read

Aya 50-56

Na kwa A’ad (tulimpeleka) ndugu yao Hud, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye tu. Hamkuwa nyinyi isipokuwa ni wazushi mnaozusha ibada ya masanamu.

Hud anatokana na kabila la A’ad kinasaba na kinchi, ndio maana Mwenyezi Mungu akamsifu kuwa ni ndugu yao. Ujumbe wake huu ni ujumbe wa mitume wote.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika kisa cha Nuh katika Aya 26 ya sura hii, na kisa cha Hud katika Juz.8 (7:65).Na tumetaja ilipo kaburi yake na kwamba yeye ndiye wa kwanza kuzungumza kiarabu; naye ndiye baba wa ya Yaman na Mudhar. Rudia huko.

Enyi watu wangu! Siwaombi ujira juu ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa yule aliyeniumba, basi hamtumii akili?

Anayefanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hataki riziki kutoka kwa mwengine na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayedhuru na kunufaisha. Tafsiri hii imepita katika Aya 29 ya sura hii.

Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake

Tofauti kati ya kuomba maghufira na kutubia ni: Kuomba maghufira ni kutaka msamaha wa yaliyopita bila ya kuangalia yajayo. Na kutubia ni kuomba msamaha kwa yaliyopita na kuahidi kutofanya tena

Atawaletea mbingu zenye mvua tele na atawazidishi nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke kuwa waovu.

Inaonyesha kuwa wao walikuwa ni watu wa kilimo na mifugo ndio maanaMwenyezi Mungu akawavutia kwenye mvua nyingi; kama ambavyo kauli yake: ‘Atawazidishia nguvu juuu ya nguvu zenu,’ inafahamisha kuwa walikuwa ni watu wenye nguvu za Kiundani na dhahiri (kimaana na kimaada) Hilo linaonyeshwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِعَادٍ {6}

إِرَمَ ذَاتِ الْعِمَادِ {7}

الَّتِي لَمْ يُخْلَقْ مِثْلُهَا فِي الْبِلَادِ {8}

Je, hukuona jinsi Mola wako alivyowafanya Aa’d Wairam wenye maguzo marefu. Ambao mfano wao haukuumbwa katika miji” (89:6-8).

Unaweza kuuliza kuwa Mwenyezi Mungu ameunganisha baina ya imani na kuteremshwa mvua. Utasemaji wewe ulipofasiri Juz. 9 (8:2) ukasema kuwa dini haioteshi ngano na kwamba Mwenyezi Mungu hupitisha mambo kwa desturi ya kimaumbile?

Jibu: Ni kweli kwamba Mwenyezi Mungu anapitisha mambo kulingana na desturi ya kimaumbile, hilo halina shaka. Lakini hilo halizuwii kupatikana muujiza, au kuacha desturi kwa hekima fulani. Ukomo wa desturi zote na maumbile unaishilia kwenye matakwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Yeye pekee ndiye msababishaji wa sababu zote. Na matakwa haya matakatifu yanaweza kufungamana na kupatikana kitu moja kwa moja bila ya kupitia sababu yoyote iliyozoeleka; kama Tufani ya Nuh n.k. Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka kutoidhihirisha miujiza hii inayohalifu kawaida, isipokuwa kwa kupatikana mtume, ili kuthibitisha utume wake, kuitikiwa mwito wake au kuwaadhibu maadui zake.

Kwa maneno mengine ni kuwa kupita mambo kwa desturi ni kitu kingine na muujiza ambao unategemea matakwa ya Mwenyezi Mungu ni kitu kingine.

Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi.

Huu ni uongo na uzushi. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hatumi mjumbe ila humsheheni na hoja za kutosha juu ya utume wake. Watu wa Hud walikataa mwito wake na hoja zake kwa vile zinapingana na hawaa zao; kama ilivyokuwa kwa kaumu nyingine za mitume. Mwenyezi Mungu anasema:

كُلَّمَا جَاءَهُمْ رَسُولٌ بِمَا لَا تَهْوَىٰ أَنْفُسُهُمْ فَرِيقًا كَذَّبُوا وَفَرِيقًا يَقْتُلُونَ {70}

“Kila alipowafikia Mtume kwa yale zisiyoyapenda nafsi zao kundi moja wakalikadhibisha na kundi jengine wakaliua.”Juz.6 (5:70)

Wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kauli yako.

Mwenye Kitabu Al-Mughni anasema kuwa herufi a’n hapa ni ya sababu; yaani hatuwezi kuacha miungu kwa sababu tu ya kusema kwako iacheni, bila kutuonyesha dalili wala ubainifu .

Na wala sisi hatukuamini wewe.

