read

Aya 61-63: Swaleh

Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye

Imetangulia Aya hii kwa herufi zake katika Juz. 8 (7:73).
Yeye ndiye aliyewaumba kutokana na ardhi.

Hakuna kitu chochte chenye uhai, kiwe binadamu, mnyama au mmea, ila kitakuwa kimetokana na Ardhi moja kwa moja au kupitia kingine.

Na akaifanya iwe koloni lenu.

Qur’ani Tukufu imelitumia neno hili ukoloni (istimari) kwa maana ya kuamirisha na kuendeleza. Na hii ndiyo maana yake nzuri. Ama hivi leo neno hili linatumika katika dhulma, unyang’anyi na kuwakandamiza wanyonge; na hiyo ndiyo maana mbaya sana. Angalia kifungu cha ‘Mwenyezi Mungu ameitengeneza ardhi na binadamu akaiharibu’ katika Juz. 8 (7:56)

Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake.

Hud aliwaambia watu namna hii hii katika Aya 52 ya sura hii. Huko tumeeleza tofauti kati ya kuomba maghufira na kutubia.

Hakika Mola wangu yuko karibu mwenye kuitikia maombi.

Yuko karibu na mwenye kumfanyia ikhlas na mwenye kumwitikia anayeitikia mwito wake.

Wakasema: Ewe Swaleh! Ulikuwa ukitarajiwa kwetu kabla ya haya ya kutukataza kuabudu masanamu. Lakini hivi sasa, baada ya kutukataza hatukuamini tena.

Hivi unatukataza kuabudu waliyokuwa wakiyaabudu mababa zetu?

Vizazi na vizazi wameyaabudu na wakayapelekea madhabihu na hakuna yeyote aliyewahi kuwakataza, je yeye watamkubalia kweli?

Na sisi tuna shaka na wasiwasi kwa haya unayotuitia.

Hii ndiyo mantiki ya kijinga kila mahali na kila wakati. Kila kitu ni desturi yetu na kufuata wazee wetu tu.

Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa nina dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na akanipa rehema kutoka kwake, basi ni nani atakayenisaidia kwa Mwenyezi Mungu kama nikimwasi?

Walimwambia Swaleh kuwa wanashaka naye, naye akawaambia, hebu niambieni nifanyeje ikiwa nina uhakika kwamba Mwenyezi Mungu amenituma kwenu na akaniamrisha niwalinganie kwenye Tawhid; tena akanipa dalili za kutosha juu ya ujumbe huu, je, nimuasi kwa ajili ya kuwaridhisha nyinyi? Na ni nani atakayenikinga na adhabu yake kama nikimwasi?

Basi hapo hamtanizidishia isipokuwa hasara tu.

Kundi la wafasiri wamesema kuwa maana yake ni, nikiwatii mtanifanya nipate hasara. Na wengine wakasema kuwa ni, upinzani wenu haunizidishii chochote isipokuwa ni hasara yenu.

Tuonavyo sisi ni kuwa Swaleh alitaka kuwaambia watu wake lau atawakubalia, basi watamwamini, lakini yeye hatapata radhi ya Mwenyezi Mungu.

وَيَا قَوْمِ هَٰذِهِ نَاقَةُ اللَّهِ لَكُمْ آيَةً فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّهِ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ قَرِيبٌ {64}

Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu, ni ishara kwenu, basi mwacheni ale katia ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya isije ikawaangamiza adhabu iliyo karibu.

فَعَقَرُوهَا فَقَالَ تَمَتَّعُوا فِي دَارِكُمْ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ ۖ ذَٰلِكَ وَعْدٌ غَيْرُ مَكْذُوبٍ {65}

Wakamchinja. Basi (Swaleh) akasema: Stareheni katika mji wenu kwa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyokadhibishwa.

فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا نَجَّيْنَا صَالِحًا وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِنَّا وَمِنْ خِزْيِ يَوْمِئِذٍ ۗ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ {66}

Ilipofika amri yetu tulimwokoa Swaleh na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu kutokana na hizaya ya siku hiyo. Hakika Mola wako ni mwenye nguvu, mwenye kushinda.

وَأَخَذَ الَّذِينَ ظَلَمُوا الصَّيْحَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دِيَارِهِمْ جَاثِمِينَ {67}

Na ukelele ukawaangamiza wale waliodhulumu, wakapambaukiwa wameanguka kifudifudi katika majumba yao.

كَأَنْ لَمْ يَغْنَوْا فِيهَا ۗ أَلَا إِنَّ ثَمُودَ كَفَرُوا رَبَّهُمْ ۗ أَلَا بُعْدًا لِثَمُودَ {68}

Kama kwamba hawakuwemo humo. Ehee! Hakika Thamud walimkufuru Mola wao. Ehee! Thamud wamepotelea mbali.