read

Aya 7-15: Yusuf Na Nduguze

Masilahi Kuliko Udugu

Binadamu ni mtumwa wa hisia zake, ni vigumu kuepukana nazo au kujipu- rukusha nazo. Kwa nini? Kwani inawezekana kukiepusha kitu na dhati yake? Kitu cha kwanza cha hisia hizi ni masilahi; yaani kutaka raha na kufukuza machungu. Maamuzi ya kufanya au kuacha jambo yanategemea masilahi.

Ama udugu si chochote ikiwa hauna raha au kuweka mbali machungu. Kwa hiyo kiwango cha pendo la mtu kwa jamaa zake linapimwa kwa masilahi haya. Mfano mzuri wa hilo ni kwamba huzuni na masikitiko ya kumpoteza ndugu yanakuja kutokana na kiwango cha alivyokuwa akinufaika naye wakati alipokuwa hai; kama ambavyo ndugu anaweza kuwa adui mkubwa akiwa anasababisha machungu au kuharibu raha na ladha.

Ni akina mama wangapi wamewaua watoto wao kwa sababu ya starehe tu?1 Ni watoto wangapi wamewaua wazazi wao kwa sababu ya kuharakisha mirathi? Qabil alimuua Habil nao ni ndugu waliotokamana na tone moja la manii na wakawa katika mfuko mmoja wa uzazi.
Wana wa israil walimtupa Yusuf kwenye shimo bila ya kuwa na hurumma ya udugu na damu moja.

Ndio Ali, Amirul mumin (a.s.) akasema: “ Udugu una haja kubwa zaidi ya mapenzi kuliko mapenzi kwenye udugu.” Hata mapenzi na urafiki chimbuko lake ni ladha ya roho, lakini mara nyingi mtu anjisahau na kusahau uhalisi wake, akaufanya udugu utokane na masilahi.

Kwa hiyo si dharura masilahi yawe ndiyo yanaupeleka utu. Kwani mtu safi aliye na ikhlas anaamini kwa kauli na vitendo kwamba masilahi yake ni masilahi ya jamii. Kwa hiyo anaumia ikiwa jamii inaumia na anafurahi ikiwa inafuraha. Anaona heri ni kuisimamisha haki na uadilifu.

Ama asiyekuwa hivyo basi haoni umuhimu ila umuhimu wake wala maisha isipokuwa maisha yake tu; kama walivyofanya wana wa israil kwa Yusuf ili wapate kupendwa wao na baba yao, lakini matokeo yake ni kuadhibiwa kwa kunyimwa na Mwenyezi Mungu hilo walilolitaka, wakastahiki hasira ya Mwenyezi Mungu na ya mtume wake Ya’qub na Yusuf akapata utukufu na cheo, wakasimama mbele yake wakiwa dhalili huku wakikiri makosa yao na kuomba msamaha kwa kusema: “Wallahi Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi na hakika sisi tulikuwa wenye makosa” Aya 91 ya sura hii.

Kwa hakika katika Yusuf na ndugu zake kuna ishara kwa wanaouliza.

Makusudio ya ishara hapa ni mazingatio na mafunzo.

Wana wa israil walimtupa Yusuf shimoni, si kwa lolote ila ni kwamba baba yao alikuwa akimpenda na kumhurumia zaidi. Maquraishi walimpiga vita Muhammad na wakafika kikomo cha kumuudhi, naye ni mquraishi mwenzao, kwa sababu tu Mwenyezi Mungu alimfanya bora kuliko wao na kuliko watu wote. Hata hivyo Mwenyezi Mungu alimnusuru Yusuf na ndugu zake na akamnusuru Muhammad na jamaa zake.

Katika hayo kuna mawaidha na mafunzo kwa wenye kutaka kujua uhakika na kufaidika nao.

Waliposema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi na hali sisi ni kikundi imara. Hakika baba yetu yumo katika upotevu dhahiri.

