read

Aya 57-60: Wakirudi Nyuma

Maana

Wakirudi nyuma, basi mimi nimekwishawafikishia niliyotumwa kwenu bila ya kuchoka wala kuzembea.

Na Mola wangu atawaleta watu wengine badala ya nyinyi baada ya kuwaletea adhabu ya dunia kabla ya Akhera.

Wala hamumdhuru kitu kwa kuacha kwenu imani

Hakika Mola wangu ni mwenye kuhifadhi kila kitu anachunga kila kitu na kukiangalia kwa ujuzi wake na hekima yake. Anasema ibn Arabi katika Futahatul Makkiyya: “Kama ambavyo Mola wako ni mwenye kuhifadhi kila kitu, basi naye ni mwenye kuhifadhika na kila kitu.” Anaashiria kauli ya aliyesema: “Kila kitu kina Aya”

Ilipofika amri yetu tulimwokoa Hud na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu na tukawaokoa na adhabu ngumu.

Makusudio ya amri yetu ni adhabu yetu, kuokoka kwa kwanza ni kutokana na adhabu ya dunia na kuokoka kwa pili ni kutokana na adhabu ya Akhera.

Imesemekana kuwa kuokoka kwa kwanza ni kubainisha kuokoka na adhabu bila ya kuangalia aina yake na kuokoka kwa pili ni kubainisha aina ya adhabu iliyowashukia watu wa Hud ambayo ilikuwa ni ngumu. Maana zote mbili zinakubali. Yametangulia maelezo ya kuokoka Hud na waliokuwa pamoja naye katika Juz. 8 (7:72).

Na hao ndio Aa’d, walikanusha Ishara za Mola wao na wakawaasi mitume yake na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inadi.

Baada ya kuelza kwa ufupi kisa cha Aa’d aliashiria Mwenyezi Mungu, sababu ya kuangamia kwao kwamba ni kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu na Ishara zake, kuasi kwao mitume, kuacha kuitetea haki, kuikinga batili na kufuata kwao upotevu na utaghuti.

Mwenyezi Mungu amesema: ‘na wakawaasi mitume’ na wala hakusema na wakamuasi mtume. Kwa sabau mwenye kumwasi mtume mmoja basi ni kama amewaasi wote kwa kuangalia kuwa ujumbe ni mmoja tu, nao ni mwito wa imani ya umoja wa Mungu na ufufuo

Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na siku ya kiyama.

Yaani walifanya yanayowajibisha laana duniani na Akhera. Maana ya laana ni kuwa mbali na kheri. Ndio maana Mwenyezi Mungu akasema:

Ehee! Hakika Aa’d walimkufuru Mola wao. Ehee! Wamepotelea mbali watu wa Hud.

Limekaririka neno ‘Ehe!’ kwa kutilia mkazo na kusisitiza kukanya.

وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۚ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرُهُ ۖ هُوَ أَنْشَأَكُمْ مِنَ الْأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُجِيبٌ {61}

Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye. Yeye ndiye aliyewaumba kutokana na ardhi na akaifanya iwe koloni lenu. Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake. Hakika Mola wangu yuko karibu mwenye kuitikia maombi.

قَالُوا يَا صَالِحُ قَدْ كُنْتَ فِينَا مَرْجُوًّا قَبْلَ هَٰذَا ۖ أَتَنْهَانَا أَنْ نَعْبُدَ مَا يَعْبُدُ آبَاؤُنَا وَإِنَّنَا لَفِي شَكٍّ مِمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ مُرِيبٍ {62}

Wakasema: Ewe Swaleh! Ulikuwa ukitarajiwa kwetu kabla ya haya. Hivi unatukataza kuabudu waliyokuwa wakiyaabudu mababa zetu? Na sisi tuna shaka na wasiwasi kwa haya unayotuitia.

قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِنْ كُنْتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِنْ رَبِّي وَآتَانِي مِنْهُ رَحْمَةً فَمَنْ يَنْصُرُنِي مِنَ اللَّهِ إِنْ عَصَيْتُهُ ۖ فَمَا تَزِيدُونَنِي غَيْرَ تَخْسِيرٍ {63}

Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa nina dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na akanipa rehema kutoka kwake, basi ni nani atakayenisaidia kwa Mwenyezi Mungu kama nikimwasi? Basi hapo hamtanizidishia isipokuwa hasara tu.