read

Aya 6 – 8: Hakuna Mnyama Yoyote Katika Ardhi

Maana

Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu.

Neno Daabbah, kilugha lina maana ya kila anayetembea ardhini. Na kidesturi lina maana ya mnyama anayepandwa kama vile punda, farasi n.k.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameumba ardhi na akampa kila anayetembea ardhini mahitaji yake yote, kuanzia mdudu, mbu, ndovu, binadamu n.k. Na akampa kila mmoja uwezo wa kuhangaikia riziki yake.

Kwa hiyo maana ya Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu amejaalia kwa kila kiumbe hai riziki yake iliyowekwa ardhini. Na wala sio kuwa Mwenyezi Mungu amekadiria riziki mahsus kwa kila kiumbe hai, ambayo haizidi kwa kuihangaikia wala kupungua kwa kuacha kuitafuta, kama wasemavyo wengine! La, Sio hivyo! Mwenye Tafsir Al-Manar anasema: “Baadhi ya watu na washairi wanadai kuwa kuchumma na kuacha kuchumma ni sawa, kama wanavyosema baaadhi ya wajinga wasiojali:

Mekwishapita kalamu bure sijihangaishe
Kuhangaikia riziki ni sawa na kujikalia
Sijitie na wazimu wala sijishughilishe
Alo tumboni mwa mama riziki hujipatia

Mshairi huyu ndiye anayestahiki kuitwa mwenda wazimu wala sio yule anayeihangaikia riziki yake.
Kwa maelezo zaidi unaweza kurudia Juz.6 (5:64) kifungu cha ‘riziki na ufisadi,’ Juz.7 (5:100) kifingu cha ‘je riziki ni bahati au majaaliwa?’ Juz.8 (7: 56) kifungu cha ‘Mwenyezi mungu ameitengeneza vizuri ardhi na binadamu akaiharibu’

Na anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu kinachobainisha.

Makusudio ya mapitio hapa ni alipokuwa kabla ya kuwa katika tumbo la uzazi na kabla ya kutembea ardhini. Na Kitabu kinachobainisha ni fumbo la kwamba Mwenyezi Mungu anajua vizuri kila kitu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayesababisha sababu za kuishi na uhai wa kila mnyama, vyovyote alivyo na atakavyokuwa.

Kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu ni muweza na Mjuzi wa kila kitu.

Naye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (7:54) .

Na arshi yake ilikuwa juu ya maji.

Makusudio ya arshi (kiti cha enzi) ni utawala na ufalme. Aya inafahamisha kuwa maji yalikuwa kabla ya kuumbwa mbingu na ardhi. Ama yalitoka wapi au yalikuwa vipi, hakuna nukuu ya Aya wala Hadith mutawatir juu ya hilo. Akili peke yake haina ujuzi wa hilo.

Hatuna tafsiri yoyote kuhusu mada ya kwanza iliyoumbiwa ulimwengu, isipokuwa neno lake Mwenyezi Mungu. ‘kuwa ukawa’ atakayekanusha haya tutamsomeya:

لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ {6}

“Mna dini yenu na mimi nina dini yangu.” (109:6)

Ili awajaribu ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo?

Yaani Mwenyezi Mungu ametuleta sisi katika ardhi na akatupatia nishati zilizomo ndani yake, ili awapambanue wale wanaoishi kwa jasho lao na wanaoishi kwa jasho la wenzao. Atawaadhibu hawa kwa kuasi kwao na kuwapa thawabu wale kwa utiifu wao.

Na kama ukisema, hakika nyinyi mtafufuliwa baada ya kufa, bila shaka waliokufuru watasema hayakuwa haya ila ni uchawi ulio wazi.

Aya hii ni kama Aya nyingine miongoni mwa Aya nyingi zinazowaelezea wanaokadhibisha ufufuo; isipokuwa ina tofauti moja tu, kwamba hapa kumeelezwa kukadhibisha kwao kwa kufafanisha ufufuo na uchawi, kuwa ni kuwahadaa watu ili wavutike kumfuata Mtume Muhamad (s.a.w.).

Na kama tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda uliohisabiwa bila shaka watasema: Nini kinachozuia hiyo adhabu?

Yaani watasema ni kitu gani kinachozuia adhabu isitufikia ikiwa ni kweli?

Sikilizeni! Siku itakapowajia basi haitaondolewa kwao.

Kwa sababu adhabu yake Mwenyezi Mungu haiwezi kuzuiwa na watu wenye makosa.

Na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

Yaani adhabu itawashukia, kuwa ni malipo ya dharau zao na kutohofia kwao ghadhabu za Mwenyezi Mungu. “Dhambi kubwa ni ile aliyoipuuza mwenye dhambi hiyo” kama asemavyo Imam Ali (a.s.).

Na miongoni mwa kauli zake nyingine ni: “Mtu mwenye dhana nzuri zaidi ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemhofia zaidi Mwenyezi Mungu.”

وَلَئِنْ أَذَقْنَا الْإِنْسَانَ مِنَّا رَحْمَةً ثُمَّ نَزَعْنَاهَا مِنْهُ إِنَّهُ لَيَئُوسٌ كَفُورٌ {9}

Na kama tukimwonjesha mtu rehma inayotoka kwetu, kisha tukamwondolea, hakika yeye hukata tamaa akakufuru.

وَلَئِنْ أَذَقْنَاهُ نَعْمَاءَ بَعْدَ ضَرَّاءَ مَسَّتْهُ لَيَقُولَنَّ ذَهَبَ السَّيِّئَاتُ عَنِّي ۚ إِنَّهُ لَفَرِحٌ فَخُورٌ {10}

Na kama tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyompata, bila shaka husema: taabu zimeniondokea. Hakika yeye ndiye mwenye kufurahi sana akijitapa.

إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَٰئِكَ لَهُمْ مَغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ {11}

Isipokuwa wale waliosubiri na wakatenda mema, hao watapata msamaha na ujira mkubwa.