Maana ya Aya hii na inayoifuatia iko wazi, lakini pamoja na hayo tunaifuatilia kila Aya na yale yanayonasibiana nayo. Wana wa israil walipoona baba yao amelemea zaidi kwa Yusuf na ndugu yake, hasadi na chuki iliwachemka na wakaanza kuulizana: Kwa nini huyu mzee ameathirika na hawa watoto wawili na hali sisi ni wakubwa tena ni wengi wenye nguvu tulio na manufaana kumhudumia? Hakika huyu mzee amepotea.

Yusuf na nduguye, Benjamin, mama yao alikuwa mmoja, aliyeitwa Rachel. Mara nyingi hutokea chuki baina ya watoto kutokana na kuoa wake wengi.

Muuweni Yusuf au mtupeni nchi ya mbali uso wa baba yenu utawaelekea nyinyi.

Walikula njama ya kumuua si kwa chochote ila, ni kwa kutaka kuhodhi mapenzi ya baba yao; kama wanavyokiri wenyewe. Hii ndio mantiki ya wenye kuhodhi na kulimbikiza; ‘uwa na ufukuze’ hata kama ni ndugu wa damu, ili upate faida na chumo.

Na baada ya haya mtakua watu wema.

Wafasiri wanasema kuwa makusudi ya wema hapa ni wema wa dini; kwamba wao watatubia baada ya tendo lao hili ovu. Lakini dhahiri ya mfumo wa maneno inafahamisha kuwa makusudio ni kuwa wema kwa baba yao wao peke yao.

Akasema msemaji kati yao: Msimuue Yusuf, lakini mtumbukizeni ndani ya kisima, watamuokota baadhi ya wasafiri, ikiwa nyinyi ni wenye kufanya.

Katika Tawrat, Kitabu cha mwanzo 37:18-22, imesemwa kuwa aliyeyasema haya ni Reuben na ni ya yake ilikuwa ni kumtoa Yusuf kisimani baada ya kuondoka ndugu zake.

Wakasema: Ewe baba yetu! Mbona hutuamini kwa Yusuf na hakika sisi ni wenye kumnasihi, tunampenda na kumtakia kila la heri. Hivi ndivyo alivyo mwenye hadaa na vitimbi, kila mahali na kila wakati, ni mbwa mwitu katika ngozi ya kondoo.

Mpeleke kesho pamoja nasi afaidi na acheze, na bila shaka sisi tutamhifadhi.

Walijua kwamba baba yao anampenda Yusuf na anapenda afurahi na pia walijua jinsi alivyokuwa akimlinda sana. Kwa hiyo wakamwingilia kwa mlango huo huo. Yusuf anacheza huku wao wakimlinda na jambo lolote baya: ‘kikulacho kinguoni mwao.’

Akasema: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na ninahofia asije mbwa mwitu akamla nanyi mmeghafilika naye.

Aliwapa udhuru kwamba yeye hawezi kuachana na Yusuf. Hilo likawazidishia chuki. Pia aliwapa udhuru kwamba anahofia asiliwe na mbwa mwitu. Razi anasema juu ya udhuru huu: Ni kama mbaye amewatafutia hoja. Mithali inasema: “Balaa iliponzwa na ulimi”

Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na sisi ni kundi imara, basi hakika sisi tutakuwa kwenye hasara.

Mzee akaghurika na akawaachia Yusuf nao wakawa ni katika watu walio kwenye hasara.

Basi walipokwenda naye na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima, walilitekeleza hilo wakidhani kuwa wamepata yale waliyoyataka, lakini Yusuf alimkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yake naye akamlinda na ubaya wa hila walizozifanya.

Na tukampa wahyi bila shaka utakuja waambia jambo lao hili na hali hawatambui.

Mwenyezi Mungu alimtuliza moyo Yusuf kwamba wewe utaokoka kutokana na mitihani yako hii na kwamba utawapa habari ya hili walilolifanya bila ya kukutambua.

Baina Ya Watoto Wa Israil Na Watoto Wa Maulama

Kwa mnasaba huu mambo yanyonasibiana kati ya watoto wa maulama wa kidini na watoto wa Israil.

