimbilio wala kukana.

Hayo ni apate kujua kuwa mimi sikumfanyia khiyana alipokuwa hayuko.

Wafasiri wametofautiana kuhusu Aya hii: Kuna wanaosema kuwa haya ni maneno ya Yusuf kwa maana ya kuwa nimetaka uchunguzi pamoja na wanawake wengine ili mheshimiwa waziri ajue kuwa ikumfanyia khiyana kwa mkewe wakati hayuko.

Wengine wanasema kuwa ni maneno ya mke wa waziri. Sisi tuko pamoja na wanaosema hivi kwa kuangalia dhahiri ya mfumo wa kuungana maneno. Hapo dhamir ya sikumfanyia khiyana inamrudia Yusuf. Maana yake ni kuwa mke wa waziri hakumtaja kwa ubaya Yusuf wakati akiwa gerezani mpaka sasa. Hata pale alipomsingizia kwa mumewe mwenyewe Yusuf alikuwepo.

Na kwamba Mwenyezi Mungu haviongoi vitimbi vya wahaini.

Bali anawafedhehesha, anafichua siri yao na anawanusuru nao waumini, kama alivyowafedhehsha wanawake na kumnusuru Yusuf.

وَأَرَادُوا بِهِ كَيْدًا فَجَعَلْنَاهُمُ الْأَخْسَرِينَ {70}

“Na walimkusudia ubaya, lakini tukawafanya wao ndio wenye kupata hasara.” (21:70).