Huu ni ufafanuzi wa kauli yao ya kutoacha miungu yao. Amesema kweli yule aliyesema: Mtu ndiye aliyeumba Miungu wala sio miungu iliyoumba mtu.

Hatuna la kusema ila baadhi ya miungu yetu imekutia balaa.

Kauli yao hii inaonyesha upeo wa ujinga wao na imani yao iliyo kombo ya vigano. Mawe yaliyotulia wanayaamini kuwa yanamdhuru anayesema yasiabudiwe! Mtu akifikia kiwango hiki cha ujinga basi ni wa kuachana naye tu. Ndio maana Mwenyezi Mungu akawasifu kwa uziwi na upofu.

Akasema: Hakika mimi ninamshuhudisha Mwenyezi Mungu na nyinyi shuhudieni kwamba niko mbali na hao mnaowashirikisha. Mkamwacha Yeye basi nyote nifanyieni vitimbi tena msinipe muda.

Walipomwambia kuwa miungu yao imemdhuru, aliwapinga na kuwapa ushindani kuwa wajikusanye wao na waungu wao na wajaribu kila wawezavyo wamdhuru na yeye yuko tayari. Hii maana yake ni kwamba wao wako kwenye mghafala na ni wenye kudanganyika.

Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu Mola wangu na Mola wenu.

Hii ndio sababu ya kushinda kwao kumdhuru na kuwabeza wao na masanamu yao.

Hakuna mnyama yeyote isipokuwa Yeye amemshika utosi wake.

Yaani hakuna kiumbe chochote ila Mwenyezi Mungu hukiendesha vile atakavyo. Hakuna chochote kinachoweza kujikinga au kujinufahisha hicho chenyewe tu, sikwambii kunufaisha au kudhuru kingine.

Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka.

Yeye ndiye anayenusuru na kutweza na anatoa thawabu na kuadhibu kwa msingi wa njia hii iliyonyooka, njia ya haki na uadilifu.
Unaweza kuuliza: Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye aliyeshika hatamu ya mja na utosi wake, kwa maana ya kumpeleka vile atakavyo; na ikiwa Yeye Mwenyezi Mungu yuko juu ya njia iliyonyooka, hapo patakuwa na mambo mawili:

1. Kuwa mja ni mwenye kuendeshwa hana hiyari; kwa sababu anakokotwa.

2. Kuwa kila mtu yuko juu ya njia iliyonyooka katika vitendo vyake vyote na kauli zake; kwa vile anamfuata; Mungu sawa na mnyama aliyefungwa hatamu anavyomfuata yule mwenye kushika hatamu akiwa kwenye njia nzuri na mnyama naye atakuwa kwenye njia nzuri?

Jibu: Makusudio ya kushika utosi sio kuwa mja hana hiyari katika cho- chote; isipokuwa ni fumbo la uweza wa Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu na kwamba Yeye pekee ndiye mwenye kunufaisha. Hiyo ni kuwajibu washirikina ambao wameyapa masanamu uwezo wa kudhuru na kunufaisha.

فَإِنْ تَوَلَّوْا فَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ مَا أُرْسِلْتُ بِهِ إِلَيْكُمْ ۚ وَيَسْتَخْلِفُ رَبِّي قَوْمًا غَيْرَكُمْ وَلَا تَضُرُّونَهُ شَيْئًا ۚ إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَفِيظٌ {57}

Wakirudi nyuma, basi mimi nimekwishawafikishia niliyotumwa kwenu. Na Mola wangu atawaleta watu wengine badala ya nyinyi. Wala hamumdhuru kitu. Hakika Mola wangu ni mwenye kuhifadhi kila kitu.

وَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا نَجَّيْنَا هُودًا وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِنَّا وَنَجَّيْنَاهُمْ مِنْ عَذَابٍ غَلِيظٍ {58}

Ilipofika amri yetu tulimwokoa Hud na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu na tukawaokoa na adhabu ngumu.

وَتِلْكَ عَادٌ ۖ جَحَدُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَعَصَوْا رُسُلَهُ وَاتَّبَعُوا أَمْرَ كُلِّ جَبَّارٍ عَنِيدٍ {59}

Na hao ndio Aa’d, walikanusha Ishara za Mola wao na wakawaasi mitume wake na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inadi.

وَأُتْبِعُوا فِي هَٰذِهِ الدُّنْيَا لَعْنَةً وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا إِنَّ عَادًا كَفَرُوا رَبَّهُمْ ۗ أَلَا بُعْدًا لِعَادٍ قَوْمِ هُودٍ {60}

Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na siku ya kiyama. Ehee! Hakika Aa’d walimkufuru Mola wao. Ehee! Wamepotelea mbali watu wa Hud.