Watoto wa Israil walisema: “Hakika baba yetu yumo katika upotevu dhahiri.” Baadhi ya watoto wa mulama nao husema hivyo hivyo ikiwa wameambiwa na baba zao yale yasiyowapendeza hata kama ni maneno ya Mwenyezi Mungu.

Watoto wa Israil walisema: “Muuweni Yusuf au mtupeni nchi (ya mbali) uso wa baba yenu utawaelekea nyinyi”

Watoto wa maulama nao wanafanya hivyo hivyo. Wanawafanyia njama viongozi wazuri waliowaaminifu, wanawazushia mambo na kuwachafua ili nyuso za baba zao ziwaelekee wao. Wanawafanyia kazi mashetani wao kisha wanapata malipo kwa pesa za kigeni. Athari ikiwa kubwa zaidi na malipo nayo yanakuwa makubwa.

Watoto wa Israil walikuja na kanzu ya Yusuf “ina damu ya uongo” Kila siku baadhi ya watoto wa maulama wanakwenda na uzushi wanaowazushia watu wema, ili wao waonekani wazuri na waaminifu.

Watoto wa Isralil walikuja kwa baba yao “usiku wakilia” wakificha vitendo vyao kwa unafiki na machozi ya mamba.

Vile vile baadhi ya watoto wa maulama, mbele ya baba zao wanajifanya ni wacha Mungu wenye ikhlasi kwa uongo na ria.

وَجَاءُوا أَبَاهُمْ عِشَاءً يَبْكُونَ {16}

Wakaja kwa baba yao usiku wakilia.

قَالُوا يَا أَبَانَا إِنَّا ذَهَبْنَا نَسْتَبِقُ وَتَرَكْنَا يُوسُفَ عِنْدَ مَتَاعِنَا فَأَكَلَهُ الذِّئْبُ ۖ وَمَا أَنْتَ بِمُؤْمِنٍ لَنَا وَلَوْ كُنَّا صَادِقِينَ {17}

Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana mbio na tukamwacha Yusuf kwenye vitu vyetu, basi mbwa mwitu akamla. Na wewe hutatuamini, ijapokuwa tunasema kweli.

وَجَاءُوا عَلَىٰ قَمِيصِهِ بِدَمٍ كَذِبٍ ۚ قَالَ بَلْ سَوَّلَتْ لَكُمْ أَنْفُسُكُمْ أَمْرًا ۖ فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ وَاللَّهُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ {18}

Na wakaja na kanzu yake ina damu ya uongo, bali nafsi zenu zimewashawishi kutenda jambo, lakini subira ni njema. Na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayoyasema.

وَجَاءَتْ سَيَّارَةٌ فَأَرْسَلُوا وَارِدَهُمْ فَأَدْلَىٰ دَلْوَهُ ۖ قَالَ يَا بُشْرَىٰ هَٰذَا غُلَامٌ ۚ وَأَسَرُّوهُ بِضَاعَةً ۚ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِمَا يَعْمَلُونَ {19}

Ukaja msafara. Wakamtuma mchota maji wao. Akatumbukiza ndoo yake. Akasema: Ee habari njema! Huyu hapa mvulana! Wakamficha ili awe bidhaa. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayoyafanya.

وَشَرَوْهُ بِثَمَنٍ بَخْسٍ دَرَاهِمَ مَعْدُودَةٍ وَكَانُوا فِيهِ مِنَ الزَّاهِدِينَ {20}

Na wakamuuza kwa thamani duni kwa pesa za kuhisabiwa, na walikuwa hawana haja naye.
  • 1. Nimesoma kwenye gazeti kwamba mwanamke mmoja alikuwa na mpenzi wake na mtoto wake mdogo akiwa amelala naye. Mtoto alipolia yule mama akamnyonga. Vile vile nimesoma kwamba msichana mmoja alimuua baba yake kwa sumu, na alipoulizwa akasema: Nataka tubaki peke yetu nyumbani mimi na mpenzi wangu. Namna hii dini na dhamiri inaondoka yakija matamanio.