read

Aya 69-73: Malaika Wanambashiria Ibrahim

Maana

Na wajumbe wetu walimjia ibrahim na bishara, wakasema: Salaam! Naye akasema: Salaam!

Wajumbe walikuwa ni Mlaika waliomjia Ibrahim (a.s.) kwa sura za kibinadamu, ili wampe habari njema ya kumzaa Ish-haq (a.s.). Walianza kwa maakuzi, naye akawarudishia mfano wake au zaidi. Mwenyezi Mungu ameashiria ugeni huu pale aliposema:

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ {24}

Je, imekufikia hadithi ya wageni waheshimiwa wa Ibrahim?” (51:24)

Hakukaa ila akaleta ndama aliyeokwa.

Ibrahim (a.s) alikuwa maarufu kwa ukarimu na kuwapenda wageni. Kwa hiyo aliharakisha kutayarisha ndama aliyechomwa kwa moto wa mbali, kwa kuangalia hali ya wageni. Ndama alikuwa amenona, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَرَاغَ إِلَىٰ أَهْلِهِ فَجَاءَ بِعِجْلٍ سَمِينٍ {26}

“Mara akaenda kwa watu wake akaleta ndama aliyenona” (51:26)

Alipoona mikono yao hamfikii, aliwatilia shaka na akawahofia.

Hawakuweza kula kwa sababu wao si watu. Kwahiyo Ibrahim akawahofia kwa sababu yeye aliwachukulia ni watu kumbe sivyo; na hajui wanataka nini. Mtu yeyote, awe Maasum (aliyehifadhiwa na dhambi) au la, akijiwa na jambao la ghafla asilolijua mwisho wake, lazima ahofie.
Malaika walipomuona hali yake Wakasema: Usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut, wala hatuna ubaya na wewe wala kaumu yako. Mahali pengine hofu imeelezwa:

Akasema:

إِنَّا مِنْكُمْ وَجِلُونَ {52}

“Hakika sisi tunawaogopa.” (15:52).

Na mkewe kasimama wima akacheka.

Kusimama ni kusikiliza mazungumzo yanayoendelea baina ya mumewe na Malaika. Ama kicheko, Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye. Kila mazungumzo kwa wanawake ni bashasha. Wafasiri wamegawanyika kuhusu hilo.

Tukampa bishara ya Is-haq na baada ya Is-haq, Ya’qub.

Yaani tukampa habari njema ya kumzaa Is-haq na Is-haq atamzaa Ya’qub. Hiyo inafahamisha kuwa mtoto wa mtoto ni mtoto.

Akasema: Miye! Hivi nitazaa na hali mimi ni kikongwe na huyu mume wangu ni mzee? Hakika hili ni jambo la ajabu!

Alistaajabu kwa vile si desturi mwanamke aliye katika umri wake kuweza kuzaa au mwanamume aliye katika umri wa mumewe kuweza kuzaa. Katika Kitabu cha kikiristo, Kutoka, imeelezwa kuwa Ibrahim wakati huo alikuwa na umri wa Miaka mia na mkewe, Sarah alikuwa na miaka tisini. Sisi hatukikubali Kitabu hicho. Tunalolifahamu ni kuwa wote wawili walikuwa wazee sana. Ama idadi ya miaka yao anayeijua ni Mungu.

Wakasema: Unastajabu amri ya Mwenyezi Mungu?

Vipi isiwezekane na yeye amri yake ni kukiambia kitu kuwa kikawa.

Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake iko juu yenu enyi watu wa nyumba hii.

Na amewahusu na neema nyingi. Na hii ni mojawapo. Kuna ajabu zaidi ya kuufanya moto uwe baridi na salama kwa Ibrahim?

Hakika yeye ni Mwenye kusifiwa Mwenye kutukuzwa.

Ni mwenye kusifiwa kwa sababu ana sifa njema ni mwenye kutukuzwa kwa sabubu ana ukarimu. Kwa hiyo siajabu kumpa anayemuomba na asiyemuomba na mwenye kutazamia na asiyetazamia.

فَلَمَّا ذَهَبَ عَنْ إِبْرَاهِيمَ الرَّوْعُ وَجَاءَتْهُ الْبُشْرَىٰ يُجَادِلُنَا فِي قَوْمِ لُوطٍ {74}

Basi hofu ilipomwondokea Ibrahim na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya watu wa Lut.

إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَحَلِيمٌ أَوَّاهٌ مُنِيبٌ {75}

Hakika Ibrahim alikuwa mpole, mwenye huruma, mwepesi wa kurejea (kwa Mungu).

يَا إِبْرَاهِيمُ أَعْرِضْ عَنْ هَٰذَا ۖ إِنَّهُ قَدْ جَاءَ أَمْرُ رَبِّكَ ۖ وَإِنَّهُمْ آتِيهِمْ عَذَابٌ غَيْرُ مَرْدُودٍ {76}

Ewe Ibrahim! Achana nayo haya. Hakika amri ya Mola wako imekwishakuja, na hakika wao itawafikia adhabu isiyorudishwa.